• HABARI MPYA

    Monday, July 08, 2019

    RASMI TFF ‘YAMTUPIA VIRAGO’ AMUNIKE BAADA YA TAIFA STARS KUBORONGA AFCON

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limemfuta kazi kocha Mnigeria wa timu ya taifa, Emmanuel Amunike baada ya Taifa Stars kufanya vibaya kwenye Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zinazoendelea nchini Misri kufuatia kufungwa mechi zote tatu za Kundi C.
    Taarifa ya TFF leo imesema kwamba wamefikia makubaliano ya pamoja na Amunike kusitisha mkataba baina yao.
    Aidha, TFF imesema kwamba itatangaza Kocha wa muda atakayekiongoza Taifa Stars katika mechi za kuwania tiketi ya Fainali za Ubingwa wa Mataifa wa Afrika (CHAN), zinazohusisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee.

    Baada ya kufungwa 2-0 na Senegal, 3-2 na Kenya na 3-0 na Algeria, Taifa Stars iliondoka Misri bila hata pointi moja, ikishika mkia kwenye Kundi C, nyuma ya jirani zao, Kenya waliovuna pointi tatu, huku Senegal iliyomaliza na pointi sita katika nafasi ya pili ikiungana na Algeria iliyokusanya pointi tisa kwenda hatua ya 16 Bora.
    Taifa Stars ya kocha Emmanuel Amunike imeshindwa kuvunja rekodi ya kikosi cha mwaka 1980 kilichoshiriki fainali hizo mjini Lagos, Nigeria ambacho angalau kiliambulia pointi moja baada ya sare na Ivory Coast ya 1-1, kikitoka kufungwa 2-1 na Misri na 3-1 na wenyeji, Nigeria.
    Na haikuwa ajabu Mnigeria huyo umri wa miaka 48, winga wa zamani wa Barcelona ya Hispania kuamua kujiuzulu wadhifa wake baada ya kikosi cha Taifa Stars kurejea nyumbani.
    Amunike aliyeng’ara na Super Eagles katika fainali za Kombe la Dunia mwaka 1994 nchini Marekani akicheza wingi ya kushoto, anaondoka baada ya kuiongoza Taifa Stars katika jumla ya mechi 10, ikishinda mbili tu, kufungwa sita na sare mbili.
    Taifa Stars imekuwa timu ya kwanza ya taifa ya wakubwa Amunike kufundisha, baada ya awali kuwa kocha wa timu ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ya kwao, Nigeria kuanzia mwaka 2014 hadi 2017.
    Zaidi ya hapo, Amunike mwenye umri wa miaka 47 alifundisha klabu za Al Hazm ya Saudi Arabia, kama Kocha Msaidizi mwaka 2008 kabla ya kuhamia Julius Berger hadi mwaka 2011 alipojiunga na Ocean Boys, zote za Nigeria.
    Alipoachana na U-17 ya Nigeria akaenda kufundisha Al Khartoum SC ya Sudan kuanzia mwaka 2017 hadi 2018 na sasa anakuja kuujaribu ‘mfupa’ uliowashinda wengi, Taifa Stars.   
    Kisoka, Amunike aliibukia klabu ya Concord mwaka 1990 kabla ya kwenda kuchezea Julius Berger 1991, zote za kwao, Nigeria baadaye Zamalek ya Misiri mwaka 1991 hadi 1994 ndipo akahamia Ulaya.
    Alianza na klabu ya Sporting CP ya Ureno kuanzia 1994 hadi 1996 kabla ya kuhamia Barcelona ambako alicheza hadi mwaka 2000 alipohamia Albacete zote za Hispania na mwaka 2003 alijiunga na Busan I'Cons ya Korea Kusini alikocheza hadi 2004 akahamia Al-Wehdat ya Jordan kumalizia soka yake.
    REKODI YA AMUNIKE TAIFA STARS
    1. Tanzania 0-0 Uganda (Kufuzu AFCON- Kampala)
    2. Tanzania 0-3 Cape Verde (Kufuzu AFCON – Praia)
    3. Tanzania 2-0 Cape Verde (Kufuzu AFCON – Taifa)
    4. Tanzania 0-1 Lesotho (Kufuzu AFCON – Maseru)
    5. Tanzania 3-0 Uganda (Kufuzu AFCON- Taifa)
    6. Tanzania 0-1 Misri (Kirafiki Alexandria)
    7. Tanzania 1-1 Zimbabwe (Kirafiki Cairo)
    8. Tanzania 0-2 Senegal (AFCON 2019) Cairo
    9. Tanzania 2-3 Kenya (AFCON 2019) Cairo

    10. Tanzania 0-3 Algeria (AFCON 2019) Cairo 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: RASMI TFF ‘YAMTUPIA VIRAGO’ AMUNIKE BAADA YA TAIFA STARS KUBORONGA AFCON Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top