• HABARI MPYA

    Thursday, July 25, 2013

    PIGO STARS, MCHA VIALLI HATARINI KUWAKOSA THE CRANES KESHOKUTWA

    Na Boniface Wambura, Kampala, IMEWEKWA JULAI 25, 2013 SAA 6: 37 MCHANA
    KIUNGO mshambuliaji wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Khamis Mcha ‘Vialli’ anaweza kuikosa mechi dhidi ya Uganda keshokutwa kuwania tiekti ya kucheza Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN), zinazohusisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee dhidi ya Uganda, The Cranes.
    Kiungo huyo wa Azam FC anaweza kuikosa mechi hiyo itakayopigwa kwenye Uwanja wa Mandela, Namboole kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya goti.
    Hatikati; Khamis Mcha 'Vialli' yuko hatarini kuwakosa The Cranes Jumamosi

    Wachezaji wengine wote wa Stars wako katika hali nzuri na hata Mcha aliyekuwa, Dadktari wa timu, Mwanandi Mwankemwa amesema anaendelea tayari na wanampa mazoezi mepesi.
    Kikosi cha kamili cha Stars ilichoko hapa kinaundwa na makipa Juma Kaseja, Mwadini Ali na Ali Mustafa. Mabeki ni Aggrey Morris, David Luhende, Erasto Nyoni, Kelvin Yondani, Nadir Haroub na Vincent Barnabas.
    Viungo ni Amri Kiemba, Athuman Idd, Frank Domayo, Haruni Chanongo, Khamis Mcha, Mudhathir Yahya, Salum Abubakar na Simon Msuva. Washambuliaji ni John Boko, Juma Luizio na Mrisho Ngasa.
    Stars iliwasili Kampala jana jioni tayari kwa mechi ya kuwania tiketi ya CHAN, Fainali ambazo zitafanyika mwakani nchini Afrika Kusini.
    Stars ambayo iliwasili ikitokea jijini Mwanza ilipokuwa imepiga kambi ya siku kumi kujiandaa kwa mechi hiyo itakayoamua ni timu ipi kati ya hizo mbili itakwenda Afrika Kusini mwakani imefikia hoteli ya Mt. Zion iliyoko eneo la Kisseka katikati ya Jiji la Kampala.
    Kocha Mkuu wa Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager, Kim Poulsen ameridhishwa na kiwango cha hoteli hiyo, kwani ndiyo ambayo timu ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars) ilifikia Novemba mwaka jana ilipokuja Kampala kushiriki michuano ya Kombe la Chalenji inayoandaliwa na Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).
    Stars ambayo ilitiwa chachu na Rais Jakaya Kikwete alipokutana nayo Uwanja wa Ndege wa Mwanza wakati ikiondoka kuja Kampala, na kuitakia kila la kheri itafanya mazoezi yake ya mwisho kesho (Julai 26 mwaka huu) Uwanja wa Mandela kujiandaa kwa mechi ya Jumamosi.
    Kocha Kim amesema ingawa mechi hiyo ni ngumu, lakini kikosi chake kimejiandaa kuikabili Uganda kwani wachezaji wako wako vizuri na ari kwa ajili ya mechi iko juu.
    Wakati huo huo, Kocha Kim Poulsen atakuwa na Mkutano na Waandishi wa Habari siku ya Jumatatu (Julai 29 mwaka huu). Mkutano huo utafanyika saa 5 kamili asubuhi katika ukumbi wa mikutano wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: PIGO STARS, MCHA VIALLI HATARINI KUWAKOSA THE CRANES KESHOKUTWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top