• HABARI MPYA

    Thursday, September 26, 2013

    YANGA WAMALIZANA NA NGASSA, HAENDI KOKOTE NA ATALIPIWA DENI AKIPIGE JANGWANI

    Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA SEPTEMBA 26, 2013 SAA 10:05 JIONI
    KIKAO cha mchana huu baina ya uongozi wa klabu ya Yanga ya Dar es Salaam na mshambuliaji Mrisho Khalfan Ngassa kimefikia mwafaka kuhusu deni la mchezaji huyo kwa klabu ya Simba SC, Sh. Milioni 45, imefahamika.
    Yanga SC italipa fedha hizo na Ngassa ataendelea kucheza katika klabu hiyo akiachana na mpango wa kwenda Oman, anakotakiwa na klabu moja ya huko, ambayo iko tayari kutoa kiasi cha Sh. Milioni 100, ambazo zingelipa deni la Wekundu wa Msimbazi na nyingine kulipwa Yanga ambao wana Mkataba naye kwa sasa.
    Hata hivyo, haijajulikana Ngassa atailipaje fedha hizo Yanga, baada ya awali kuwapo kwa habari juu ya namna mbili, kwanza kukatwa mshahara na nyingine kuongezewa Mkataba.
    Huyu wetu tu; Mrisho Ngassa (katikati) akiwa na Mjumbe wa Baraza la Wadhamini la Yanga SC, Francis Kifukwe kulia na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya klabu, Mussa Katabaro kushoto. Kijana anabaki Jangwani.

    Awali, Ngassa aligoma kusaini Mkataba wa kulipiwa deni hilo kwa kuhofia kurudia kosa alilofanya kusaini Mkataba na Simba SC ambao hakuuelewa.
    Ngassa alishituka na kugoma kusaini Mkataba huo wa kulipiwa deni, hadi kwanza aupeleke kwa Wakili wake akaupitie, chanzo kilisema jana. “Unajua Simba walimuambia anasaini kukubali kucheza kwa mkopo, kumbe anasaini Mkataba mpya, sasa amekuwa mjanja sana sasa hivi,”kilisema chanzo. 
    Chanzo hicho kilisema kwamba, Yanga ilitaka kumlipia Ngassa deni na kuongeza miaka miwili katika Mkataba wake kutoka miwili ya sasa, lakini yeye mwenyewe mchezaji amependekeza alipiwe deni hilo na baada ya hapo atakuwa anakatwa kwenye mshahara wake.
    Baada ya suluhu hiyo, Ngassa sasa anaweza kuanza kuichezea Yanga SC katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Jumamosi dhidi ya Ruvu Shooting, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Ikumbukwe Ngassa alifungiwa mechi sita za mashindano kwa kosa la kusaini Mikataba na timu mbili, Simba na Yanga SC. Pamoja na adhabu hiyo aliyomalizia Jumapili, Ngassa alitakiwa kurejesha fedha alizochukua Simba SC Sh. Milioni 30 pamoja na fidia ya Sh Milioni 15, jumla Milioni 45.
    Sakata la Ngassa linaanzia Agosti mwaka jana alipoukera uongozi wa iliyokuwa klabu yake, Azam FC kwa kwenda kubusu jezi ya Yanga SC baada ya kufunga bao la ushindi katika Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame dhidi ya AS Vita ya DRC, Uwanja wa Taifa.
    Baada ya kuiwezesha Azam, kutinga fainali ya michuano hiyo kwa ushindi wa 2-1, uongozi ulimuamuru kocha Stewart Hall asimpange mchezaji huyo kwenye fainali dhidi ya Yanga SC, lakini akakaidi na kumpanga na timu ikafungwa.
    Kilichofuatia, Azam FC iliamua kutangaza kumuuza mchezaji huyo kwa mkopo na Simba SC wakashinda tenda hiyo, wakati Stewart alifukuzwa na kwenda Sofapaka ya Kenya. Mserbia, Boris Bunjak aliajiriwa Azam, lakini hata kabla ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu msimu uliopita akafukuzwa na Stewart akarejeshwa kazini.
    Ngassa aligoma kuuzwa bila idhini yake, lakini Simba SC wakaketi naye mezani na kufikia makubaliano, kabla ya kumtangaza rasmi kujiunga na klabu hiyo. Baadaye Simba SC ikasema ilimuongezea Mkataba mchezji huyo na kumpa Sh. Milioni 30, wakati yeye mwenyewe anasema alipewa fedha hizo, ili akubali kucheza kwa mkopo.
    Yanga SC wakaamini maneno ya Ngassa na alipomaliza muda wake wa kuitumikia Simba SC kwa mkopo kumalizia Mkataba wake na Azam, akasaini kurejea Jangwani.
    Hata hivyo, TFF ikabaini mchezaji huyo alisaini Simba SC pia hivyo kumfungia mechi sita na kumtaka arejeshe Sh. Milioni 30 na fidia ya Sh. Milioni 15.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: YANGA WAMALIZANA NA NGASSA, HAENDI KOKOTE NA ATALIPIWA DENI AKIPIGE JANGWANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top