• HABARI MPYA

    Monday, July 29, 2013

    ZFA WAKO WAPI MAKOCHA HAWA NA WANAFANYA KAZI GANI?

    IMEWEKWA JULAI 29, 2013 SAA 12"23 ASUBUHI
    SITAKOSEA kama nitasema kwamba, miongoni mwa kazi za Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), ni kusimamia timu zetu za taifa, za wachezaji wa umri mbalimbali.
    Kabla ya kujiuzulu kwa aliyekuwa Rais wa ZFA Ali Ferej Tamim, uongozi wa chama hicho uliwahi kuwaita waandishi wa habari na kuwapa taarifa za utekelezaji wa mipango ya chama katika kuendeleza mpira wa miguu nchini. 
    Miongoni mwa mipango hiyo, ilikuwa kujenga timu imara za taifa kwa umri tafauti, kuanzia ngazi ya watoto na wakubwa.
    Kupitia mkutano huo na waandishi uliofanyika mwaka 2011 katika ofisi za zamani za chama hicho zilizokuweko hoteli ya Bwawani, tuliambiwa na viongozi wa ZFA kuwa, imeamua kuteua makocha 14 kwa ajili ya kuchagua wachezaji na kuwafundisha katika timu mbalimbali za taifa.

    Kwa upande wa timu ya wakubwa yaani Zanzibar Heroes, waliopewa jukumu la kuifundisha walikuwa, Stewart John Hall, na wasaidizi wake, Hemed Suleiman ‘Moroko’ na Ali Mohammed ‘Kidy’.
    Pia tukaelezwa kutakuwa na timu ya vijana walio chini ya miaka 23 (U-23).
    Hii ingefudishwa na Abdelfatah Abbas, raia wa Misri, akisaidiwa na Juma Sheha.
    Aidha, Juma Sumbu alipewa jukumu la kuinoa timu ya vijana walio chini ya miaka 20 (U-20), na msaidizi wake, ni Ali Abdalla, wakati Mussa Jaribu akavishwa kofia ya kuifundisha timu ya wachezaji walio chini ya miaka 17 (U-17) sambamba na msaidizi wake Sheha Khamis.
    Mbali na hizo, pia ZFA ilisema imeamua kuunda timu ya watoto walio chini ya miaka 15 (U-15), ambayo kocha wake ni Alley Mohammed Alley, huku Iddi Mohammed akitajwa kuwa msaidizi wa kikosi hicho.
    Timu nyengine ni ile ya watoto wadogo wenye umri wa chini ya miaka 12 (U-12), ambayo kocha wake tulielezwa kuwa ni Hababuu Ali Omar, na Bundala Ramadhan, ndiye msaidizi wake.
    Na mwisho, ni timu ya taifa ya wanawake, ambayo kocha mwenye dhamana wa kuifundisha ni Nasra Juma Mohammed na msaidizi wake ni Ali Mohammed ‘Kidy’ ambaye pia ametajwa kuwa msaidizi wa Zanzibar Heroes.
    Lakini jambo la kushangaza, tangu wakati huo, hakuna chochote kinachofanyika kuhusiana na timu hizo na namna ya kuziendeleza, yaani hazikuchaguliwa kabisa na inaonekana uteuzi wa makocha hao ulikuwa ni porojo za ‘kufurahisha barza’ tu.
    Katika hali ya kawaida, baada ya ZFA kuteua makocha hao, ilipaswa iwape taarifa za maandishi juu ya uteuzi wao, na ifanye nao kikao ili kuwafafanulia majukumu yao.
     Yawezekana hayo yalifanyika, lakini ni kwa kiasi gani makocha hao waliwezeshwa kufanya ziara katika wilaya zote Unguja na Pemba ili kuangalia mashindano mbalimbali na kuchagua wachezaji wa kufaa kuzichezea timu hizo.
    Nina hakika hakuna jitihada zozote zilizochukuliwa kuhakikisha makocha hao wanafanya kazi waliyopewa, kwa kuwa ZFA yenyewe haina chanzo chochote cha kupata fedha za kutekeleza shughuli zake, sikwambii kusimamia timu saba za taifa.
    Ni rahisi kusema kwa mdomo kwamba mtu au taasisi inakusudia kufanya hili au lile, lakini unapofika wakati wa vitendo, kama hakuna fedha, hakutafanyika kitu, na ndivyo ilivyotokea.
    Kubwa tunalolishuhudia, ni kushughulikiwa kwa timu ya wakubwa, Zanzibar Heroes, tena hilo hufanyika kila wakati wa mashindano ya Chalenji yanayoshirikisha timu za mataifa ya Afrika Mashariki na Kati.
    Na hili nalo kwa kiasi kikubwa linabebwa na serikali, au pale wanapotokea wadhamini, huchangia walichonacho kugharamia mahitaji ya timu ikiwemo kuipatia vifaa wa ajili ya mashindano.
    Mimi huwa ninajiuliza, huwaje chama kikubwa kama ZFA kifanye maamuzi ya kukurupuka, na kushindwa kujiendesha kisasa?
    Ni wazi kuwa ZFA inakosa wataalamu ambao ingeweza kuwatumia kupanga mpango kazi wake na kuusimamia ipasavyo.
    Lakini hata ikiwa nao watu walio weledi, itawezaje kuwalipa ikiwa yenyewe ina mzigo wa madeni, hasa lile la kodi inayodaiwa na hoteli ya Bwawani ambayo imefikia shilingi milioni 14 sasa?
    Kwa hivyo, kama haina uwezo huo, kwa nini iwaite waandishi wa kujikweza kwamba ina mipango mingi na mizuri lakini mwisho wa habari ishindwe kuitekeleza?
    Tukiacha timu za umri mwengine, ZFA inaweza kueleza, kwa nini inashindwa kumtumia ipasavyo kocha Abdelfatah Abbas ambaye serikali ya Misri ilimleta msaada kwa ajili ya kuisaidia Zanzibar kujenga timu za vijana?
    Hapa hakuna tatizo la ukosefu wa fedha, kwani ZFA haipaswi kumlipa Abbas hata shilingi, kwa kuwa mambo yake yote yanasimamiwa na serikali yake na ile ya Zanzibar.
    Mara kadhaa, kocha huyo amekaririwa akilalamika katika vyombo vya habari akidai kutopewa ushirikiano na chama hicho.
    Kwamba picha kati ya ZFA na Mmisri huyo haziendi, si jambo linalotaka tochi kuliona, kwani mwaka juzi, alidiriki kuikimbia timu ya taifa ya Zanzibar Heroes iliyokuwa Dar es Salaam kwenye mashindano ya Chalenji ya Cecafa kutokana na madai ya kuingiliwa kazi na kutopewa uhuru kama kocha mwenye dhamana ya kuifundisha timu.
    ZFA inaweza kuwaeleza Wazanzibari, nchi yao imevuna nini tangu kuja kwa kocha huyo nchini?
    Kazi aliyotakiwa kuifanya Abbas akiwa hapa, ni kukusanya vijana mbalimbali wenye vipaji kwa msaada wa ZFA na kuwaendeleza, kama alivyokuwa akifanya mtangulizi wake Abdelaziz Badr El Din Hadad.
    Badala yake kocha huyo amekuwa akitwishwa mzigo usio wake, kuinoa Zanzibar Heroes, au kuwa kocha kiraka wa kuzibeba klabu zinazoshiriki mashindano ya Kombe la Kagame kama alivyokwishawahi kufanya mara kadhaa.
    Lakini tujiulize, ZFA imezifanyia kazi vipi programu za kocha huyo alizopeleka kwa chama hicho kwa ajili ya kupata usaidizi na muongozo ili atekeleze kazi iliyomleta?
    Kutokumtumia vyema Abbas, ndiko kunakosababisha mara kwa mara ailaumu ZFA kwamba haimpi ushirikiano, na hivyo kushindwa kutekeleza programu zake.
    Sasa baada ya ZFA kupata Rais mpya kufuatia kujiuzulu kwa marais wawili katika vipindi vifupi, Ali Ferej Tamim aliyekalia kiti kwa miaka mingi na Amani Makungu aliyeongoza kwa miezi saba tu, nadhani wakati umefika uongozi wa chama hicho ujitathmini kujua wapi unakosea na pia kiondokane na maamuzi ya kukurupuka, na mipango isiyoweza kuitekeleza.  
    Aidha, lazima sasa ZFA ijipange kujenga safu mpya itakayoweza kubuni namna ya kuiingizia mapato, ama kwa kutafuta mikopo ya kibenki ili kubuni miradi, au kwa kupigania kupata haki zake kutokana na fursa ambazo Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) linaipa Tanzania kupitia mgongo wa TFF zikiwemo fedha za kuendeshea ofisi.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: ZFA WAKO WAPI MAKOCHA HAWA NA WANAFANYA KAZI GANI? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top