• HABARI MPYA

    Tuesday, July 30, 2013

    AZAM FC WAPAA JUMAMOSI KWENDA AFRIKA KUSINI KUWEKA KAMBI YA KUJIANDAA NA MSIMU

    Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA JULAI 30, 2013 SAA 2:44 ASUBUHI
    AZAM FC inatarajiwa kuondoka nchini mchana wa Jumamosi kwa ndege ya Shirika la Afrika Kusini, kwenda Johanesburg, Afrika Kusini kuweka kambi ya wiki mbili kujiandaa na msimu mpya.
    Timu hiyo yenye maskani yake, Chamazi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, itaondoka na kikosi chake kizima kasoro wachezaji wawili tu majeruhi, kiungo Mkenya, Humphrey Mieno na mshambuliaji Mganda, Brian Umony.
    Meneja wa Azam FC, Jemadari Said ameiambia BIN ZUBEIRY asubuhi ya leo kwamba, timu inaendelea na mazoezi kwenye Uwanja wake wa Azam Complex, Chamazi kwa ajili ya safari hiyo, wakati majeruhi Umony na Mieno wanafanya mazoezi ya gym.
    Azam wakijifua ufukweni

    Mshambuliaji huyo wa zamani wa kimataifa wa Tanzania na klabu ya Kariakoo United ya Lindi, amesema kwamba timu ikiwa Afrika Kusini pamoja na kuweka kambi ya mazoezi, pia itacheza mechi nne za kujipima nguvu dhidi ya timu kubwa za huko.
    Ingawa bado ratiba ya mechi za Azam nchini humo haijajulikana, lakini inafahamika miongoni mwa timu zitakazocheza na Azam ni Orlando Pirates, Supersport United, Kaizer Chiefs na Mamelodi Sundowns.
    Kuna uwezekano Azam ikacheza mechi zaidi kulingana na namna ambavyo timu zaidi nchini humo zitavuwiwa kucheza nayo.
    Azam inatarajiwa kurejea nchini siku moja kabla ya kucheza mechi ya kuwania Ngao ya Jamii kuashiria kufungua pazia la msimu mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Yanga SC, Agosti 17, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Safari hii Azam, washindi wa pili mara mbili mfululizo wa Ligi Kuu wamepania kutwaa Ngao mbele ya Yanga, baada ya mwaka jana kufungwa na Simba SC na kocha Muingereza Stewart Hall anajiandaa kikamilifu kwa ajili hiyo.    
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: AZAM FC WAPAA JUMAMOSI KWENDA AFRIKA KUSINI KUWEKA KAMBI YA KUJIANDAA NA MSIMU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top