• HABARI MPYA

    Monday, March 09, 2009

    TFF YAANZA KUSAKA MRITHI WA TINOCCO


    Maximo (katikati) akiwa na Tinocco kushoto na Itamar Amorin aliyekuwa kocha wa viungo wa Stars, ambaye sasa yupo Azam FC


    KATIBU Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Frederick Mwakalebela amesema kwamba wameanza mchakato wa kutafuta kocha mwingine wa timu za taifa za vijana, baada ya aliyekuwa kocha wa timu hizo, Mbrazil Marcus Tinocco kuziacha kwenye mataa.
    Alisema wamewajibika kuanza mchakato huo mapema ili kumpata mwalimu atakayeziandaa timu hizo kwa ajili ya michuano ya Afrika Mashariki na Kati.
    Mwakalebela alisema katika mchakato huo wametoa kipaumbele zaidi kwa makocha wa kigeni ili kumpata mwalimu ambaye atawaongezea ujuzi nyota hao wa baadae ambao walianza kulelewa na Tinoco.
    ``Suala hili litashughulikiwa mapema sana, hatuna muda wa kulichelewesha, vijana wanatakiwa wajiandae na mashindano mbalimbali,`` aliongeza Mwakalabela ambaye pia alisema Kamati ya Mashindano ya shirikisho hilo itakutana kesho kufanya maandalizi ya mechi zilizobakia za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, itakayoanza tena Machi 13, mwaka huu baada ya kusimama tangu Februari mwanzoni.
    Kuhusu Kocha Mkuu wa timu ya taifa, Taifa Stars, Mbrazil, Marcio Maximo Mwakalebela alisema hatima yake itajulikana baada ya serikali kukukubaliana na dau ambalo kocha huyo anataka alipwe kabla ya kusaini mkataba mpya.
    Maximo pamoja aliyekuwa kocha wa timu ya taifa ya vijana, Marcus Tinoco walikuwa wakilipwa mishahara yao na serikali.
    Alisema licha ya kocha huyo kueleza kwamba hatma yake ya kuendelea kuifundisha iko mikononi mwa Watanzania, lakini suala la kumudu mshahara na huduma nyingine ambazo atakuwa amezieleza katika mkataba mpya ni jambo muhimu la kuzingatiwa.
    Mwakalebela alisema kuwa pande zote mbili zitakutana na kujadili mkataba huo na endapo watafikia makubaliano mazuri, kocha huyo atabaki nchini na kuendelea na kazi yake ya kuwanoa wachezaji.
    Alisema kuwa mchakato rasmi kuhusiana na mkataba huo umepangwa kuanza kufanyika mwezi Aprili na nafasi ya kwanza watampa Maximo kuelezea msimamo wake.
    ``Mkataba una mambo mengi, mara baada ya Maximo kurejea kutoka likizo kwao Brazil, tutakaa naye na kuzungumza ila hata kama tunamuhitaji na yeye akatoa dau litakalotushinda itakuwa si bahati yetu kuendelea kuwa naye,`` alisema Mwakalebela.
    Alisema kuwa wao ndio watu wa karibu wanaofanya nae kazi na hata alipomaliza mkataba wa awali, walimpendekeza kuwa aendelee kubaki nchini.
    Aliongeza kuwa katika kipindi chote ambacho Maximo alikuwa hapa nchini, kocha huyo ameweza kufanya kazi nzuri, alikuwa anapenda kushirikiana na pia ameweza kuipa timu mafanikio.
    Alisema kuwa hata pale ambapo ilionekana kuna tatizo, Maximo aliweza kukutana na viongozi wa shirikisho ili kuweza kupata ufumbuzi.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TFF YAANZA KUSAKA MRITHI WA TINOCCO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top