• HABARI MPYA

    Friday, September 27, 2013

    NGASSA AWAPA NENO HILO SIMBA SC...WE ACHA TU!

    Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA SEPTEMBA 27, 2013 SAA 12:30 JIONI
    MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mrisho Khalfan Ngassa amewaambia neno moja zito Simba SC- kwamba fedha si kitu bali utu ndiyo jambo la maana kwa wanadamu.
    Ngassa amesema hayo jioni ya leo ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Ilala, Dar es Salaam baada ya kulipa deni la Sh. Milioni 45 za Simba SC, ambalo sasa linamfanya awe huru kucheza Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    “Mpira ni mchezo wa furaha, hela (fedha) si kitu, kikubwa ni utu, mradi utu wangu mimi hawajauona na nimeisaidia Simba kwa kiasi kikubwa, poa, lakini pamoja na yote sina bifu nao. Ila isipokuwa michezo ni furaha, na mimi nachukulia hii kama changamoto tu,”alisema Ngassa.
    Ngassa alifungiwa mechi sita za mashindano na TFF baada ya kubainika alisaini mikataba na timu mbili, Simba na Yanga SC. Pamoja na hayo, mshambuliaji huyo alitakiwa kurejesha fedha alizodaiwa kuchukua kusaini Mkataba wa Simba SC, Sh. Milioni 30 na fidia ya Sh. Milioni 15, ambazo amelipa jioni hii jumla ya Sh. Milioni 45.
    Hela si kitu; Ngassa amewasilisha hundi zenye thamani ya Sh. Milioni 47 kuilipa Simba SC na kuwaambia fedha si kitu, bali utu ni ubinadamu.

    Akizungumzia kusimama kwake kucheza mashindano akitumikia adhabu yake hiyo, Ngassa alisema haijamuathiri na zaidi imempa muda zaidi wa kupumzika baada ya kumaliza msimu uliopita.
    “Kiwango kushuka au kutoshuka ni mtu mwenyewe jinsi unavyojitunza wakati ambao hauchezi, na kwa ujumla jinsi ambavyo unavyojiweka kisaikolojia, mimi niko sawa na zaidi kupumzika kwa muda fulani, inanipa nguvu ya kurudi na moto zaidi,”alisema.
    Kuhusu mlipaji wa deni hilo, kama ni yeye au Yanga, Ngassa amesema; “Katika suala la fedha, nimelipa mwenyewe, kwa hiyo kama kuna mwanachama ambaye ameguswa, anaweza kunisaidia kupoza machungu, lakini sio kama uongozi ndio uliotoa, ni mimi mwenyewe fedha zangu ndiyo nimetoa,”amesema.
    Alipoulizwa ni fundisho gani alilolipata baada ya tukio zima hilo, Ngassa amesema; “Nawashauri wachezaji wenzangu kwamba, wanapoingia mikataba na klabu, wahakikishe wanakuwa na mawakili, ili wawasaidie kujua kilichomo ndani yake na wasaini mikataba ambayo wanaielewa,”. 
    “Kilichotokea kwangu, kwa Simba ni wamefoji tu, lakini mimi sina bifu nao wala nini, kwa sababu mpira ni mchezo wa furaha, hela si kitu, kikubwa ni utu,”alisema.
    Akizungumzia kurejea kwake kazini baada ya kukosa mwanzo wa msimu, Ngassa alisema. “Narudi kuisaidia timu yangu, nina imani itarudi katika nafasi yake,”.
    Pamoja na hayo, Ngassa amekiri ushindani mkubwa wa namba uliopo ndani ya Yanga kwa sasa kutokana na timu kusheheni wachezaji wengi bora.
    “Changamoto ni kubwa, na kila mchezaji ana uwezo wa kucheza, kikubwa kila mtu akicheza akifanya vizuri, timu inashinda, hilo ndilo kubwa. Nikicheza mimi nikafunga, siyo kama mimi ndiyo nimeshinda, bali ni timu ndiyo imeshinda, hivyo hivyo kwa yeyote akifunga, imeshinda timu,”alisema.
    Sakata la Ngassa linaanzia Agosti mwaka jana alipoukera uongozi wa iliyokuwa klabu yake, Azam FC kwa kwenda kubusu jezi ya Yanga SC baada ya kufunga bao la ushindi katika Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame dhidi ya AS Vita ya DRC, Uwanja wa Taifa.
    Baada ya kuiwezesha Azam, kutinga fainali ya michuano hiyo kwa ushindi wa 2-1, uongozi ulimuamuru kocha Stewart Hall asimpange mchezaji huyo kwenye fainali dhidi ya Yanga SC, lakini akakaidi na kumpanga na timu ikafungwa.
    Kilichofuatia, Azam FC iliamua kutangaza kumuuza mchezaji huyo kwa mkopo na Simba SC wakashinda tenda hiyo, wakati Stewart alifukuzwa na kwenda Sofapaka ya Kenya. Mserbia, Boris Bunjak aliajiriwa Azam, lakini hata kabla ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu msimu uliopita akafukuzwa na Stewart akarejeshwa kazini.
    Ngassa aligoma kuuzwa bila idhini yake, lakini Simba SC wakaketi naye mezani na kufikia makubaliano, kabla ya kumtangaza rasmi kujiunga na klabu hiyo. Baadaye Simba SC ikasema ilimuongezea Mkataba mchezaji huyo na kumpa Sh. Milioni 30, wakati yeye mwenyewe anasema alipewa fedha hizo, ili akubali kucheza kwa mkopo.
    Yanga SC wakaamini maneno ya Ngassa na alipomaliza muda wake wa kuitumikia Simba SC kwa mkopo kumalizia Mkataba wake na Azam, akasaini kurejea Jangwani.
    Hata hivyo, TFF ikabaini mchezaji huyo alisaini Simba SC pia hivyo kumfungia mechi sita na kumtaka arejeshe Sh. Milioni 30 na fidia ya Sh. Milioni 15.     
    Ngassa alijiunga na Yanga SC kwa mara ya kwanza mwaka 2007 akitokea Kagera Sugar ya Bukoba na baada ya misimu mitatu akahamia Azam FC, ambako mwaka jana alivuruga na kuuzwa kwa mkopo Simba, kabla ya kurejea rasmi Jangwani, miezi mitatu iliyopita.
    Ngassa sasa anatarajiwa kuanza kuichezea Yanga SC kesho katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Ruvu Shooting, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: NGASSA AWAPA NENO HILO SIMBA SC...WE ACHA TU! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top