• HABARI MPYA

    Tuesday, July 23, 2013

    SIMBA SC YAFANIKIWA KUMREJESHA OWINO, YAMTEMA SSENKOOM

    Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA JULAI 23, 3013 SAA 5: 10 ASUBUHI
    KIMEELEWEKA, Simba SC imefanikisha kumrejesha beki wake wa zamani wa kimataifa wa Uganda, Joseph Owino na imeamua kumtema pia na beki wake mwingine Mganda, Samuel Ssenkoom.
    Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe ameiambia BIN ZUBEIRY kwamba benchi la Ufundi limependekeza Owino asajiliwa na sasa mipango inakwenda vizuri.
    Anarudi; Hans Poppe kulia akizungumza na Owino kushoto Jumamosi. Katikati ni Basena

    Kuhusu Ssenkoom, Poppe amesema kwamba benchi la Ufundi chini ya kocha Mkuu, ABdallah Athumani Seif ‘King Kibaden’ limesema mchezaji huyo ni mzuri, lakini hana tofauti na wachezaji wazawa kiuchezaji hivyo hakuna haja ya kuingia gharama za ziada kwa ajili yake.
    “Tumefanya mazungumzo na mchezaji na klabu yake, mambo yanaenda vizuri na Owino anarejea nyumbani Msimbazi. 
    Na ninaomba uweke wazi hii, sisi hatukumtelekeza huyu mchezaji kama watu wanavyosema, alipoumia akiwa kwetu tulimpeleka kupatiwa matibabu India, baada ya hapo akatakiwa apumzike kwa mwaka mmoja, ndipo tukamuondoa katika usajili ili apatiwe matibabu,”.
    “Lakini yeye akaenda kusaini Azam. Yote kwa yote tunashukuru leo anarudi nyumbani akiwa fiti kabisa,”alisema Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).  
    Simba SC imeamua kumrejesha beki huyo hodari, baada ya kuvutiwa naye mwoshoni mwa wiki akiichezea URA ya kwao dhidi ya Wekundu hao wa Msimbazi, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Owino ambaye kwa sasa ni Nahodha wa timu ya Mamlaka ya Mapato Uganda, aliiongoza vyema katika mchezo huo wa kirafiki na kuibwaga Simba SC mabao 2-1, ikitoka nyuma kwa 1-0 hadi mapumziko.
    Owino alicheza tena kwa dakika 45 katika mchezo mwingine wa URA dhidi ya Yanga SC Jumapili, timu hizo zikitoka sare ya 2-2, lakini yeye aliondoka uwanjani timu yake ikiwa inaongoza 1-0.
    Ametemwa; Ssenkoom kushoto ametemwa. Hapa ni wakati akiwasili Dar es Salaam akiwa katika mahojiano na BIN ZUBEIRY

    Owino ilikuwa arejeshwe Simba SC dirisha dogo msimu uliopita akitokea Azam FC, lakini Wekundu hao wa Msimbazi hawakuridhishwa naye kutokana na kuonekana bado hayuko fiti.
    Wakati huo, Owino alikuwa anachezea Azam FC ambayo ilitaka kubadilisana beki huyo na kiungo mshambuliaji wa Simba, Uhuru Suleiman. Baada ya Simba SC kumkataa Owino alikwenda kusaini URA ambako ameng’ara na sasa anarejeshwa Msimbazi. Uhuru alihamia Azam kwa mkopo, ambako hata hivyo baada ya msimu ametolewa kwa mkopo Coastal Union ya Tanga.   
    Akizungumzia suala hilo, Owino alisema kwamba hakuna tatizo yeye kurejea Simba SC anawakaribisha kwa mazungumzo na wakiafikiana atarejea Msimbazi.
    “Mimi sina tatizo, Simba SC ni kama nyumbani, nilikuwa hapa na si ajabu kurudi hapa. Waje tuzungumze,”alisema.
    Hans Poppe alifanya mazungumzo ya awali na Owino Jumamosi Uwanja wa Taifa, akiwa na Meneja wa Simba SC, Mganda Moses Basena ambaye amepewa jukumu la kushughulikia uhamisho wake kutoka URA.
    Wachezaji wengine wa kigeni Simba SC ni kipa Abbel Dhaira, kiungo Mussa Mudde wote Waganda pia na mshambuliaji Mrundi, Tambwe Amisi.
    Imeachana na beki mwingine Mganda, Assumani Buyinzi, kiungo kutoka DRC, Felix Cuipoi pamoja na mshambuliaji Msudan, Kon James waliokuwa majaribioni. 
    Owino alisajiliwa Simba SC kwa mara ya kwanza mwaka 2009 na akaichezea timu hiyo hadi 2011 alipoumia goti na kutemwa. Alikaa nje msimu mzika kabla ya msimu uliopita kusajiliwa Azam, ambako dirisha dogo alitemwa na kurejea Uganda.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: SIMBA SC YAFANIKIWA KUMREJESHA OWINO, YAMTEMA SSENKOOM Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top