• HABARI MPYA

    Thursday, March 19, 2009

    YANGA KUJIHAKIKISHIA MICHUANO YA AFRIKA MWAKANI?

    KLABU ya Yanga jioni ya leo itashuka dimbani kwenye Uwanja wa Uhuru, zamani Taifa mjini Dar es Salaam kumenyana na Polisi Morogoro katika mfululizo wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara, inayodhaminiwa na Vodacom.
    Mabingwa watetezi wenye pointi 42, wanashuka dimbani wakiwa na machungu ya kipigo cha mabao 3 - 0 kutoka kwa Al- Ahly ya Misri kwenye mchezo wa awali, Raundi ya Kwanza, Ligi ya Mabingwa Afrika mjini Cairo Jumapili iliyopita.
    Watoto hao wa Mtaa wa Twiga na Jangwani watashusha dimbani silaha zao zote kwa dhamira ya kujipoza machungu ya Cairo na kutaka kutetea ubingwa wao mapema. Aidha, Yanga ikishinda mechi ya leo mbali na kujihakikishia kucheza michuano ya Afrika mwakani, pia itakuwa imebakiza pointi kutangaza ubingwa.
    Mchezo huo unatarajiwa kuwa wenye upinzani mkali licha ya Polisi Moro kuwa kati ya timu zilizo katika hatihati ya kushuka daraja.
    Pia, maafande hao wenye pointi 16 wapo katika wakati mgumu wa kutaka kubakia ligi kuu msimu ujao, hivyo mchezo wa leo unaonyesha kuwa na umuhimu zaidikwao ili waweze kushinda na kuanza kujinasua katika pango la kushuka daraja.
    Kocha wa Yanga, Dusan Kondic ambaye aliwatibua wachezaji na mashabiki kwa kauli yake mjini Cairo kuwa timu yake haiwezi kuishinda Ahly na kusonga mbele katika michuano ya Afrika, anatazamiwa kuweka kando kihoro hicho na kuelekeza nguvu zake katika mechi hiyo ya ligi kuu.
    Katika mchezo huo, Mserbia huyo anaweza kuendelea kumwamini kipa Mzungu Obren Curkovic au kumpa nafasi Juma Kaseja ili kulinda hadhi ya mabingwa hao.
    Katika ulinzi, anaweza kuwatumia mabeki, Nadir Haroub Cannavaro, Wisdom Ndhlovu, Shadrack Nsajigwa au pengine wale ambao hawakuikabili Ahly, Fred Mbuna, Abuu Mtiro ili kuwazuia washambuliaji wa Polisi Moro.
    Pia, anaye kiraka Nurdin Bakari ambaye anaweza kuwasaidia washambuliaji, Mrisho Ngassa, Ben Mwalala na viungo Athuman Iddi Chuji, Godfrey Bonny, Shamte Ally ili kuisumbua safu ya ulinzi ya Polisi.
    Pia, anao Jerry Tegete, Mike Barasa ambao wanaweza kusaidiwa na Gaudence Mwaikimba ili kuhakikisha timu yao inazidi kuchuma pointi na kuukaribia ubingwa mapema.
    Mshambuliaji kimara wa mabao, Boniface Ambani hatacheza leo kutokana na kushukia Nairobi wakati wakirejea kutoka Misri pamoja na beki wa timu hiyo, George Owino.
    Kocha wa Polisi, John Simkoko alisema mchezo huo utakuwa mgumu kwani unaikutanisha timu yake na moja ya timu bora nchini na hivyo kazi wanayo wachezaji wake.
    "Tuko katika hali mbaya na tunahitaji kujinusuru na hili panga la kushuka daraja,tunacheza na timu bora, hivyo mechi itakuwa ngumu kwetu, lakini tutapigana hadi mwisho.
    "Vijana wangu wako vizuri, wana ari na nimewaeleza kila mechi ina umuhimu kwetu ili kujiokoa, hivyo leo tutacheza kufa au kupona ili kuhakikisha tunashinda," alisema Simkoko.
    Yanga inaongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 42 inafuatiwa na Simba yenye pointi 27 sawa na Kagera Sugar, lakini zinazidia kwa mabao ya kufunga na kufungwa.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA KUJIHAKIKISHIA MICHUANO YA AFRIKA MWAKANI? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top