• HABARI MPYA

    Saturday, March 14, 2009

    MGOSI AAPA KUFIA SIMBA


    MSHAMBULIAJI wa klabu ya Simba ya Dar es Salaam, Mussa Hassan Mgosi (pichani kushoto akiwa na Jabir Aziz), amesema kwamba kama atakosa timu ya kuchezea nje ya nchi, basi atachezea klabu yake hiyo hadi mwisho wa maisha yake.
    Akizungumza na DIMBA juzi mjini Dar es Salaam, Mgosi ambaye aling’ara kwenye Michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) iliyomalizika Jumapili iliyopita mjini Abidjan, Ivory Coast, alisema kwamba amepata wakala Msenegali, Said Chang, ambaye ameingia naye mkataba.
    Alisema wakala huyo amemuahidi kumpa taarifa juu ya wapi atakwenda kucheza kati ya nchi za Ufaransa, India, Norway na Falme za Kiarabu, ambako anamtafutia nafasi.
    “Ni kati ya hizo nchi nne, nasubiri, nadhani siku mbili hizi atanijulisha,” alisema Mgosi, ambaye baada ya michuano hiyo, ameteuliwa kwenye kikosi cha CHAN, akiwa katika orodha ya wachezaji wa akiba.
    Mgosi, ambaye ni mchezaji pekee wa Tanzania kuingia kwenye kikosi hicho, mafanikio yake yametokana na subira, nidhamu, kujituma na kusikiliza kwa makini maelekezo ya walimu.
    “Kama utakumbuka nilishapata nafasi mbili, mwaka 2005 nilikwenda Afrika Kusini katika klabu ya Meritzburg Classic, mambo hayakuwa mazuri, mwaka jana nikaenda Oman (Oman Club), pia mambo hayakuwa mazuri.
    Lakini sijakata tamaa, nimeendelea kuwa mchezaji mwenye dhamira fulani, inshaallah siku moja nitatimiza ndoto zangu,” alisema nyota huyo, aliyezaliwa Agosti 20, 1985 wilayani Moshi, mkoani Kilimanjaro.
    Mgosi, aliyepata elimu yake ya msingi katika shule ya Pasua, Moshi kabla ya kujiunga na Sekondari ya Makongo, Dar es Salaam, alisema pamoja na mafanikio hayo, hawezi kuvimba kichwa na kujiona amefika kwa sababu bado hajatimiza ndoto zake.
    “Mimi ninataka kucheza Ulaya siku moja, hizo ndizo ndoto zangu, ninachofanya hivi sasa ni kuongeza bidii na kufanyia kazi yale mapungufu yangu ambayo wataalamu wanayaona,” alisema mchezaji huyo, aliyemuoa Jasmin Elias, mwaka 2006 na kuzaa naye watoto wawili, Hassan na Nailat.
    Kabla ya kutua Simba mwaka 2005, Mgosi aliichezea Mtibwa Sugar ya Morogoro kwa msimu mmoja wa 2004, ambayo alijiunga nayo kutoka klabu iliyomuibua kisoka, JKT Ruvu, aliyoanza kuichezea 2001, akitokea sekondari ya Makongo.
    JKT ilivutiwa na Mgosi akiwa kwenye kikosi cha timu ya vijana chini ya umri wa miaka 17, enzi hizo kikinolewa na Mnigeria, Ernest Mokake (sasa marehemu). Baadaye alipandishwa timu ya chini ya miaka 20, kabla ya kuchukuliwa timu ya wakubwa, Taifa Stars mwaka 2005.
    Wakati wa usajili wa msimu huu, kocha wa Yanga, Dusan Kondic, alijaribu bila mafanikio kutaka kumsajili Mgosi sambamba na nyota mwingine wa Simba, beki Kelvin Yondani. Lakini alifanikiwa kuwapata kipa Juma Kaseja, mabeki Nurdin Bakari na George Owino.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MGOSI AAPA KUFIA SIMBA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top