• HABARI MPYA

    Saturday, August 25, 2012

    SIMBA NA TIMU YA OLIECH SASA KESHO ARUSHA

    Simba SC

    Na Mahmoud Zubeiry
    MECHI ya kujiandaa na Ngao ya Jamii, kwa mabingwa wa Tanzania Bara, Simba SC, dhidi ya Mathare United ya Kenya iliyokuwa ichezwe leo kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha, sasa itachezwa kesho.
    Habari za ndani kutoka Simba, ambazo BIN ZUBEIRY imezipata, zimesema kwamba kuahirishwa kwa mechi hiyo, kumetokana na Mathare inayoshiriki Ligi Kuu Kenya, kukabiliwa na mchezo wa ligi hiyo leo.
    Chanzo chetu kutoka Simba, kimesema kwamba baada ya mechi yao hiyo, Mathare ambayo ilimuibua kisoka mshambuliaji wa AJ Auxerre ya Ufaransa, Dennis Oliech itapanda basi kuvuka mpaka wa Namanga kuja Arusha tayari kwa mechi hiyo.
    Baada ya mechi hiyo, Jumamosi ijayo Simba itacheza mechi nyingine ya kujipima nguvu mkoani Tanga kabla ya kurejea Dar es Salaam tayari kutetea Ngao yao, waliyoitwaa pia mwaka jana kwa kuifunga Yanga 2-0, mabao ya Felix Sunzu na Haruna Moshi ‘Boban’.
    Simba itamenyana na Azam katika mechi ya Ngao ya Jamii ya kuashiria kufunguliwa kwa pazia la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Septemba 8, mwaka huu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Kuchelewa kwa mechi hiyo ambako kumeenda sambamba na kuchelewa kuanza kwa ligi hiyo, kumetokana na kuchelewa kufikiwa mwafaka mapema wa mkataba mpya wa udhamini wa Ligi Kuu. Mkataba wa awali wa Vodacom na TFF unafikia tamati mwishoni mwa mwezi huu na kusainiwa mkataba mwingine, baada ya majadiliano yanayoendelea.
    Lakini kwa kuwa Mkutano Mkuu wa TFF uliopita uliridhia kuanzia msimu ujao Ligi Kuu iendeshwe na kampuni itakayoundwa na klabu za Ligi Kuu mjadala kuhusu udhamini mpya wa ligi umekuwa mrefu kutokana na kuhusisha pande tatu, klabu, wadhamini na shirikisho.
    Lakini sasa, kwa vyovyote, hata maridhiano ya mkataba mpya wa udhamini na Vodacom yachelewe tena, mechi hiyo itachezwa Septemba 8, ikiwa ni wiki moja kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu.
    Kihistoria hiyo itakuwa mechi ya tano ya Ngao ya Jamii kuchezwa nchini na ya pili kuishirikisha timu nje ya wapinzani wa jadi wa soka ya Tanzania, Simba na Yanga.
    Mtibwa ilicheza na Yanga mwaka 2009, baada ya Simba kugoma na ikashinda mabao 2-1 na kutwaa Ngao, wakati kabla ya hapo, mwaka 2001, Ligi Kuu ya Tanzania ikiwa bado inadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia ya Safari Lager, ilichezwa mechi ya kwanza ya Ngao kihistoria.
    Katika mechi hiyo, Yanga ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Simba na mwaka juzi Yanga iliifunga tena Simba kwa penali 3-1 kufuatia sare ya 0-0 na mwaka jana, Simba ilitwaa Ngao ya kwanza katika historia yake, kwa kuifunga Yanga mabao 2-0. 
    Wakati huo huo: Kiungo Mganda, Mussa Mude amerejea juzi nchini na yuko Dar es Salaam kwa matibabu, kabla ya kuungana na wenzake kambini Arusha. “Kama inavyofahamika, Mude ni majeruhi, alipewa mapumziko na amerudi ndani ya muda aliotakiwa, sasa ataonana na daktari kwa vipimo kabla ya kwenda kuungana na wenzake kambini,”alisema kiongozi mmoja wa Simba.  

    MABINGWA WA MECHI ZA NGAO YA JAMII:
    Mwaka         Mshindi       Matokeo
    2001             Yanga           2-1 Simba
    2010             Yanga           0-0 Simba (3-1penalti)
    2011             Simba           2-0 Yanga
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA NA TIMU YA OLIECH SASA KESHO ARUSHA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top