• HABARI MPYA

    Thursday, September 19, 2013

    YANGA WADAI WACHEZAJI, SEIF MAGARI NA BIN KLEB CHANZO CHA MATOKEO MABAYA YA TIMU LIGI KUU

    Na Mahmoud Zubeiry, Mbeya, IMEWEKWA SEPTEMBA 19, 2013 SAA 1:48 ASUBUHI
    WANACHAMA na wapenzi wa Yanga SC walioongozana na timu mjini hapa, wameanza kukata tamaa juu ya mwenendo wa timu hiyo katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya sare tatu mfululizo, wakisema mambo mawili makubwa, wachezaji kutojituma na mgawanyiko ndani ya uongozi.
    Baada ya sare ya tatu mfululizo ya 1-1 na Prisons mjini hapa jana, kama ilivyokuwa dhidi ya Coastal Union Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na Mbeya City Uwanja wa Sokoine mjini hapa, baadhi ya wanachama waliangua kilio uwanjani.
    Wakiondoka kinyonge Uwanja wa Sokoine, walikuwa wakiwalaumu wachezaji wao kutojituma, kwamba imesababisha timu kuambulia pointi tatu ndani ya mechi tatu.
    Mbona hamuonekani? Seif Magari kushoto akikumbatiana na swahiba wake Abdallah Bin Kleb baada ya kukamilisha usajili wa Mrisho Ngassa. Mwingine kulia ni Mussa Katabaro. 

    Lakini pia walikuwa wakisema, kitendo cha kutengwa kwa mfanyabiashara Seif Ahmad ‘Magari’ nacho kinaweza kuwa kinachangia matokeo hayo.
    Wanadai Seif ni rafiki mkubwa wa Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya klabu yao- Abdallah Ahmed Bin Kleb, hivyo kumpoteza mmoja wao ni sawa na kuwapoteza wote.
    Wamestaajabu Bin Keb kutoonekana katika mechi za karibuni za timu hiyo kwa taarifa za kuwa kwenye safari za kibiashara wakati si kawaida yake na wanahisi hali hiyo kwa kiasi kikubwa inachangia matokeo mabaya. 
    Wanachama hao wameingiwa hofu pia juu ya mchezo wao ujao dhidi ya Azam FC Jumapili Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwamba nao unaweza kuleta matokeo mabaya.
    Hamjitumi? Wachezaji wa Yanga SC jana Uwanja wa Sokoine 

    “Timu iondoke hapa Alhamisi, itafika Dar es Salaam usiku na wachezaji wamechoka. Sasa tazama, Ijumaa na Jumamosi siku mbili tu ujiandae kucheza na Azam?”alihoji Paulina, mmoja wa wanachama waliosafiri na timu kutoka Dar es Salaam.
    Yanga SC imeambulia pointi sita tu katika mechi nne za mwanzo wa msimu, ikishinda 5-1 dhidi ya Ashanti United na kufuatiwa na sare tatu mfululizo za 1-1 dhidi ya Coastal, Mbeya City na Prisons.
    Baada ya mechi jana kocha wa Yanga SC, Mholanzi, Ernie Brandts hakutaka hata kuzungumza na Waandishi wa Habari, wakati mpinzani wake, Jumanne Chale wa Prisons alisema timu yake ingeweza kushinda kama ingetumia vizuri nafasi ilizozipata. 
    Nimrudishe Seif? Mwenyekiti wa Yanga SC, Yussuf Manji yupo katika wakati mgumu hivi sasa kutokana na timu kufanya vibaya

    Chale akawazungumzia Yanga akisema kwamba ni timu inayofungika, kwa sababu katika uchezaji wake inaacha mianya ya wazi ya wapinzani kupita na akajutia sare hiyo.
    Jerry Tegete alitangulia kuifungia Yanga SC dakika ya 37 jana akiunganisha krosi maridadi ya winga Simon Msuva kabla ya Michael Peter kuisawazishia Prisons dakika ya 77 akiunganisha krosi ya Omega Seme anayecheza kwa mkopo kutoka Jangwani.  
    Yanga SC ilicheza vizuri zaidi kipindi cha kwanza na kupoteza nafasi mbili nzuri za kufunga mabao zaidi dakika ya tatu, Didier Kavumbangu alipowababatiza mabeki shuti kali baada ya kupokea krosi ya Simon Msuva na Jerry Tegete dakika ya saba aliwatoka vizuri mabeki wa Prisons, lakini akapiga nje.
    Kipindi cha pili, Prisons walibadilika nao kuanza kushambulia langoni mwa Yanga na kwa ujumla katika ngwe hiyo timu zilishambuliana kwa zamu na mchezo ulikuwa mkali baada ya matokeo kuwa 1-1.
    Yanga walionekana kupigana zaidi kusaka bao la ushindi, lakini Prisons walisimama imara kuzuia na kushambulia pia na dakika ya 87 almanusra Prisons wapate bao la pili baada ya Ibrahim Isihaka kupiga kichwa juu kidogo ya lango kufuatia krosi ya Julius Kwanga.    
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: YANGA WADAI WACHEZAJI, SEIF MAGARI NA BIN KLEB CHANZO CHA MATOKEO MABAYA YA TIMU LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top