• HABARI MPYA

    Saturday, March 14, 2009

    WAMISRI WAMSAKA NGASSA CAIRO


    Majuto Omary, Cairo
    MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania na Yanga, Mrisho Ngassa (pichani) amewapiga chenga ya mwili waandishi wa habari wa Misri waliokuwa wakimwinda baada ya kuwasili mjini hapa wakitaka kumhoji.
    Baada ya kumkosa licha ya kuwa na picha zake kadhaa, watangazaji wa kituo cha televisheni cha klabu ya Al Ahly, wapinzani wa Yanga walimnasa mshambuliaji Mkenya Boniface Ambani na kumhoji kwa muda ambapo aliwaeleza kuwa wao wamefika hapa kuiandika uopya historia ya soka ya Afrika.
    Baadaye waandishi hao waliwadaka beki Nurdin Bakari na kiungo Abdi Kassim ambaye ndiye nahodha wa Yanga na kuzungumzia mchezo wao wa kesho, ambao umekuwa gumzo kubwa katika mitaa na vyombo vya habari vya hapa.
    Hata hivyo, akizungumza na Mwananch, Ngassa alisema wao (Yanga) wamejiandaa kupambana na Al Ahly hadi dakika ya mwisho na kuweka historia mpya.
    Alisema kuwa wamekuja hapa kufanya kitu hasa kile waliochokidhamiria na watahakikisha kuwa wanawalazimisha wapinzani wao kucheza kama ambavyo wanataka wao.
    "Tunaujua umuhimu wa mechi hiyo ya kesho na ukweli kwamba sisi ni timu pekee ya Tanzania tunaoshiriki mashindano ya kimataifa.
    "Al Ahly ni timu wenye historia kubwa hapa Misri na Afrika kwa ujumla na hivyo umakini zaidi unatakiwa kila sehemu baada wanajua fitna za waamuzi katika mechi kama hizi.
    "Mabeki wetu inawabidi wacheze kwa uangalifu zaidi, maana nasikia hao Al Ahly ni wazuri kwa mipira ya faulo, sisi tutatakiwa zaidi kumiliki mpira na wao watataharuki kuona tunatawala mchezo," alieleza.
    Kiungo huyo mshambuliaji aliongeza kuwa kuwa wao watatumia zaidi uzoefu walioupata kwenye michuano ya Afrika (CHAN) iliyomalizika wiki jana ili kuhakikisha wanafanya vyema katika mechi hiyo ambayo imelifanya jiji la Cairo kuwa kimya huku magazeti yakimpamba zaidi kiungo mshambuliaji, Mohamed Abou Treika na Muangola, Flavio Amado katika kurasa zao za michezo kuwa ni 'visu' vyao dhidi ya Yanga.
    Hata hivyo, baadhi ya mashabiki wa soka wa hapa wamesema timu ya Al Ahly haina matokeo mazuri katika ligi kutokana na kuhamisha mawazo yote katika mchezo wao dhidi ya Yanga.
    Gazeti moja la hapa jana lilisema kuwa wanaijua Yanga kutokana na kupata mikanda mbalimbali ya michezo yao hivi karibuni ikiwamo ile dhidi ya Etoile d'Or Mirontsy ya Comoro.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: WAMISRI WAMSAKA NGASSA CAIRO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top