• HABARI MPYA

    Wednesday, September 25, 2013

    KIMWAGA AMEWASILISHA UJUMBE, BILA MIKAKATI THABITI, AKADEMI YA AZAM HAITAKUWA NA FAIDA

    IMEWEKWA SEPTEMBA 25, 2013 SAA 12:20 ASUBUHI
    JINA Joseph Kimwaga limeteka mazungumzo na mijadala mingi kuhusu soka ya Tanzania kwa sasa- kufuatia kinda huyo kuifungia bao la ushindi Azam FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Jumapili dhidi ya Yanga SC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Kimwaga aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya kinda mwenzake, Farid Mussa alipigiwa mpira mrefu dakika ya 90 akamzidi mbio Mbuyu Twite na kumhadaa Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kabla ya kufumua shuti kumtungua kipa Ally Mustafa ‘Barthez’ kuifanya Azam ishinde 3-2.

    Hata Farid aliyeanza alicheza vizuri sana na alisaidia mno Azam kushambulia langoni mwa Yanga akimpita mara kadhaa Mbuyu Twite na kutia krosi nyingi. Kwa ujumla wachezaji wote hawa wamesifiwa sana baada ya mechi ya Jumapili.
    Lakini ajabu, Kimwaga na mwenzake pamoja na kufanya vizuri siku hiyo, hawakuwa chaguo la kocha Muingereza Stewart John Hall kucheza mechi hiyo, bali waliingizwa kwenye programu za mchezo huo kwa shinikizo la Wakurugenzi wa timu, ambao wanaheshimu uwezo wao.
    Kufuatia Azam FC kulazimishwa sare ya 1-1 na timu dhaifu, Ashanti United katikati ya wiki iliyopita, na kuonekana kabisa wachezaji hawakucheza kwa kujituma, Wakurugenzi walimuamuru Stewart kuanza kuwatumia wachezaji wa kikosi cha pili, Azam Akademi. 
    Pamoja na Stewart kuonekana kutokuwa na imani na makinda wa Akademi, lakini alishinikizwa na akaambiwa awaweke kando wachezaji wote ambao walionekana dhahiri kucheza bila kujituma dhidi ya Ashanti United.
    Na katika mchezo huo dhidi ya Yanga SC wachezaji wa kudumu wa kikosi cha kwanza cha Azam FC kama Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na Khamis Mcha ‘Vialli’ hawakuwepo hata benchi, badala yake makinda Kimwaga na Farid walichukua nafasi. 
    Farid alianza na kucheza vizuri wingi ya kushoto akimpita mara kadhaa Mbuyu Twite na kutia krosi nyingi maridadi kabla ya kumpisha ‘mshindi wa mechi’, Kimwaga dakika ya 72 akaenda kuwamaliza Yanga SC.
    Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Dominic Nyamisana, aliyesaidiwa na Charles Simon na Flora Zablon wote wa Dodoma, hadi mapumziko, Azam walikuwa mbele kwa bao 1-0.
    Bao hilo lilifungwa na John Bocco ‘Adebayor’ sekunde ya 34 tu, baada ya kuuwahi mpira uliorudishwa na beki Kevin Yondan kufuatia pigo la kichwa la Brian Umony na kuutumbukiza nyavuni. 
    Yanga SC inayofundishwa na Mholanzi, Ernie Brandts, ilikuja juu baada ya bao hilo na kufanya mashambulizi mengi langoni mwa Azam, lakini hadi dakika 45 za kwanza zinamalizika hawakufanikiwa kupata bao.
    Lakini kipindi cha pili, Yanga walirudi na moto mkali na kufanikiwa kusawazisha bao dakika ya 48 kupitia kwa Mrundi, Didier Kavumbangu aliyeutokea mpira mrefu na kwenda kumchambua kipa wa Azam, Aishi Manula.  
    Yanga iliongeza kasi ya mashambulizi langoni mwa Azam na kufanikiwa kupata bao la pili, dakika ya 65 mfungaji Hamisi Kiiza aliyemalizia pasi ya Simon Msuva.
    Beki Kevin Yondan aliunawa mpira kwenye eneo la hatari dakika ya 68 na Kipre Herman Tchetche akaenda kufunga kwa penalti dakika ya 69 na kufanya 2-2.
    Azam waliokoa shambulizi la hatari langoni mwao na kuanzisha shambulizi la haraka- na mchezaji bora wa michuano ya Kombe la Uhai msimu uliopita, Kimwaga hakufanya makosa- hadi mwisho Azam 3-2 Yanga.
    Simon Msuva anaingia katika msimu wa tatu kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na wa pili katika klabu ya Yanga SC tangu asajiliwe kutoka Moro United. Msuva ni mchezaji tegemeo wa Yanga SC kwa sasa na pia mchezaji wa timu ya taifa, Taifa Stars.
    Lakini Msuva ametokea Azam Akademi na alikuwa pamoja na Kimwaga kwenye timu hiyo. Tena, Kimwaga alikuwa mchezaji anayeng’ara na kufanya vizuri kuliko Msuva. Pamoja na hayo, Kimwaga ndiyo anaanza kucheza Ligi Kuu, wakati mwenzake anakaribia kuanza kuambiwa ‘mzee’.
    Ndiyo, soka ya Tanzania baada ya misimu mitatu, mchezaji anaanza kuitwa mzee na kupigwa mizengwe apotee- sasa huko ndiko anakoelekea Msuva. Kitakachomfanya Msuva aheshimike ni kulinda na kukuza kiwango chake, vinginevyo atakiona cha moto.  
    Mudathir Yahya ni kiungo chipukizi wa Azam ambaye kwa sasa ameanza kukomazwa katika kikosi cha Taifa Stars. Baada ya kuanza kuitwa Stars tangu msimu uliopita, sasa amepandishwa pia kikosi cha kwanza cha Azam ingawa hajaaminiwa kucheza.
    Huyu Mudathir ameibuka pamoja na Seif Abdallah Karihe visiwani Zanzibar, lakini mwenzake anaingia katika msimu wa pili Ligi Kuu, huku yeye akisubiri kucheza mechi ya kwanza ya ligi hiyo wakati wowote chini ya kocha Stewart. Azam ilivutiwa na Seif baada ya kumuona aking’ara Ruvu Shooting msimu uliopita, ingawa tangu amefika Chamazi, amekuwa hatumiki mara nyingi.
    Kuna uwekezaji mkubwa katika akademi ya Azam- kuna wachezaji wameiva mno kucheza Ligi Kuu, lakini hawapati nafasi ya kupanda kikosi cha kwanza. Matokeo yake wachezaji kama Msuva waliamua kuondoka na wametimiza ndoto zao.
    Ibrahim Jeba pia alikimbilia Simba SC, baada ya kuona muda wa kucheza umefika, lakini bado hajaanza kupewa nafasi, ingawa baadaye Azam ilipambana ikamrejesha. Uwekezaji wa akademi ya Azam ni mkubwa sana, lakini utakuwa hauna manufaa yoyote kama hakutakuwa na mipango endelevu kwa ajili ya vijana.
    Kama Msuva ambaye alionekana bado Azam, alikwenda kucheza Moro United Ligi Kuu hadi kuivutia klabu kubwa kama Yanga, basi wapo wengi wengine, ambao wanaweza kwenda kucheza Mbeya City, Ashanti United, Kagera Sugar kukuza vipaji vyao.
    Wapo wengi ambao wanaweza kwenda kucheza hata Ligi Daraja la Kwanza timu mbalimbali nchini kukuza vipaji vyao. Wapo wengi ambao wanaweza kwenda kucheza hata Ligi Kuu ya Zanzibar kukuza viwango vyao.
    Azam FC isiwe na ndoto tu za kusubiri Mamilioni ya Pauni kwa kuuza wachezaji Ulaya, bali ifikirie hata kuanza kupata fedha kidogo kwa kuuza wachezaji humu nchini, hata kuwatoa kwa mikopo, na baadaye inaweza kuja kuwauza kwa bei nzuri waking’ara huko wanakocheza.
    Hakuna sababu ya kumlaumu Stewart kwa nini hakuwaamini Kimwaga na Mussa, wakati ni yeye aliyemwamini kipa kutoka akademi, Aishi Manula na sasa anadaka mechi kubwa kama dhidi ya Yanga SC. Kinachotakiwa kwa sasa ni kutengeneza mikakati ya kuendeleza vipaji vinavyozalishwa pale Chamazi, kwani hata Ulaya ni hivyo pia- wachezaji wa akademi za Manchester United, Arsenal wanacheza klabu mbalimbali nchini humo.
    Mfano ni Fraizer Lee Campbell, anayechezea Cardiff City katika Ligi Kuu ya England, ambaye awali alichezea Manchester United, Royal Antwerp, Hull City, Tottenham Hotspur na Sunderland.
    Mshambuliaji huyo aliyezaliwa Septemba 13, mwaka 1987 ni zao la akademi ya Manchester United. Baada ya kucheza mechi nne za kikosi cha kwanza bila kufunga mabao, msimu wa 2006–2007, akapelekwa kwa mkopo Royal Antwerp ya Ubelgiji, ambako alifunga mabao 24 katika mechi 38. Akapelekwa pia kwa mkopo Hull City na Tottenham Hotspur, ambako alifunga mabao 15 katika mechi 37 klabla ya kuuzwa moja kwa moja Sunderland mwanzoni mwa msimu wa 2009–2010 kwa Pauni Milioni 3.5. 
    Akiwa Sunderland alishindwa kung’ara kutokana na kusumbuliwa na maumivu, lakini baada ya kuuzwa Cardiff Januari mwaka huu kwa Mkataba wa miaka mitatu na nusu, naye sasa ni kati ya washambuliaji wa kuogopwa Ligi Kuu ya England. Sasa ni takriban miaka mitano tangu ujio wa akademi ya Azam, wazi wachezaji wengi wamezalishwa pale na wengine wapya kila siku wanaingia, lakini vipi maendeleo yao? Niishie hapa kwa leo. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: KIMWAGA AMEWASILISHA UJUMBE, BILA MIKAKATI THABITI, AKADEMI YA AZAM HAITAKUWA NA FAIDA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top