• HABARI MPYA

    Monday, March 30, 2009

    MVUA YAITIBULIA SIMBA TAIFA

    MVUA kubwa iliyonyesha kwenye baadhi ya maeneo Dar es Salaam jana, ilisababisha mchezo wa Ligi Kuu soka ya Vodacom Tanzania Bara kati ya Simba na Azam kuvunjika baada ya kuchezwa kwa dakika 45 za kipindi cha kwanza. Simba iliyokuwa ikiongoza kwa bao 1-0 hadi mchezo unavunjika itarudiana na Azam iliyopanda Ligi Kuu msimu huu, kwenye Uwanja huo huo, iwapo mvua haitanyesha tena. Tangu asubuhi jana, hali ya hewa ya Jiji la Dar es Salaam ilikuwa ya mvua, ingawa baadhi ya sehemu ilikuwa kubwa, huku maeneo mengine ilikuwa ya kawaida, ikiwamo eneo la Uwanja wa Uhuru lililopo wilayani Temeke. Hali hiyo ilifanya mchezo wa Simba na Azam kuchezwa lakini baadhi ya maeneo yakiwa na utelezi, ambao hata hivyo haukuwa wa kutisha kufanya pambano lisishindwe kufanyika. Hata hivyo hali ilibadilika uwanjani hapo kuanzia saa 10:40 alasiri, wakati wingu lilipotanda na dakika 15 baadaye mvua kubwa kuanza kunyesha, tukio lililotokea dakika mbili baada ya mwamuzi kupuliza filimbi kuashiria mapumziko. Ni kama mvua hiyo ilikuwa ikisubiri dakika 45 zimalizike, kwani karibu dakika zote za muda wa mapumziko, ilianza kunyesha kwa kasi kubwa na kusababisha maeneo mengi ya uwanja huo kuwa na madimbwi, hali ambayo ilizua hofu kama mchezo huo ungeweza kuendelea. Baada ya muda wa mapumziko kumalizika, huku uwanja huo ambao una nyasi za bandia ukiwa umejaa maji kwa sehemu kubwa na kuonyesha kila dalili kwamba mechi isingeweza kuendelea, baadhi ya mashabiki walivamia uwanja na kuanza kuyatoa maji ili mchezo uendelee. Mashabiki hao ambao wengi walikuwa wakitumia kandambili, kofia na makasha mbalimbali kukausha maji, walifanya kazi hiyo kwa ushirikiano mkubwa, lakini bado baadhi ya sehemu maji yalikuwa yamejaa, huku pia muda ukizidi kwenda, ingawa mvua iliacha kunyesha. Kutokana na hali hiyo mwamuzi wa mchezo huo, Amon Paul kutoka Mara, aliwaita manahodha wa timu zote mbili, Shekhan Rashid wa Azam na Nico Nyagawa wa Simba, ambapo baada ya kuzungumza nao kwa dakika chache, walifikia uamuzi wa kuvunja mchezo huo. Ingawa hadi jana jioni ilikuwa haijatolewa taarifa rasmi na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuhusiana na majaliwa ya mchezo huo, lakini kulingana na kanuni za ligi hiyo, mchezo huo utarudiwa leo. Baadhi ya mashabiki wa Simba, walionekana wakilalamika kuhusiana na uamuzi huo wa kuahirishwa mechi kwa madai kuwa maji yangekaushwa na mchezo ungeendelea. "Uamuzi wa kuvunja mechi umechukuliwa haraka, leo hawa walikuwa hawatoki, washukuru mvua," alisema Issa Said shabiki maarufu wa Simba. Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Nyagawa, Shekhan na mshambuliaji wa Simba, Emeh Izuchukwu, walidai walikuwa tayari mchezo uendelee, huku Shekhan akisisitiza kuwa kutokana na kwamba walishafungwa kuendelea ilikuwa lazima. Baadhi ya mashabiki wa Yanga, walikuwa wakiwakejeli Simba kwamba huwa wanajitamba mvua ikinyesha wanafanya vizuri, lakini jana iliwageuka. Mwaka 2001 katika michuano ya Kombe la Washindi Simba iliifunga Ismailia ya Misri mabao 2-0 katika mchezo uliofanyika Uwanja huo huo wakati huo ukijulikana kama Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, lakini baada ya dakika 45 kipindi cha kwanza mvua kubwa ilinyesha na kusabisha mchezo uvunjike na uliporudiwa siku iliyofuata Simba iliambulia kushinda 1-0, hivyo kutolewa, kwani ilihitaji kushinda 3-0 kutokana na kufungwa 2-0 kwenye mechi ya kwanza mjini Cairo. Katika mchezo wa jana, bao la Simba lilifungwa dakika ya 33 na Ramadhan Chombo 'Redondo' akimalizia kazi nzuri ya Ulimboka Mwakingwe, ambapo timu hiyo ingeweza kupata mabao mengi, lakini washambuliaji wake hawakuwa makini, hali ambayo pia iliikuta Azam, ambayo licha ya kupata nafasi chache lakini umaliziaji haukuwa mzuri. Simba inayoshika nafasi ya tano katika msimamo wa ligi ikiwa na pointi 27 ipo katika vita ya kuwania nafasi ya pili katika ligi hiyo ambayo itaiwezesha kucheza michuano ya Kombe la Shirikisho mwakani. Timu nyingine zinazowania nafasi hiyo ni Mtibwa Sugar, Prisons na Kagera Sugar zenye pointi 28 kila moja ila zinatofautiana uwiano wa mabao, ambapo zote zimebakisha michezo minne kumaliza ligi, wakati Simba bado michezo mitano. Naye John Nditi anaripoti kutoka Morogoro kuwa timu ya Polisi Moro, jana ilizidi kujiondoa katika balaa la kushuka daraja, baada ya kuifunga Toto African bao 1-0 Uwanja wa Jamhuri mjini humo. Bao hilo lilifungwa dakika ya 54 na beki wa Toto African Shaaban Aboma katika harakati za kuokoa, ambapo sasa Polisi imefikisha pointi 22, huku Toto African ikiwa na pointi 24.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MVUA YAITIBULIA SIMBA TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top