• HABARI MPYA

    Thursday, August 30, 2012

    HAMKANI SI SHWARI COASTAL UNION

    Kocha Mgunda akizungumza na wachezaji wake juzi

    Na Prince Akbar
    HAMKANI si shwari ndani ya Coastal Union ya Tanga, kufuatia kile kinachoelezwa mgawanyiko baina ya viongozi kuhusu benchi la ufundi la klabu hiyo, linaloongozwa na Kocha Mkuu, Juma Mgunda, akisaidiwa na Habib Kondo, Kocha wa mazoezi ya viungo, Ally Jangalu na Kocha wa makipa, Bakari Shime.
    Coastal Union imefungwa mechi tatu za kujipima nguvu katika ya nne ilizocheza na hata hiyo mechi waliyoshinda, mashabiki hawakuridhishwa na kiwango na kwa hali hiyo wanatoa shinikizo la kufanyika mabadiliko katika benchi la ufundi.
    Baadhi ya viongozi wa Coastal wanaunga mkono, lakini wengine wanapingana na wazo hilo, wakidai bado ni mapema sana na hasa ikizingatiwa timu ipo kwenye mechi za kujipima nguvu kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Hali ilikuwa mbaya zaidi jana baada ya Coastal kufungwa mabao 2-0 na Bandari ya Mombassa, Kenya katika mchezo wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.
    Mabao ya Bandari inayocheza Ligi Daraja la Kwanza Kenya, yalitiwa kimiani na kiungo David Naftali dakika ya 27 kwa shuti la umbali la mita 35, baada ya kupewa pasi na mshambuliaji Thomas Maurice, wote Watanzania.
    Bao la pili lilifungwa na Evan Wandela dakika ya 88 kwa kichwa akiunganisha kona iliyochongwa na Hussein Puzzo.
    Baada ya mchezo huo, mashabiki wa Coastal waliwatia kashikashi makocha Juma Mgunda na Msaidizi wake Habib Kondo wakidai hawafai na kutaka waondolewe, hali ambayo ilifanya waondolewe uwanjani kwa msaada wa Polisi.
    Hali hii inajitokeza kwa mara ya pili, baada ya juzi pia timu hiyo ikicheza na JKT Oljoro ya Arusha pamoja na kushinda bao 1-0, mashabiki walilalamikia kiwango kibovu na kuzomea makocha. Jumamosi, Coastal itacheza Yanga Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Katika hali ambayo inaashiria hata Mgunda haridhishwi na kiwango cha timu yake, juzi aliwaweka kikao wachezaji wake kuwapa nasaha juu ya hali ya timu na namna wanavyokaribisha shinikizo kutoka nje mapema.
    Mgunda aliwaleza wazi wachezaji wa timu hiyo matatizo yao ya kiuchezaji akitolea mfano mechi mbili zilizopita, zikiwemo dhidi ya Oljoro na Polisi mjini Morogoro.
    Alitumia takriban saa nzima akizungumza na wachezaji hao, ambao walionekana kutulia wakimsikiliza kwa makini.
    Katika mchezo wa Jumatatu, bao pekee la mabingwa hao wa 1988, lilitiwa kimiani na beki mpya aliyesajiliwa kutoka Simba SC, Juma Jabu dakika ya 32 baada ya kupanda mbele kusaidia mashambulizi akiteleza kutokea wingi ya kushoto.
    Huo ulikuwa ni ushindi wa kwanza wa Wagosi hao wa Kaya, ndani ya mechi nne za kujipima nguvu, ikitoka kufungwa 3-2 na Bandari mjini Mombasa, Kenya na 1-0 dhidi ya Polisi mjini Morogoro na 2-0 na Bandari.
    Pamoja na ushindi huo, mashabiki wa Coastal hawakuridhishwa na kiwango cha timu na kuanza kubeza uwezo wa makocha wa timu hiyo, Juma Mgunda na msaidizi wake, Habib Kondo.
    Coastal iliwekeza kwenye usajili wa kishindo, ikiamini itafanya vizuri katika Ligi Kuu, lakini kwa matokeo haya ya awali tayari hofu imeanza kuingia na wakati mashabiki wakitilia hofu uwezo wa makocha, wengine wanatilia hofu uwezo wa wachezaji waliosajiliwa, wakiamini inaweza kuwa ni bora kwa majina tu.
    Kikosi cha Coastal kinaundwa na makipa; Juma Mpongo, Abraham Chove na Rajab Kaumba, mabeki; Said Sued (Nahodha) Mbwana Kibacha (Nahodha Msaidizi) Othman Omary, Juma Jabu, Ismail Suma, Jamal Machelenga, Cyprian Lukindo na Philipp Mugenzi.
    Viungo watakuwa ni Jerry Santo, Razack Khalfan, Mohamed Binslum, Khamis Shango, Mohamed Issa, Mohamed Soud, Suleiman Kassim ‘Selembe’, Lameck Dayton, Joseph Mahundi, Aziz Gilla na Shaffih Kaluani, wakati washambuliaji ni Nsa Job, Atupele Green, Danny Lianga na Pius Kisambale.
    Mbali na Kocha Mkuu, mshambuliaji wake wa zamani, Mgunda,  na Msaidizi wake, beki wa zamani wa Pan African, Habibu Kondo, benchi la ufundi la Coastal linakamilishwa na kocha wa viungo, mchezaji wake wa zamani, Ally Jangalu na kocha wa makipa Bakari Shime.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HAMKANI SI SHWARI COASTAL UNION Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top