• HABARI MPYA

    Wednesday, August 29, 2012

    UGONJWA WASHAMBULIA VIUNGO TUPU YANGA

    Athumani Iddi 'Chuji'; Mmoja
     wa viungo wagonjwa Yanga

    Na Mahmoud Zubeiry
    VIUNGO sita wa klabu ya Yanga ya Dar es Salaam, Haruna Niyonzima, Nizar Khalfan, Rashid Gumbo, Juma Seif ‘Kijiko’, Idrisa Assenga na Athumani Iddi ‘Chuji’ ni wagonjwa.
    Kocha Mkuu wa Yanga, Tom Saintfiet, raia wa Ubelgiji aliiambia BIN ZUBEIRY jana kwamba, miongoni mwao wanasumbuliwa na Malaria na wengine mafua.
    Saintfiet alisema kwamba baadhi yao hawakufanya mazoezi tangu Jumamosi timu hiyo ikiwa Kigali, Rwanda, wengine walicheza mechi ya Jumapili dhidi ya Polisi ambayo Yanga ilishinda mabao 2-1, lakini jana hakuna kati yao aliyefanya mazoezi.  
    Koha huyo alisema anaendelea kusikilizia hali zao kuangalia uwezekano kama watacheza japo mechi ya Jumamosi dhidi ya Coastal Union, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Kwa upande mwingine, kocha huyo alisema maendeleo ya timu ni mazuri na anafurahishwa na uwezo unaoonyeshwa na wachezaji vijana wadogo kama Simon Msuva, ambaye ameleta changamoyo mpya kwenye safu ya ushambuliaji ya klabu hiyo.
    Yanga ilirejea juzi Dar es Salaam, kutokea Kigali, Rwanda, ambako ilicheza mechi mbili za kujipima nguvu na kushinda zote.
    Yanga ilimaliza ziara yake jana nchini Rwanda kwa ushindi wa mabao 2-1, wafungaji Stefano Mwasika aliyesawazishia, baada ya Fabrice kutangulia kuifungia Polisi na Nahodha Msaidizi, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ akafunga la pili.
    Katika mchezo wa awali Ijumaa, Yanga waliwachapa mabingwa wa zamani wa Afrika Mashariki na Kati, Rayon Sport mabao 2-0 kwenye Uwanja huo huo wa Amahoro mjini Kigali.
    Yanga ambao siku moja kabla ya mechi hiyo ya kwanza, walitembelea Ikulu ya Rwanda, walipoalikwa na rais Paul Kagame kupeleka Kombe la Afrika Mashariki na Kati, ambalo tangu mwaka 2002 mfadhili wake mkuu na mlezi wake ni Rais Kagame, siku hiyo mabao yake yalitiwa kimiani na Hamisi Kiiza dakika ya pili na Simon Msuva dakika 12.
    Awali, Yanga ilikuwa icheze pia na mabingwa wengine wa zamani wa Kombe la Kagame, APR, lakini kutokana na timu hiyo kukabiliwa na mgogoro hivi sasa uliosababisha kufukuzwa kwa kocha Mholanzi, Ernest Brandy na nafasi yake kupewa kocha mzalendo kwa muda, imeshindwa kucheza.
    Yanga itaendelea na mazoezi kwenye Uwanja wa sekondari ya Loyola kujiandaa na Ligi Kuu ya Bara, inayotarajiwa kuanza Septemba 15 na Jumamosi itacheza na mabingwa wa Ligi Kuu 1988, Coastal Union.
    Yanga ilitwaa Kombe la Kagame kwa mara ya pili mfululizo mwezi uliopita, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa kuifunga Azam FC mabao 2-0, ambayo yalitiwa kimiani na Hamisi Kiiza ‘Diego Milito’ na Said Bahanuzi ‘Spider Man’.
    Hiyo kwa ujumla ilikuwa mara ya tano mfululizo, Yanga inatwaa Kombe hilo, baada ya awali kuchukua mwaka jana, wakiifunga Simba katika fainali bao 1-0, Uwanja wa Taifa mfungaji Kenneth Asamoah ambaye ametemwa, ingawa siku hiyo Kiiza pia alifunga bao safi, ambalo refa alilikataa.
    Yanga ilichukua kwa mara ya kwanza Kombe hilo, mwaka 1975 ikiifunga tena Simba katika fainali, mabao 2-0 wafungaji Sunday Manara ‘Computer’ na Gibson Sembuli (sasa marehemu) Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
    Ikachukua tena mwaka 1993, Uwanja wa Nakivubo, Kampala, Uganda kwa kuifunga SC Villa mabao 2-1, yaliyotiwa kimiani na Said Nassor Mwamba ‘Kizota’ (sasa marehemu) na Edibily Jonas Lunyamila.
    Ilichukua tena mwaka 1999, ikiifunga tena SC Villa, Uwanja wa Nakivubo, kwa penalti 5-3, kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 120, Yanga ikisawazisha bao kupitia kwa Lunyamila, baada ya Hassan Mubiru kutangulia kuifungia Villa, siku hiyo Manyika Peter akicheza penalti mbili za Waganda.   
    Aidha, kwa kutwaa Kombe hilo chini ya Mbelgiji huyo, Yanga imeendeleza rekodi yake ya kutwaa mataji ya michuano hiyo, chini ya makocha wa kigeni baada ya mwaka 1975 kuchukua chini ya Tambwe Leya aliyekuwa raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kabla ya kuchukua uraia wa Tanzania, (sasa marehemu), 1993 chini ya Nzoyisaba Tauzany aliyekuwa raia wa Burundi kabla ya kuchukua uraia wa Tanzania, mwaka 1999 chini ya Raoul Shungu wa DRC na mwaka jana chini ya Mganda, Sam Timbe.
    Katika kuongeza msisimko kwenye michuano hiyo, Kampuni ya Quality Group Limited, imeongeza dola za Kimarekani 20,000, zaidi ya Sh. Milioni 30 za Tanzania kwenye zawadi za michuano hiyo.
    Ofisa Mtendaji Mkuu wa Quality, Yussuf Manji, ambaye pia ni Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, alimpa ahadi hiyo rais wa Rwanda, Paul Kagame wakati klabu hiyo ilipomtembelea rais huyo Ikulu ya Rwanda, Alhamisi kijiji cha Urugwiro.
    Kwa dola hizo 20,000 sasa kitita cha zawadi za washindi wa michuano hiyo kinatuna hadi kufika dola 80,000 kufuatia dola 60,000 zinazotolewa na rais Kagame.
    Mwaka 2002, rais Kagame aliweka rekodi ya kuwa mdhamini wa kwanza kutoa zawadi za mashindani hayo, dola 60,000 ambazo zimekuwa zikigawanywa kwa washindi watatu wa juu.
    Mbali na zawadi hizo, rais Kagame pia anatoa dola 15,000 kila mwaka kwa maandalizi ya michuano hiyo na kufanya mchango wake jumla kuwa dola 75,000.
    Kwa mchango wake huo mkubwa, Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limeyapa jina la rais huyo mashindano hayo.
    Mwakani, michuano ya CECAFA Kagame itafanyika mjini Kigali kuanzia Januari, kwa mujibu wa Katibu wa CECAFA, Nicholas Musonye.
    Musonye ataenda Kigali mapema mwezi ujao kukutana na viongozi wa Wizara ya Michezo kujadili zaidi kuhusu maandalizi ya michuano hiyo.
    Yanga ni mabingwa wa Kombe kwa miaka mfululizo, katika fainali mbili mfululizo zilizofanyika Dar es Salaam hivyo kufanya wawe wametwaa Kombe hilo mara tano jumla na mwakani wataongozana na wapinzani wao wa jadi, Simba SC kwenye michuano hiyo.
    Wenyeji Rwanda wanatarajiwa kuwakilishwa na mabingwa mara tatu wa michuano hiyo, APR, ambao mwaka huu waliambulia nafasi ya nne baada ya kufungwa na AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) katika mchezo wa kusaka mshindi wa tatu na Polisi.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: UGONJWA WASHAMBULIA VIUNGO TUPU YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top