• HABARI MPYA

    Sunday, August 11, 2013

    MANJI AWAAMBIE WANA YANGA NA SUALA LA UJENZI WA UWANJA WA KISASA LIMEFIKIA WAPI?

    IMEWEKWA AGOSTI 11, 2013 SAA 1, 30 ASUBUHI
    KWA kutumia mamlaka yake Kikatiba, Mwenyekiti wa klabu ya Yanga SC, Alhaj Yussuf Mehboob Manji ameitisha Mkutano wa dharula ambao utafanyika Agosti 18, mwaka huu ukumbi wa PTA, Saba Saba, Dar es Salaam, kujadili suala la Mkataba wa haki za matangazo ya Televisheni katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Yanga SC wamepinga Mkataba ulioingiwa kati ya Bodi ya Ligi Kuu na kampuni ya Azam TV, zaidi kwa sababu zao binafsi, ikiwemo chuki zao dhidi ya Azam kwa kitendo cha kumuuza kwa mkopo kwa wapinzani wao, Simba SC mshambuliaji Mrisho Ngassa badala ya kuwauzia wao (Yanga SC).

    Ngassa amemaliza Mkataba wake Simba SC na sasa amejiunga tena na Yanga SC, ingawa Wekundu wa Msimbazi, wanasema bado wana Mkataba naye na suala lake sasa litaamuliwa na TFF.
    Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeingilia kati mzozo huo kwa kuwa wao ndio wenye soka yao na kuwaambia Yanga- vema wakatae kusaini Mkataba, mechi zao za nyumbani hazitarushwa, lakini za ugenini ambazo  ni haki ya wapinzani wao, zitarushwa.
    Kwa hili, Yanga SC ndiyo wanapeleka suala hilo katika Mkutano Mkuu, yaani hawataki kabisa mechi zao zirushwe hata za ugenini kwa kuwa hawajasaini Mkataba kwa matakwa yao wenyewe.
    Viongozi wakuu wa Yanga SC sina shaka juu ya kiwango chao cha elimu, lakini hapa linakuja suala la uelewa katika suala husika- wanaweza kuwa wana hoja za msingi kwa mitazamo yao juu ya kukataa Mkataba wa Azam TV, lakini baada ya klabu zote 13 kuusaini, hawatakuwa na haki katika mechi zao za ugenini.
    Asilimia kubwa ya mechi za Yanga kwa ujumla zitachezwa Dar es Salaam kwa kuwa timu nyingi zinatumia Uwanja wa Taifa, ukiondoa mechi saba tu dhidi ya Coastal Union na Mgambo JKT (Mkwakwani, Tanga), Mbeya City na Prisons (Sokoine, Mbeya), Rhino FC (Ally Hassan Mwinyi, Tabora), Mtibwa Sugar (Jamhuri, Morogoro) na Kagera Sugar (Kaitaba, Bukoba).
    Mechi tano za ugenini dhidi ya Simba SC, Azam FC, JKT Ruvu na Ashanti United, Ruvu Shooting zote zitachezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kuonyeshwa bila kipingamizi, hivyo kutengeneza idadi ya mechi 12 za mabingwa hao kuonyeshwa kwa msimu pamoja na zile saba za ugenini.
    Bado unaweza kuona pamoja na Yanga SC kukataa kusaini Mkataba, lakini mechi zake 13 za msimu mzima zitaonyeshwa. Hapana shaka Mkutano wa Agosti 18, utalijadili kwa kina suala hilo.
    Ikumbukwe Manji aliingia madarakani, Julai 14, mwaka jana katika uchaguzi mdogo kuziba nafasi za viongozi waliojiuzulu akiwemo Mwenyekiti, Wakili Lloyd Baharagu Nchunga na Makamu wake, Davis David Mosha.
    Miezi mitano tangu aingie madarakani, Desemba mwaka jana Manji akatoa ahadi ya kuijengea klabu hiyo Uwanja wa kisasa na Januari akamtaja mkandarasi, Kampuni ya Beijing Constructions Engineering Group iliyojenga Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwamba ndiye atakayejenga Uwanja huo mpya wa Yanga.
    Baadaye, mwaka huu kampuni hiyo ikawasilisha ramani za viwanja kadhaa, Yanga SC iachague moja, ili zoezi la ujenzi wa Uwanja huo lianze.
    Kwa mujibu wa makubaliano hayo, ujenzi huo wa Uwanja utakaokuwa na uwezo wa kuchukua mashabiki 30,000 hadi 40,000 ulipangwa kuanza rasmi Juni, mwaka huu- na leo Agosti 11 ni zaidi ya miezi miwili zoezi hilo halina hata dalili za kuanza.
    Ikumbukwe pia, Manji alitangaza mpango wa kulikarabati na jengo dogo la klabu hiyo, liliopo Mtaa wa Mafia na kuwa jengo la kitegauchumi la klabu, akaunda Kamati chini ya Mwenyekiti, Ridhiwani Kikwete kusimamia zoezi hilo na huko pia hakuna taarifa zozote za maendeleo yake.
    Hadithi za ujenzi wa Uwanja mpya Yanga SC, ukarabati wa jengo la Mafia sasa ni maarufu masikioni mwa wengi, zikisimuliwa na wasimulizi tofauti kuanzia enzi za akina Tarimba Abass wanaongoza klabu hiyo.
    Na zimeendelea hata wakati wa uongozi uliopita wa Mwenyekiti, Wakili Lloyd Baharagu Nchunga, lakini suala la utekelezaji wake ndilo limekuwa gumu.
    Kuna sababu za kumuamini Manji, kwa sababu kila ukiitazama Yanga ya leo, bila ya yeye ngumu kupata picha ingekuwaje.
    Manji aliingia Yanga mwaka 2006 baada ya jitihada zilizofanywa na wanachama wa klabu hiyo akina Theonist Rutashoborwa (sasa marehemu), Mzee wa Mpunga, Mawakili Lugaziya na Matunda na baadhi ya Waandishi wa Habari za michezo wenye mapenzi na klabu hiyo, kuanzisha harambee ya Saidia Yanga, kufuatia hali mbaya ya kiuchumi kukithiri ndani ya klabu hiyo, chini ya uongozi wa Francis Kifukwe.
    Katika kutafuta misaada ya kuibeba timu wakati huo ipo kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame ndipo wakampata Manji naye kwa mapenzi yake, akasema; “Nitaubeba mzigo wote”, na kweli hadi leo, amekuwa akiilea Yanga tangu kama mfadhili hadi sasa Mwenyekiti.
    Hadi sasa, Manji ameingia kwenye historia Yanga kama miongoni mwa watu muhimu kuwahi kutokea kwenye klabu hiyo, bila hata ya ahadi ya Uwanja. Bila shaka hata wana Yanga pia na Watanzania wengi wanamuamini na kumuheshimu Manji.
    Ahadi hii ya Uwanja kwa kiasi kikubwa imebeba mustakabali wa heshima ya Manji mbele ya Yanga SC na kipimo cha ahadi zake nyingine ndani na nje ya klabu na pia kipimo cha uadilifu wake kwa ujumla. Miezi miwili mbele sasa tangu wana Yanga waambiwe ujenzi utaanza, lakini hakuna lolote na wala Mwenyekiti huyo hajatoa taarifa yoyote juu ya kukwama kwa zoezi hilo.
    Nini maana yake? Ameweza kulivalia njuga suala la kupita tu la Azam TV kiasi cha hadi kuliitia Mkutano Mkuu, wakati suala la msingi kama hilo la maendeleo ya klabu, kitu ambacho ndiyo kiu ya wana Yanga wengi wenye akili zao timamu, amekaa kimya!
    Naam, wakati umefika sasa Manji awape taarifa za maendeleo ya mradi wa ujenzi wa Uwanja wa kisasa wa klabu na si vibaya akafanya hivyo katika Mkutano wake wa dharula Agosti 18, pamoja na suala la Azam TV, pia awaambie wana Yanga amefikia wapi katika suala la ujenzi wa Uwanja wa klabu? Eid Mubarak. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: MANJI AWAAMBIE WANA YANGA NA SUALA LA UJENZI WA UWANJA WA KISASA LIMEFIKIA WAPI? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top