• HABARI MPYA

    Tuesday, March 10, 2009

    ARSENAL KUIVAA AS ROMA BILA ADEBAYOR


    Hapa wanataniana Adebayor (kushoto) na Ronaldo (kulia), lakini ukweli ni kwamba timu zao kesho zina kibarua kizito Ulaya


    LONDON, Uingereza
    KOCHA wa Arsenal, Arsene Wenger, amekiri kwamba timu yake itajitupa uwanjani kesho katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya AS Roma bila ya mshambuliaji wake mahiri, Emmanuel Adebayor.
    Arsenal kesho itakuwa na kazi ngumu ya kuendeleza ushindi wa bao 1-0 ilioupata katika mechi ya kwanza iliyokuwa nyumbani, ili kujihakikishia tiketi ya Robo Fainali ya michuano hiyo mikubwa barani Ulaya.
    Hata hivyo, harakati hizo za Arsenal kusaka tiketi ya Robo Fainali huenda zikakwama na sababu mojawapo ni kwamba Adebayor, mmoja wa washambuliaji mahiri, atakwenda Roma kama akiwa msafiri na si mchezaji.
    Adebayor hakuichezea Arsenal mechi mbili tangu aumie misuli katika mechi ya Ligi Kuu ya England dhidi ya Tottenham mwezi uliopita, huku matarajio ya kupona mapema yakiwa madogo. Hata hivyo, Wenger ana matumaini ya kumtumia beki wake, Kolo Toure, ambaye naye alikuwa majeruhi: "Kwa hakika Adebayor hatoweza kucheza, lakini nitasubiri ili nijue kuhusu Kolo kabla ya kuamua kikosi changu cha kwanza.
    "Tunakwenda katika mechi dhidi ya Roma tukiwa na matumaini ya kufanya vizuri na tunaamini tutafanya hivyo, jambo zuri ni kwamba hatujafungwa nyumbani, tunafahamu kwamba hatutocheza kwa kujihami tu, tutalazimika kushambulia na kujaribu kufunga," alisema.

    Ferguson kumfunga mdomo Mourinho?


    LONDON, Uingereza
    WAKATI, Manchester United ikiumana na Inter Milan kesho katika mechi ya kusaka tiketi ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, gumzo kubwa ni kwa makocha Jose Mourinho wa Inter na Sir Alex Ferguson wa Man United.
    Kubwa ambalo mashabiki wa Man United watapenda kulisikia baada ya mechi hiyo ni kuibuka na ushindi ambao utamfanya Mourinho awe kimya, kwani iwapo ataibuka mshindi atakachozungumza kinaweza kuongeza machungu kwa Man United.
    Mourinho na Ferguson huko nyuma waliwahi kuwa na historia ya kugombana na kupatana, kesho timu zao zinajitupa kwenye Uwanja wa Old Trafford zikisaka tiketi ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, baada ya kutoka sare ya bila kufungana katika mechi ya kwanza.
    Kugombana mara kwa mara kwa makocha hao kuliwahi kutokea wakati Mourinho akiinoa Chelsea na hata kufikia hatua ya kusuluhishana katika klabu ya pombe, lakini baada ya kikao cha kusuluhishana Mourinho aliibuka na kusema kwamba walikula pamoja mvinyo lakini mvinyo ulikuwa mchungu sana.
    "Tulikaa tukala mvinyo pamoja, lakini mvinyo ulikuwa mchungu, jamaa alikuwa analalamika kwa sana na nafikiri sasa nahitaji kumletea mvinyo kutoka Ureno ambao ni mtamu na bila shaka utamfanya asiwe mwenye kulalamika," alisema Mourinho katika hali ya dhihaka.
    Kesho, Ferguson ataingia uwanjani na kikosi chake akiwa katika mkakati wake wa kuibuka na ushindi ili kuendelea vyema na safari ya kulitetea taji hilo kwa kulitwaa mara ya pili mfululizo, wakati Mourinho atawania kuhakikisha anaiwezesha Inter kulibeba taji hilo kama alivyofanya mwaka 2004 akiwa na FC Porto ya Ureno.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: ARSENAL KUIVAA AS ROMA BILA ADEBAYOR Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top