• HABARI MPYA

    Saturday, July 20, 2013

    HAYA NDIYO YANATUKWAMISHA MICHUANO YA KIMATAIFA KILA SIKU

    NI swali gumu kidogo japo, linaonekana jepesi kwa majibu ya mkato. Ukiangalia kiufundi, timu yetu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars sio mbaya na ni ya ushindani wa kweli pamoja ya kupoteaza mechi dhidi ya Morocco na Ivory Coast.
    Jasho liliwatoka wapinzania, ukizingatia Morocco walikuwa nyumbani na sehema ya magoli yao yametokana na mipira ya adhabu ikiwemo penalty. 

    Ukizingatia pia, wengi wa wachezaji wetu ni wafupi, hili nalo ni tatizo mojawapo, kwa hiyo huu ni udhaifu wetu au wa wachezaji wetu, hata pale zinapopigwa kona, sehemu kubwa ya mashabiki hushikilia mioyo yetu.
    Na utaona baada ya wachezaji kuokoa wanasema, afadhali hasa tunapokuwa tumetangulia kufunga goli, lakini mara zote pamoja na ufupi wao, wanajituma kuruka juu kuliko wapinzani wao.
    Nakubali timu yetu ni bora, kinachowashinda zaidi ni uzoefu, tunakutana na timu zenye wachezaji wengi wanaocheza Ulaya kwenye mafunzo bora zaidi na vifaa, , sasa tufanye nini na hawa ndio wachezaji wetu?
    Kwanza ni kweli wakati mwingine wanacheza rafu pasipo sababu, la pili eneo la robo uwanja upande wa goli letu, wachezaji wanapaswa kutumia nguvu kistaarabu, yaani bila madhara, tatu mtu mwenye kasi na uchu wa kufunga mabao huonekana kuanzia katikati, hakuna sababu ya kusubiri hadi anaingia katika eneo la hatari.
    Kingine, tunapaswa kuwaanda watoto na kuwachagua wakiwa na miaka 8 hadi 12, maumbo makubwa yanaonekana na yanajulikana, kuwatengea shule yao wawe wanasoma masomo ya kawaida na soka tu, wanakaa bweni wanapa mazoezi ya nguvu, ufundi, mbinu na kucheza na mpira kwa ustadi.
    Si kwamba Tanzania wachezaji wenye maumbo makubwa hawapo, wapo sana, kwa sababu Waafirika tunafanana, lakina sina maana wafupi na wenye vipaji wasipewe nafasi, la hasha inategemea na nafasi uwanjani, hasa zile za pembeni wanazoeshwa wakiwa wadogo, haya ni malengo yya muda mrefu.
    Kwa hili la vijana, wahusika wakuu ni klabu na watu binafsi kama kile kituo cha Arusha kwa sasa ingawa ile si shule ni kituo tu na wengi wa watoto wake wanaanzia umri wa miaka 14 na kuendelea.
    Serikali na TTF wanaandaa sera, taratibu na usimamiaji pia kuwasaidia hata kuwatafutia wataalamu na wafadhili ndani na nje, kwa hiyo watu waelewe ushindi wa timu ya taifa hautengenezwi mwezi au siku, ni mchakato wa muda mrefu unaowahusisha watu binafsi, vikundi, makampuni, vyama nya mpira na  Serikali.
    Kingine kinachotukwamisha ni hila na hujuma zinazofanywa na timu tunazokutana nazo kwenye viwanja vyao vya nyumbani, tunaathiriwa kuanzia Uwanja wa ndege watazusha zogo na kutuchanganya kisaikolojia kama siyo kwa wachezaji, basi ule msafara wa watu waliokwenda nao, ili mradi mtoke mmekasirika.
    Wanafanya makusudi kabisa, ili kuwaondolea wachezaji wetu hali ya kufikiria mchezo na kujikuta wanajawa na jazba mapema, kama Stars walivyofanyiwa Morocco hivi karibuni, hadi kupuliziwa dawa kwenye vyumba vya kubadilishia nguo.
    Wahusika hapa ni TFF, wanatakiwa kwenda mapema kufanya ukaguzi wa kina mpaka njia ya kupitia, lazima pia iwe na kakitengo ka intellejensia kuipeleleza timu pinzani na tabia zao wanapokuwa uwanjani kwa pia hata tabia za mashabiki wao na hali ya usalama katika uwanja wao wanaokwenda.
    Kwa upande wetu, nasi tumekuwa wapole mno hakuna timu si za taifa wala vilabu vilitoka na malalamiko ya hujuma kwa hiyo huwa wanacheza kama wapo nyumbani ndio maana tunafungwa kirahisi kwenye Uwanja wetu wa nyumbani, sina maana nasi tuwafanyie fuja la hasha, ila jua watalaamu wa saikolojia wanaliweza hili bila kuwanyima huduma muhimu kwa hili naomba niishie hapa.
    Kingine, marefa hawa nao wamekuwa wahanga wetu wa muda mrefu nakumbuka hapo Uwanja wa taifa tukicheza na Cameroon, Danny Mruwanda kawatoka mabeki amebaki na kipa alisukumwa akadondoka chini na refa alipeta kwa uhakika ingekuwa upande wao, angetoa penalti, tukio lingine tuliwahi kupata penalti na Mauritus, Emamanuel Gabriel alipiga penalti akafunga, refa akaamuru arudie na akarudia akakosa.
    Nafikiri huo ndio ulikuwa mchezo wake wa mwisho kwa Emmanuel Gabriel Taifa Stars. Hapa sina jibu la moja kwa moja kwa nini sisi, kwa sababu yapo matukio ya wazi ya upendeleo, achana na hizo penalti nayo ni mifano tu matukio ni mengi mno.
    Sababu nyingine sisi tunaojiita wachambuzi wa soka, tunakuwa si wazalendo, tunawakatisha wachezaji tama, tena mnasubiri wengine tumepoteza mchezo, tunaanza nilijua hatufiki mbali, huwezi kupambana na Ivory Coast, nilijua hamuendi Brazil, tumefugwa na Morocco na tuna mechi ya muhimu sana na Ivory Coast uwanja wa nyumbani, eti mchambuzi anaongea hayo, jamani mashinadano ni vita tunatakiwa tushikamane vyombo vyote vya habari, mitandao, mashabiki na viongozi- wimbo wetu ni mmoja, kuwa mpinzani wetu hatoki basi.
    Kwa mfano hata mchezo wetu na Gambia una umuhimu sana katika kulinda nafasi katika viwango vya FIFA pia ni fursa kwa wachezaji wetu kucheza Ulaya badala ya kuwaelimisha wachezaji na mashabiki juu ya hilo tunashadadia tunaenda kukamilisha ratiba, hii siyo sahihi.
    Hata kuwa washindi wa pili katika kundi ni sifa, mashindano mengine unaweza usianzie hatua za awali kama tulivyoanzia kipindi hiki.
    Hapa kuna umuhimu wa serikali yetu kuingiza somo la uzalendo katika mitaala yetu kuanzia msingi hadi chuo kikuu, hatukatai kukosoa basi kuwe na staha sio kishabiki na kukatishana tamaa.
    Zipo sababu nyingi sana, hizo kwangu mimi ni kubwa zaidi ila innapenda kushauri klabu zetu nazo ndio wadau wakubwa ili timu ya Taifa ifanikiwe lazima tuwe na klabu imara sana na ligi yenye ubora, wajenge shule na za michezo kwa mazingira yetu ni vigumu kuwa na timu za vijana bila shule mfano shule ipo Kunduchi, atoke saa 9 au 10 mazoezi Msimbazi au Jangwani na nyumbani Mbezi na nauli hapewi na mzee anapingana naye kuhusu kucheza mpira hapa unapata mchezaji gani?
    Mwisho Serikali ikishirikiana na TFF kuna sababu ya kuwekeza kwa dhati kabisa katika michezo kuzalisha wataalamu, ujenzi wa miundombinu ikiwemo kuboresha viwanja na ujenzi wa viwanja vipya.
    Pia tuanze kufanya tafiti za kina kabisa kwenye michezo kupata majawabu yasio na shaka, nahisi watu wanahisi hakuna sababu ya kufanya utafiti kwenye michezo, la hasha hakuna mafanikio katika nyanja yoyote bila utafiti, ndio maana tuna suluhu za kubahatisha na majawabu ya muda mfupi.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: HAYA NDIYO YANATUKWAMISHA MICHUANO YA KIMATAIFA KILA SIKU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top