• HABARI MPYA

    Tuesday, July 02, 2019

    DEO GRACIA KANDA MUKOKO NI MCHEZAJI MPYA WA SIMBA SC KUTOKA TP MAZEMBE

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    WINGA wa kimataifa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Deo Gracia Kanda Mukoko amesaini mkataba wa mwaka mmoja kujiunga na klabu ya Simba ya Dar es Salaam kutoka TP Mazembe ya Lubumbashi.
    Taarifa ya Simba SC leo imesema kwamba ni matarajio Kanda mwenye umri wa miaka sasa ataisaidia klabu kuendelea kufanya vizuri msimu ujao kutokana na uwezo na uzoefu wake mkubwa wa kucheza mashindano makubwa, ikiwemo Klabu Bingwa ya Dunia ya FIFA.
    Kanda anakuwa mchezaji mpya wa saba kusajiliwa Simba SC na wa tano wa kigeni, baada ya Wabrazil watatu, mabeki beki Gerson Fraga Vieira ATK ya Ligi Kuu ya India na Tairone Santos da Silva kutoka klabu ya Atletico Cearense FC, mshambuliaji, Wilker Henrique da Silva kutoka Bragantino, zote za Daraja la Nne nchini Brazil na kiungo Msudan Sharaf Eldin Shiboub Ali Abdalrahman.
    Mtendaji Mkuu wa Simba SC, Crescentius Magori (kushoto) akimtambulisha Deo Kanda baada ya kusaini 

    Wengine wapya ni wazawa wawili, ni kipa Beno Kakolanya kutoka Yanga SC ya Dar es Salaam na beki Kennedy Wilson Juma kutoka Singida United Ya Singida.
    Kanda alitua kwa mara ya kwanza Mazembe mwaka 2009 na alikuwemo kwenye kikosi cha timu hiyo kilichoshiriki klabu bingwa ya dunia ya FIFA mwaka 2010, kabla ya kuhamia Raja Casablanca ya Morocco mwaka 2013.
    Alicheza Morocco kwa msimu mmoja kabla ya mwaka 2014 kurejea nyumbani, DRC na kujiunga AS Vita alikocheza kwa msimu mmoja pia kisha akajiunga tena na Mazembe mwaka 2015 hadi sasa anatolewa kwa mkopo.
    Pamoja na kusaini wachezaji wapya, SImba SC pia imewapa mikataba mipya wachezaji wake kadhaa wa msimu uliopita, wakiwemo kipa Aishi Manula, mabeki Erasto Nyoni, Shomari Kapombe, Nahodha Msaidizi, Mohammed Hussein ‘Tshabalala, Muivory Coast, Serge Wawa Pascal viungo Jonas Mkude, Mzambia Clatous Chama na washambuliaji Nahodha Mkuu, John Bocco na Meddie Kagere raia wa Rwanda.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: DEO GRACIA KANDA MUKOKO NI MCHEZAJI MPYA WA SIMBA SC KUTOKA TP MAZEMBE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top