• HABARI MPYA

    Thursday, August 30, 2012

    AZAM YAWAPOKONYA PINGU AZAM NA KUWATUPA WENYEWE GEREZANI

    Ibra Mwaipopo

    Na Princess Asia
    AZAM FC imeibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Prisons jioni hii kwenye Uwanja wa Chamazi, katika mchezo wa kirafiki, maalum kwa timu hiyo kujiandaa na mechi ya Ngao ya Jamii Septemba 12, mwaka huu dhidi ya Simba SC.
    Katika mchezo huo, bao pekee la Azam FC lilitiwa kimiani na kiungo Ibrahim Mwaipopo dakika ya 34, baada ya kupunguza mabeki wawili wa Prisons na kutumbukiza mpira nyavuni.
    John Raphael Bocco ‘Adebayor’ na Pappie aliye kwenye majaribio kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), wote walicheza leo na walifanya vizuri, lakini tatizo waliwekewa ulinzi mkali mno na mabeki wa Prisons.   
    Baada ya mchezo huo, Azam watashuka tena dimbani Jumapili kwenye Uwanja huo kumenyana na Coastal Union katika mchezo mwingine wa kirafiki.
    Mechi hizo za kujipima nguvu, zinakuja katika wakati ambao makali ya
    mshambuliaji wa Azam FC, John Raphael Bocco ‘Adebayor’ yameongezeka mno tangu arejee kutoka Afrika Kusini, alikokuwa anafanya majaribio ya kujiunga na Super Sport United, ambako inaelezwa alifuzu.
    Bocco amekuwa akifunga sana mabao katika mazoezi ya timu hiyo, Uwanja wa Chamazi na hata uwezo wake wa kumiliki mpira, kuwatoka mabeki, kasi na kupaa juu kupiga vichwa, vimeongezeka pia.
    Hizi ni habari njema kwa Azam washindi wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, inayofundishwa na kocha wake Raia wa Serbia Boris Bunjak, kuelekea mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya mabingwa Simba SC, Septemba 12, mwaka huu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Bocco ambaye alifunga mabao mawili, wakati Azam inaichapa mabao 8-0 Transit Camp Jumamosi Uwanja wa Chamazi, mengine yakifungwa na Papie, mshambujliaji mpya aliye kwenye majaribio kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Kipre Herman Tcheche na Abdulhalim Humud kila mmoja nae alifunga mabao mawili, alifanya majaribio kwa wiki mbili na Super Sport.
    Katika majaribio, imeelezwa Bocco amefuzu na Azam inataka ilipwe dola za Kimarekani 200,000 ili kumuuza, ingawa klabu ya Afrika Kusini inaonekana kutaka kutoa dau dogo chini ya hapo.  Imeelezwa wiki hii viongozi wa Super Sport wanatarajiwa kuja nchini kujadili zaidi juu ya kumnyakua mfungaji huyo bora wa Ligi Kuu msimu uliopita. 
    Azam inatarajiwa kuivaa Simba katika mechi ya Ngao ya Jamii ya kuashiria kufunguliwa kwa pazia la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Septemba 12, mwaka huu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ikiwa ni mchezo wake wa kwanza katika historia ya Ngao hiyo.
    Kihistoria hiyo itakuwa mechi ya tano ya Ngao ya Jamii kuchezwa nchini na ya pili kuishirikisha timu nje ya wapinzani wa jadi wa soka ya Tanzania, Simba na Yanga.
    Mtibwa ilicheza na Yanga mwaka 2009, baada ya Simba kugoma na ikashinda mabao 2-1 na kutwaa Ngao, wakati kabla ya hapo, mwaka 2001, Ligi Kuu ya Tanzania ikiwa bado inadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia ya Safari Lager, ilichezwa mechi ya kwanza ya Ngao kihistoria.
    Katika mechi hiyo, Yanga ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Simba na mwaka juzi Yanga iliifunga tena Simba kwa penali 3-1 kufuatia sare ya 0-0 na mwaka jana, Simba ilitwaa Ngao ya kwanza katika historia yake, kwa kuifunga Yanga mabao 2-0.
    Ikumbukwe mara ya mwisho Simba SC ilipokutana na Azam FC, katika Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame mwezi uliopita Dar es Salaam, ilifungwa mabao 3-1, yote yakifungwa na Bocco na lile la kufutia machozi kwa wekundu hao Msimbazi liliwekwa kimiani na beki mahiri Shomari Kapombe, aliyemajeruhi kwa sasa.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM YAWAPOKONYA PINGU AZAM NA KUWATUPA WENYEWE GEREZANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top