• HABARI MPYA

    Wednesday, July 31, 2013

    KASEJA: SIJAMALIZANA NA LUPOPO

    Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA JULAI 31, 2013 SAA 10:17 JIONI
    NAHODHA wa timu ya soka ya taifa ya soka ya Tanzania, Taifa Stars, Juma Kaseja amesema kwamba amefanya mazungumzo tu na wakala wa klabu ya St. Eloi Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), lakini bado hajaingia Mkataba na klabu hiyo ya Lubumbashi.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY leo mchana, Kaseja amesema kwamba mtu aliyejitambulisha kwake kama wakala wa Lupopo alimfuata wakafanya mazungumzo na kufikia makubalino juu ya dau la usajili, mshahara na mambo mengine ya msingi.
    Hatujamalizana; Juma Kaseja amefikia makubaliano na Lupopo, bado kusaini Mkataba

    Hata hivyo, kipa huyo namba moja Tanzania amesema kwamba baada ya mazungumzo hayo na maafikiano, wakala huyo amepeleka majibu Lupopo ambao wakiafiki ndipo masuala ya Mkataba yatafuatia.
    “Nimezisikia hizo habari, kwamba mimi tayari ni mchezaji wa Lupopo, hapana, si kweli. Ni kwamba tumefanya mazungumzo tu na wakala wao na tumefikia makubaliano, nasubiri hadi nisaini Mkataba ndipo nitajihesabu tayari ni mchezaji wa Lupopo,”alisema Kaseja.
    Baada ya kuitumikia Simba SC tangu mwaka 2003, Kaseja hakuongezewa Mkataba klabu hiyo mwishoni mwa msimu naye ameamua kwenda kuanza maisha mapya sehemu nyingine.
    Pamoja na Simba SC kutomuongezea Mkataba Kaseja, ameendelea kuwa kipa chaguo la kwanza timu ya taifa mbele ya kocha Mdenmark, Kim Poulsen.
    Iwapo Kaseja atafanikiwa kuingia Mkataba na Lupopo atakwenda kuwa mpinzani mkuu wa wachezaji wenzake wa Taifa Stars, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wanaochezea Tout Puissant Mazembe ya Lubumbashi pia.
    Kaseja alicheza pamoja na Samatta na kiungo Mganda wa Mazembe, Patrick Ochan katika klabu ya Simba mwaka 2010 kabla ya 2011 wachezaji hao kuuzwa DRC.     
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: KASEJA: SIJAMALIZANA NA LUPOPO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top