• HABARI MPYA

    Saturday, July 20, 2013

    JOSEPH OWINO AREJESHWA SIMBA SC BAADA YA KUNG'ARA AKIICHEZEA URA LEO TAIFA

    Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA JULAI 20, 3013 SAA 3: 08 USIKU
    SIMBA SC imeanza mchakato wa kumrejesha beki wake wa zamani wa kimataifa wa Uganda, Joseph Owino baada ya kuvutiwa naye leo akiichezea URA ya kwao dhidi ya Wekundu hao wa Msimbazi, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Owino ambaye kwa sasa ni Nahodha wa timu ya Mamlaka ya Mapato Uganda, aliiongoza vyema leo katika mchezo huo wa kirafiki na kuibwaga Simba SC mabao 2-1, ikitoka nyuma kwa 1-0 hadi mapumziko.
    Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe amesema wamevutiwa na uchezaji wa Owino na wanaamini atakuwa suluhisho la tatizo lao la safu ya ulinzi kwa sasa.
    Unarudi nyumbani; Hans Poppe kulia akizungumza na Owino (kushoto) katikati ya Basena leo.

    “Anaonekana amepona kabisa, anacheza vizuri mno na kwa hakika amemvutia kila mmoja wetu hadi benchi la Ufundi limependekeza arejeshwe. Tumeambiwa amebakiza Mkataba wa miezi minne URA, tunaweza kufanya naye mazungumzo na baada ya hapo tutazungumza na klabu yake kama wanaweza kutupatia mara moja huyu mchezaji, au tusubiri hiyo miezi minne, maana si mbali,”alisema Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ). 
    Owino ilikuwa arejeshwe Simba SC dirisha dogo msimu uliopita akitokea Azam FC, lakini Wekundu hao wa Msimbazi hawakuridhishwa naye kutokana na kuonekana bado hayuko fiti.
    Poppe akizungumza na Waandishi wa Habari chini na juu akitoka uwanjani baada ya mechi


    Wakati huo, Owino alikuwa anachezea Azam FC ambayo ilitaka kubadilisana beki huyo na kiungo mshambuliaji wa Simba, Uhuru Suleiman. Baada ya Simba SC kumkataa Owino alikwenda kusaini URA ambako ameng’ara na sasa anarejeshwa Msimbazi. Uhuru alihamia Azam kwa mkopo, ambako hata hivyo baada ya msimu ametolewa kwa mkopo Coastal Union ya Tanga.   
    Akizungumzia suala hilo, Owino alisema kwamba hakuna tatizo yeye kurejea Simba SC anawakaribisha kwa mazungumzo na wakiafikiana atarejea Msimbazi.
    “Mimi sina tatizo, Simba SC ni kama nyumbani, nilikuwa hapa na si ajabu kurudi hapa. Waje tuzungumze,”alisema.
    Hans Poppe alifanya mazungumzo ya awali na Owino Uwanja wa Taifa, akiwa na Meneja wa Simba SC, Mganda Moses Basena ambaye amepewa jukumu la kushughulikia uhamisho wake kutoka URA.
    Tayari Simba SC inaye beki mmoja Mganda, Samuel Ssenkoom na ina mpango wa kusajili beki mwingine kinda wa kati wa kimataifa wa Rwanda na haijulikani ni ipi nafasi ya walinzi hao iwapo Owino atasajiliwa, kwani kanuni za usajili wa Ligi Kuu Bara ni wachezaji watano wa kigeni. 
    Wachezaji wengine wa kigeni Simba SC ni kipa Abbel Dhaira, kiungo Mussa Mudde wote Waganda pia na mshambuliaji Mrundi, Tambwe Amisi.
    Imeachana na beki mwingine Mganda, Assumani Buyinzi, kiungo kutoka DRC, Felix Cuipoi pamoja na mshambuliaji Msudan, Kon James waliokuwa majaribioni. 
    Owino alisajiliwa Simba SC kwa mara ya kwanza mwaka 2009 na akaichezea timu hiyo hadi 2011 alipoumia goti na kutemwa. Alikaa nje msimu mzika kabla ya msimu uliopita kusajiliwa Azam, ambako dirisha dogo alitemwa na kurejea Uganda.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: JOSEPH OWINO AREJESHWA SIMBA SC BAADA YA KUNG'ARA AKIICHEZEA URA LEO TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top