• HABARI MPYA

    Wednesday, August 29, 2012

    TFF ILICHEZA PATA POTEA, NA IMEPATA, IMEPOTEZA, SOKA YETU IMEJERUHIWA TENA


    MICHUANO ya soka ya Kombe la taifa imeshindwa kufanyika mwaka huu na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limedhihirisha haitafanyika tena.
    Na Mahmoud Zubeiry
    Sababu ni kwamba imekosa mdhamini- baada ya mdhamini wake wa awali, Kampuni Bia  Tanzania (TBL) iliyokuwa ikidhamini michuano hiyo kupitia bia ya Kilimanjaro Premium Lager kuachia michuano hiyo.
    Wazi, TBL wamejitoa Taifa Cup baada ya kupata dili la kujitangaza kupitia timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars ambayo awali ilikuwa inadhaminiwa na kampuni nyingine ya Bia nchini, Serengeti (SBL).
    Mkataba wa udhamini wa Taifa Stars na SBL ulimalizika Desemba mwaka jana na TFF ikashindwa kukubaliana dau la mkataba mpya na SBL, na kuingia mkataba mpya naTBL. TFF waliuita mkataba huo ni mnono sana. Kweli kabisa, kwa sababu TBL walipanda dau, kutoka lile walilokuwa wakitoa SBL.
    SBL walianza kuidhamini Stars mwaka 2006, ikiwa haina na haijawahi kuwa na mdhamini. Katika kipindi hicho, SBL ilitekeleza vema mkataba wake wa udhamini na timu hiyo na kuonekana dhahiri kuvuka mipaka katika kuhakikisha timu inakuwa na maandalizi mazuri na kujenga hamasa ya mashabiki kurejesha mapenzi kwa timu yao ya taifa.
    Kwa kiasi kikubwa, Tanzania walibaki mashabiki wawili tu wa soka, mmoja wa Simba na mwingine wa Yanga, lakini timu ya taifa haikuwa ikipendwa kabisa.
    Mechi za timu ya taifa zilikuwa hazivutii mashabiki kabisa na hakuna kingine kilichosababisha hali hiyo zaidi ya kushuka kwa kiwango cha timu yenyewe na uongozi mbovu uliokosa dira ya maendeleo kwa soka ya nchi hii.
    Wengi wanaamini hata SBL walijitokeza kuisaidia timu ya taifa, ili kuunga mkono jitihada za rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ambaye alianza kwa kutimiza ahadi yake ya kuipatia timu hiyo kocha wa kigeni, kwa kumleta Mbrazil Marcio Maximo.
    Ndiyo, kwa sababu wakati huo timu hiyo ilikuwa haiuziki kwa yoyote na hata TBL hawakuwa wakiitaka wakati huo.
    SBL imefanya mambo mengi yenye kuonekana wakati wake ikiidhamini Stars tangu 2006 hadi mwaka jana Desemba mkataba ulipoisha.
    Iligharamia kambi za muda mrefu kuanzia nyumbani na ugenini, ili kuhakikisha timu yetu inajengwa vema na kuwa ya ushindani.
    Huwezi kusahau kambi za mafunzo Bulyanhulu mkoani Shinyanga, baadaye Brazil na nchi za Scandinavia.
    Chini ya Maximo kwa udhamini wa SBL tulishuhudia timu yetu imekuwa ya ushindani tena na kukaribia kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika mwaka 2008 nchini Ghana kama si kufungwa na Msumbiji katika mechi ya mwisho nyumbani.
    Hadhi ya timu ya taifa ilipanda na tulishuhudia timu kubwa kama Brazil na Ivory Coast zikipokea mwaliko wa kuja kucheza nasi mechi za kirafiki hapa.
    Matunda ya udhamini wa SBL ni timu yetu kufuzu kucheza Fainali za kwanza za CHAN  nchini Ivory Coast mwaka 2009 na kwa mara ya kwanza Watanzania waliwashuhudia wachezaji wao kwenye luninga wakicheza michuano mikubwa ya Afrika.
    Kweli, baadaye timu yetu iliporomoka na zaidi ilitokana na matatizo ya ndani ya shirikisho, nidhamu za wachezaji na ‘ujuaji’ wetu Waandishi na wachambuzi uchwara wa Tanzania uliotugharimu tukampoteza kocha mzuri, Marcio Maximo.
    Lakini hata katika wakati mgumu, wakati wa kuporomoka kwa timu ya taifa, bado SBL iliendelea kuwa bega kwa bega na timu ya taifa- hata baada ya Maximo kuondoka na hatimaye mwaka juzi timu ya Bara ikatwaa Kombe la Challenge baada ya miaka 15.
    Tanzania Bara, ambayo huundwa na asilimia 90 ya wachezaji wa Taifa Stars inayoundwa kwa mseto wa wachezaji wa Bara na visiwani Zanzibar, ambayo kwenye Challenge hushiriki kama nchi kamili, ilitwaa Kombe hilo mara ya mwisho mwaka 1994 nchini Kenya.
    Kombe la Challenge lilirejea Bara chini ya kocha aliyerithi mikoba ya Maximo, Mdenmark Jan Borge Poulsen, ambaye naye tayari ameondolewa na nafasi yake kachukua Mdenmark mwenzake, Kim Poulsen.
    SBL wamekuwa wavumilivu na kuendelea kuidhamini Stars bila ya kujali matokeo mabaya, ambayo yalisababisha mashabiki waanze kuizomea timu yao.
    Wakati wa mchakato wa kuitoa Taifa Stars SBL kuihamishia TBL niliandika nikitoa angalizo kwa TFF, nikiwaambia wanapaswa kuzingatia kwamba, TBL tayari ni wadhamini wakuu wa Kombe la Taifa, ni wadhamini wakuu wa klabu za Simba na Yanga.
    Kuwapa na timu ya taifa pia, maana yake sasa wao ndio watakaokuwa wamebeba mustakabali mzima wa soka ya nchi hii, jambo ambalo kwa mtazamo wangu niliona ni hatari.
    TBL kama kampuni, ambayo ina maamuzi yake binafsi ambayo nje ya misingi ya sheria- hayawezi kuwa na upinzani wala kipingamizi chochote, nilisema, inaingia mkataba wa kuidhamini timu ya taifa, ikiwa tayari inadhamini Kombe la Taifa na klabu za Simba na Yanga kwa sababu viongozi wa sasa wa kampuni hiyo wanaridhia hilo.
    Lakini ni hatari ikitokea akaletwa kiongozi mwingine pale TBL kutoka Afrika Kusini- ambaye atakuwa hana mapenzi na soka. Anaweza kuamua mara moja, mikataba inayoendelea ikifikia tamati na iwe basi na hakuna anayeweza kupingana nao.
    Lakini soka ya Tanzania itaingia kwenye wakati mgumu sana- kumpoteza mtu ambaye alikuwa nguzo muhimu kama mdhamini wa klabu za Simba na Yanga, Kombe la Taifa na timu ya taifa kwa wakati mmoja.
    Na nilisema wazi, historia ndio inaleta wasiwasi huu. Mwaka 2001, Ligi Kuu ya Tanzania Bara ilikuwa inadhaminiwa na TBL, lakini katika hatua za mwishoni mwa ligi hiyo, kampuni hiyo ilijitoa kwa sababu ambayo sisiti kusema ndogo tu.
    Aliyekuwa Waziri wa Michezo wakati huo, Profesa Juma Athumani Kapuya kwa utashi wake aliongeza timu mbili katika hatua ya mwisho na kuwa nane badala ya sita, ambazo wakati huo FAT ilikubaliana na TBL.
    TBL ilikerwa na hilo na ikasitisha udhamini wake mara moja na mwaka huo, ingawa timu ziliitangaza bia ya Safari Lager kwa robo tatu ya msimu, lakini hazikupata chochote, pole zaidi kwa mabingwa wa mwaka huo, Simba SC ambao walikosa zawadi.
    Wakubwa walisema tu, TBL ya sasa iko chini ya Wazungu na hawataki mambo yetu ya Kiswahili, hivyo kwa uswahili wa Kapuya kuongeza timu katika hatua ya mwisho ya ligi hiyo wao wakajitoa na ligi ikabaki yatima.
    Nilisema; ipo haja ya kutafakari, uswahili alioufanya Kapuya wakati huo, kama angeufanya katika kipindi ambacho TBL ingekuwa mdhamini wa Ligi Kuu, Kombe la Taifa na timu ya taifa, soka ya nchi hii ingekumbwa na janga kubwa kiasi gani?
    Nilisema, kweli TBL wametoa dau kubwa kuliko SBL, lakini ipo haja ya TFF kutafakari mara mbili faida na athari za kuikabidhi soka yetu yote kwa TBL.
    Sikutaka kuzungumzia malumbano ya mara ya mara na klabu za Simba na Yanga juu ya utekelezaji wa mikataba yao ya udhamini, ikiwemo kelele za kucheleweshewa mishahara au kutopewa mabasi mapya makubwa waliyoahidiwa tangu wasaini mikataba mipya mwaka jana- ila niliwaasa TFF, wawe makini na maamuzi yao.
    Sasa hata mwaka haujapita tangu nimetoa angalizo hilo, leo TBL wamelitema Kombe la Taifa na hadi unaposomoa makala hii, haijakabidhi mabasi mapya makubwa waliyoahidi kutoa kwa Simba na Yanga.
    Leo TBL wamejitoa Taifa Cup, kipi kitamzuia mtu yeyote kutilia shaka mustakabali wa udhamini wao katika klabu za Simba na Yanga, ikiwa huko nyuma waliitema Ligi Kuu?
    Kupitia Ligi Kuu, bia za TBL zilikuwa zinatangazwa kwenye jezi za klabu zote nchini zikiwemo Simba na Yanga na walijitoa sasa washindwe vipi kutoa matangazo yao kwenye jezi za klabu hizo mbili tu?
    TFF walishindwa kusoma ishara za nyakati wakaingia kichwa kichwa kwa TBL na kuwapa  mkataba wa kudhamini timu ya taifa, hawakujua nini kitatokea mbele. TBL ipo kibiashara zaidi na daima wataendelea kuangalia maslahi yao zaidi juu ya kile wanachotoa, kama kitaendana na wanachopata- sijui TFF wanafikiria nini.
    Wakati nawasilisha mada hii, najipanga kwa ajili ya kuwasilisha mada kuhusu udhaifu wa TFF kuwashauri wadhamini juu ya namna ya kuwekeza fedha zao kwenye soka kwa manufaa ya soka yetu na wao pia wanufaike kibiashara.
    Hilo litakuwa Jumapili kunako majaaliwa ‘inshaallah’. Kwa sasa, tuendelee tu kuhuzunika kwa kupoteza Kombe la Taifa, huku tukiomba Mungu alete kheri zake ajitokeza mdhamini mwingine wa kuibeba michuano hiyo ya kihistoria Tanzania, tangu enzi za mababu ikiitwa Gossage. Wasalam.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TFF ILICHEZA PATA POTEA, NA IMEPATA, IMEPOTEZA, SOKA YETU IMEJERUHIWA TENA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top