• HABARI MPYA

    Saturday, September 28, 2013

    HANS POPPE ATAKA KUMBURUZA NGASSA MAHAKAMANI

    Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA SEPTEMBA 28, 2013 SAA 4:35 ASUBUHI
    KAPTENI wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Zacharia Hans Poppe amempa onyo kali, mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mrisho Khalfan Ngassa, akimuambia akirudia kusema Simba SC walifoji Mkataba wake, atamburuza Mahakamani.
    Hans Poppe ambaye ni Mjumbe Mteule wa Kamati ya Utendaji na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya klabu hiyo, amemuambia Ngassa kama jana alisema kwa bahati mbaya, basi asikosee tena kusema Wekundu wa Msimbazi walifoji Mkataba wake.
    “Mimi ndiye niliyesaini naye Mkataba huyu kijana, sasa anaposema Simba SC walifoji ina maana mimi ndiye niliyefoji? Haya maneno kama kasema kwa bahati mbaya, asirudie tena, akithubutu kurudia nitamburuza Mahakamani na sitakuwa na ‘msalie mtume’,”alisema.
    Mimi nimefoji? Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe akisaini Mkataba na Ngassa Agosti mwaka jana.

    Ngassa jana alikaririwa na vyombo vya Habari akisema kwamba Simba SC ilifoji Mkataba wake, ikimuambia anasaini kucheza kwa mkopo kumalizia Mkataba wake wa Azam, lakini kumbe ni Mkataba mpya wa kuichezea klabu hiyo baada ya ule wa mkopo.
    Akizungumza jana jioni ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Ilala, Dar es Salaam baada ya kulipa deni la Sh. Milioni 45 za Simba SC, ambalo sasa linamfanya awe huru kucheza Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Ngassa alisema fedha si kitu, bali utu ndio bora.
    “Mpira ni mchezo wa furaha, hela (fedha) si kitu, kikubwa ni utu, mradi utu wangu mimi hawajauona na nimeisaidia Simba kwa kiasi kikubwa, poa, lakini pamoja na yote sina bifu nao. Ila isipokuwa michezo ni furaha, na mimi nachukulia hii kama changamoto tu,”alisema Ngassa.
    Ngassa alifungiwa mechi sita za mashindano na TFF baada ya kubainika alisaini mikataba na timu mbili, Simba na Yanga SC. Pamoja na hayo, mshambuliaji huyo alitakiwa kurejesha fedha alizodaiwa kuchukua kusaini Mkataba wa Simba SC, Sh. Milioni 30 na fidia ya Sh. Milioni 15, ambazo amelipa jana jumla ya Sh. Milioni 45.
    Pamoja na hayo, Ngassa aliwashauri wachezaji wenzake kuwa makini wanapotaka kuingia Mikataba na klabu ili yasije yakawakuta kama yaliyomkuta yeye
    “Nawashauri wachezaji wenzangu kwamba, wanapoingia mikataba na klabu, wahakikishe wanakuwa na mawakili, ili wawasaidie kujua kilichomo ndani yake na wasaini mikataba ambayo wanaielewa,”. 
    “Kilichotokea kwangu, kwa Simba ni wamefoji tu, lakini mimi sina bifu nao wala nini, kwa sababu mpira ni mchezo wa furaha, hela si kitu, kikubwa ni utu,”alisema.
    Sakata la Ngassa linaanzia Agosti mwaka jana alipoukera uongozi wa iliyokuwa klabu yake, Azam FC kwa kwenda kubusu jezi ya Yanga SC baada ya kufunga bao la ushindi katika Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame dhidi ya AS Vita ya DRC, Uwanja wa Taifa.
    Baada ya kuiwezesha Azam, kutinga fainali ya michuano hiyo kwa ushindi wa 2-1, uongozi ulimuamuru kocha Stewart Hall asimpange mchezaji huyo kwenye fainali dhidi ya Yanga SC, lakini akakaidi na kumpanga na timu ikafungwa.
    Kilichofuatia, Azam FC iliamua kutangaza kumuuza mchezaji huyo kwa mkopo na Simba SC wakashinda tenda hiyo, wakati Stewart alifukuzwa na kwenda Sofapaka ya Kenya. Mserbia, Boris Bunjak aliajiriwa Azam, lakini hata kabla ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu msimu uliopita akafukuzwa na Stewart akarejeshwa kazini.
    Ngassa aligoma kuuzwa bila idhini yake, lakini Simba SC wakaketi naye mezani na kufikia makubaliano, kabla ya kumtangaza rasmi kujiunga na klabu hiyo. Baadaye Simba SC ikasema ilimuongezea Mkataba mchezaji huyo na kumpa Sh. Milioni 30, wakati yeye mwenyewe anasema alipewa fedha hizo, ili akubali kucheza kwa mkopo.
    Yanga SC wakaamini maneno ya Ngassa na alipomaliza muda wake wa kuitumikia Simba SC kwa mkopo kumalizia Mkataba wake na Azam, akasaini kurejea Jangwani.
    Hata hivyo, TFF ikabaini mchezaji huyo alisaini Simba SC pia hivyo kumfungia mechi sita na kumtaka arejeshe Sh. Milioni 30 na fidia ya Sh. Milioni 15.     
    Ngassa alijiunga na Yanga SC kwa mara ya kwanza mwaka 2007 akitokea Kagera Sugar ya Bukoba na baada ya misimu mitatu akahamia Azam FC, ambako mwaka jana alivuruga na kuuzwa kwa mkopo Simba, kabla ya kurejea rasmi Jangwani, miezi mitatu iliyopita.
    Ngassa sasa anatarajiwa kuanza kuichezea Yanga SC leo katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Ruvu Shooting, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: HANS POPPE ATAKA KUMBURUZA NGASSA MAHAKAMANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top