• HABARI MPYA

    Wednesday, August 29, 2012

    SIMBA SC WAZIDI KUIKUSANYIA NGUVU AZAM FC, SEPTEMBA 8 PATACHIMBIKA TAIFA

    11 mpya ya kwanza Simba SC

    Na Prince Akbar
    SIMBA leo inacheza mechi ya kirafiki na klabu ya soka ya Oljoro JKT katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha.
    Mechi hiyo ni sehemu ya maandalizi ya michuano ya Ligi Kuu ya Tanzania inayotarajiwa kuanza baadaye mwezi ujao.
    Hii itakuwa mechi ya pili ya kirafiki ya Simba kucheza jijini Arusha baada ya ile ya juzi dhidi ya Mathare United ya Kenya, ambao Wekundu hao wa Msimbazi walishinda mabao 2-1.
    Oljoro JKT imetoka kwenye michuano ya timu za majeshi hapa nchini ambapo ilichukua nafasi ya kwanza pamoja na Ruvu JKT na inacheza mechi hiyo ikitokea Tanga ambako ilifungwa bao 1-0 na Coastal Union kwenye uwanja wa Mkwakwani, Jumatatu.
    Akizungumzia pambano hilo Kocha Mkuu wa Simba, Profesa Milovan Cirkovick amesema atatoa nafasi kwa wachezaji wengi kwa kadri itakavyowezekana kwenye pambano hilo.
    Viingilio vitakuwa ni Sh 5,000 kwa VIP A, Sh 3,000 kwa VIP B na Sh 2000 kwa VIP C. Kiingilio kwa watoto kitakuwa ni Sh 1000.
    Katika mchezo, Simba itamkosa mshambuliaji wake Mzambia, Felix Sunzu ambaye ameondoka nchini jana kuelekea Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kuhudhuria mazishi ya dada yake ambaye alifariki dunia juzi jioni nchini humo.
    Dada huyo wa mshambuliaji huyo, alipatwa na mauti hayo akiwa amekwenda kumtembelea ndugu yao, beki Stopila, anayechezea Tout Puissant Mazembe siku sita zilizopita, kufuatia kupatwa na ugonjwa wa Malaria ulimpanda kichwani (Cerebral Malaria).
    Simba inatarajiwa kumenyana na Azam FC katika mechi ya kuwania
    Ngao ya Jamii ya kuashiria kufunguliwa kwa pazia la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Septemba 8, mwaka huu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Kihistoria hiyo itakuwa mechi ya tano ya Ngao ya Jamii kuchezwa nchini na ya pili kuishirikisha timu nje ya wapinzani wa jadi wa soka ya Tanzania, Simba na Yanga.
    Mtibwa ilicheza na Yanga mwaka 2009, baada ya Simba kugoma na ikashinda mabao 2-1 na kutwaa Ngao, wakati kabla ya hapo, mwaka 2001, Ligi Kuu ya Tanzania ikiwa bado inadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia ya Safari Lager, ilichezwa mechi ya kwanza ya Ngao kihistoria.
    Katika mechi hiyo, Yanga ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Simba na mwaka juzi Yanga iliifunga tena Simba kwa penali 3-1 kufuatia sare ya 0-0 na mwaka jana, Simba ilitwaa Ngao ya kwanza katika historia yake, kwa kuifunga Yanga mabao 2-0. 

    MABINGWA WA MECHI ZA NGAO YA JAMII:
    Mwaka             Mshindi Matokeo
    2001             Yanga           2-1 Simba
    2010             Yanga           0-0 Simba (3-1penalti)
    2011             Simba           2-0 Yanga
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC WAZIDI KUIKUSANYIA NGUVU AZAM FC, SEPTEMBA 8 PATACHIMBIKA TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top