• HABARI MPYA

    Wednesday, September 25, 2013

    NGASSA AGOMA KUSAINI HATI YA YANGA SC KUMLIPIA DENI LA SIMBA SC, APATA BONGE LA OFA UARABUNI

    Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA SEPTEMBA 25, 2013 SAA 10:35 JIONI
    MRISHO Khalfan Ngassa amepata timu ya Oman inayotaka kumnunua kutoka Yanga SC pamoja na kulipa deni la Simba SC, Sh. Milioni 45, lakini uongozi wa klabu yake kama unamuwekea kauzibe hivi.
    Habari za ndani ambazo BIN ZUBEIRY imezipata juu ya sakata la Ngassa na Yanga ni kwamba, mchezaji huyo amepata timu inayotaka kumnunua moja kwa moja, ikiwa tayari kutoa kiasi cha Sh. Milioni 100, ambazo zitalipa deni la Simba na nyingine kulipwa Yanga ambao wana Mkataba naye kwa sasa.
    Hata hivyo, wakati Yanga ikimzuia Ngassa kwenda Oman, nayo inaonekana kusuasua kumilipia deni la Simba SC. 
    Habari zinasema Yanga wametaka kumsainisha Ngassa Mkataba wa kumlipia deni, lakini amegoma kuusaini kwa kuhofia kurudia kosa alilofanya kusaini Mkataba na Simba SC ambao hakuuelewa.
    Mpenzi wa Yanga; Mrisho Ngassa amegoma kusaini kichwakichwa fomu za kulipiwa deni

    “Ngassa ameshituka sasa hivi, amegoma kusaini huo Mkataba wa kulipiwa deni, kwanza hadi aupeleke kwa Wakili wake akaupitie. Unajua Simba walimuambia anasaini kukubali kucheza kwa mkopo, kumbe anasaini Mkataba mpya, sasa amekuwa mjanja sana sasa hivi,”kilisema chanzo. 
    Chanzo hicho kimesema kwamba, Yanga inataka kumlipia Ngassa deni na kuongeza miaka miwili katika Mkataba wake kutoka miwili ya sasa, lakini yeye mwenyewe mchezaji amependekeza alipiwe deni hilo na baada ya hapo atakuwa anakatwa kwenye mshahara wake.
    Hadi sasa Ngassa hajasaini hati aliyotakiwa kusaini alipiwe deni hilo, maana yake kuna hatari akashindwa kuanza kucheza Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Jumamosi dhidi ya Ruvu Shooting, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Ikumbukwe Ngassa alifungiwa mechi sita za mashindano kwa kosa la kusaini Mikataba na timu mbili, Simba na Yanga SC. Pamoja na adhabu hiyo aliyomalizia Jumapili, Ngassa alitakiwa kurejesha fedha alizochukua Simba SC Sh. Milioni 30 pamoja na fidia ya Sh Milioni 15, jumla Milioni 45.
    Ukweli uko wapi? Ngassa akisaini Mkataba wa Simba SC mbele ya Hans Poppe, mwenyewe anadai hapa alikuwa anajua anasaini kukubali kucheza kwa mkopo Msimbazi. 

    Sakata la Ngassa linaanzia Agosti mwaka jana alipoukera uongozi wa iliyokuwa klabu yake, Azam FC kwa kwenda kubusu jezi ya Yanga SC baada ya kufunga bao la ushindi katika Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame dhidi ya AS Vita ya DRC, Uwanja wa Taifa.
    Baada ya kuiwezesha Azam, kutinga fainali ya michuano hiyo kwa ushindi wa 2-1, uongozi ulimuamuru kocha Stewart Hall asimpange mchezaji huyo kwenye fainali dhidi ya Yanga SC, lakini akakaidi na kumpanga na timu ikafungwa.
    Kilichofuatia, Azam FC iliamua kutangaza kumuuza mchezaji huyo kwa mkopo na Simba SC wakashinda tenda hiyo, wakati Stewart alifukuzwa na kwenda Sofapaka ya Kenya. Mserbia, Boris Bunjak aliajiriwa Azam, lakini hata kabla ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu msimu uliopita akafukuzwa na Stewart akarejeshwa kazini.
    Kutambulishwa Msimbazi; Aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Simba SC, Geoffrey Nyange 'Kaburu' akimkabidhi Ngassa jezi ya Simba Agosti mwaka jana

    Aling'ara Msimbazi; Ngassa alicheza jumla ya mechi 27 na kufunga mabao saba Simba SC pamoja na kutoa pasi 15 za mabao 
    Ngassa aligoma kuuzwa bila idhini yake, lakini Simba SC wakaketi naye mezani na kufikia makubaliano, kabla ya kumtangaza rasmi kujiunga na klabu hiyo. Baadaye Simba SC ikasema ilimuongezea Mkataba mchezji huyo na kumpa Sh. Milioni 30, wakati yeye mwenyewe anasema alipewa fedha hizo, ili akubali kucheza kwa mkopo.
    Yanga SC wakaamini maneno ya Ngassa na alipomaliza muda wake wa kuitumikia Simba SC kwa mkopo kumalizia Mkataba wake na Azam, akasaini kurejea Jangwani.
    Hata hivyo, TFF ikabaini mchezaji huyo alisaini Simba SC pia hivyo kumfungia mechi sita na kumtaka arejeshe Sh. Milioni 30 na fidia ya Sh. Milioni 15.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: NGASSA AGOMA KUSAINI HATI YA YANGA SC KUMLIPIA DENI LA SIMBA SC, APATA BONGE LA OFA UARABUNI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top