• HABARI MPYA

    Monday, July 29, 2013

    WADHAMINI TAIFA STARS, TBL WATOA YAO YA MOYONI KUHUSU TIMU

    Na Michael Mukuza, IMEWEKWA JULAI 29, 2013 SAA 7:30 MCHANA 
    LICHA ya Taifa Stars kushindwa kufuzu kucheza katika mashindano ya CHAN mwakani baada ya kufungwa na Uganda Cranes 3-1, wadhamini wa Stars, Kilimanjaro Premium Lager wamesema hawajakata tama nab ado wana imani na timu nzima na kocha Kim Poulsen.
    Akizungumza jijini Dar es Salaam baada ya Stars kuwasili, Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, George Kavishe alisema licha ya habari hizi kutokuwa njema kwa watanzania, ni vizuri kukubali matokeo na kuangalia picha kubwa na malengo ya muda mrefu.
    Wachezaji wa Taifa Stars wakiwasili jana usiku kutoka Uganda

    “Ni vyema tukumbuke kuwa kwenye mpira kuna kushinda na kushindwa,” alisema Bw Kavishe na kuongeza, “Tunapenda kuwahakikishia watanzania kuwa sisi kama wadhamini hatujakata tama na bado tuna imani na timu hii na kocha Kim Poulsen kwa hivyo tunawaomba watanzania wasife moyo.”
    Alisema wakati  walipoanza kuidhamini Taifa Stars mwezi Mei mwaka jana na kuwekeza zaidi ya shilingi bilioni mbili kwa mwaka, kwa muda wa miaka mitano, walikuwa na malengo kadhaa ikiwemo kuinua hadhi ya Timu ya Taifa, kuhakikisha wanaingia kambini kwa muda unaotakiwa, wanalipwa vizuri, wanakula na kulala vizuri na kusafiri vizuri.
    “Tumejitahidi kufanya mambo haya kwani wachezaji sasa hivi wana DVD zenye maelezo yao, tumewapa suti mpya na za kisasa na pia tumewapa basi jipya la kisasa. Mambo haya yote pamoja na mambo wanayofundishwa na Mwalimu Kim Poulsen yamesaidia kuleta mabadiliko kwa timu ya Taifa,” alisema.
    Alisema kuna mafanikio mazuri ya timu ya taifa ambayo watanzania lazima wayakumbuke kama kuzifunga timu kama Zambia, Cameroon, Morocco na Kenya.
    Kwa mujibu wa Meneja huyo walipoanza udhamini  Tanzania ilikuwa katika nafasi ya 145 kwa mujibu wa FIFA lakini sasa imesogea hadi 109. “Haya ni mafanikio makubwa kwani tumesogea hatua zaidi ya 40,” alisema.
    Alisema safari ya mafanikio katika mpira ni ndefu na inahitaji uvumilivu wa hali ya juu na kuongeza kuwa Kocha Kim Poulsen anafanya kazi nzuri ya kuibua vijana.
    “Kocha anahitaji kuungwa mkono na sisi sote kuanzia kwa TFF, sisi wadhamini na watanzania wote. Tunahitaji kuangalia picha kubwa,” alisema na kuongeza,”Nawaomba watanzania tuwe wazalendo wakati huu hii ni timu yetu na tunatakiwa kujivunia. Vyombo vya habari pia viwe mstari wa mbele kuonesha uzalendo.”
    Alisema mechi  dhidi ya Gambia itakayochezwa mwezi wa 9 ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia ni muhimu hata kama Tanzania haisongi mbele kwani itasaidia katika ngazi za FIFA.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: WADHAMINI TAIFA STARS, TBL WATOA YAO YA MOYONI KUHUSU TIMU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top