• HABARI MPYA

    Sunday, August 26, 2012

    HANS POPPE ANAKABILIWA NA CHANGAMOTO YA KUBADILI TASWIRA YA F.O.S.

    Na Mahmoud Zubeiry

    KWA muda mrefu, kundi la Friends Of Simba limekuwa likishutumiwa kuwahujumu viongozi waliopo madarakani na hii iliwahi kutokea hata Kassim Mohamed Dewji mmoja wa waasisi wa kundi hilo, akiwa madarakani.
    Kassim alikuwa Katibu Mkuu chini ya Mwenyekiti Juma Salum Muhovuge na Makamu, Ramadhani Balozi (wote marehemu)- lakini uongozi wao pia uliwahi kulishika uchawi kundi la Friends Of Simba.
    Kassim hakuwa mmoja wa viongozi waliolishika uchawi kundi la Friends, bali alituhumiwa naye kwa pamoja kuwa kibaraka wa kundi hilo katika kutekeleza mipango yao hasi.
    Mwisho wa siku K.D. alijiuzulu Simba na tangu wakati huo, haujatokea utawala ambao tangu unaingia madarakani hadi unaondoka haukuwahi kulishika uchawi kundi hilo, kiasi kwamba hadi likapewa jina na Mwina Kaduguda, Enemies Of Simba, yaani maadui wa Simba.
    Kaduguda alikuwa Katibu Mkuu katika utawala uliopita chini ya Daalal na hata sasa ‘Mr maneno mengi, vitendo haba’, Ismail Aden Rage akiwa madarakani, Friends imekwishazungumzwa vibaya.
    Hiyo ndiyo picha ya Friends of Simba ndani ya Simba, lakini bado ukimtazama mtu mmoja mmoja kutoka wale Friends of Simba, inakuwa vigumu kuamini hilo.
    Wanaoneka watu wenye mapenzi haswa na Simba, ambao wanachoweza ni kusaidia tu timu yao na si zaidi ya hapo. Friends of Simba ni kundi ambalo linaanza mi naliona, Mungu amrehemu marehemu Amin Bakhroon katika jitihada za awali za uundwaji wa kundi hilo, alikuwepo.
    Na moja ya kazi za awali za Friends ni usajili wa beki Paul John Masanja na winga Ephraim Makoye kutoka Yanga mwaka 2000, ambao hata hivyo haukufanikiwa kutokana na klabu yao kutowaruhusu, ingawa baadaye wachezaji wote hao walichezea Simba.
    Binafsi nimekuwa nakerwa na tuhuma hizo, kwa sababu  naona haziendani na dhamira ya kundi hilo- zaidi kilichopo ni mambo ya mjini, kupakana matope ili kuharibiana. Na ni kuharibiana kweli, kwa sababu kwa watu walio mbali na ukweli wanaweza kuubeba uongo na kusadiki.
    Vema, F.O.S. Alhamisi imepata uongozi mpya chini ya Mwenyekiti,
    Zacharia Hans Poppe katika kikao kilichofanyika hoteli ya JB Belmonte, katikati ya Jiji.
    Hans Poppe anachukua nafasi ya Salum Abdallah, aliyeliongoza kundi hilo kwa zaidi ya miaka mitano na kuleta mafanikio makubwa ndani ya Simba, kwa uhamasishaji wa kundi hilo lililojizolea umaarufu mkubwa ndani ya klabu hiyo.
    Mbali na Hans Pope, wengine waliochaguliwa ni Adam Mgoyi anayekuwa Makamu Mwenyekiti, nafasi ya Katibu Mkuu imekwenda kwa Mulamu Nghambi, wakati nafasi ya Katibu Msaidizi amechaguliwa Niki Magariza na Juma Pinto atakuwa Msemaji wa kundi hilo.
    Baada ya kuchaguliwa, Hans Poppe aliahidi kufanya jitihada  kuhakikisha kundi hilo linafanya kazi kwa kushirikiana na uongozi kwa lengo la kuleta maelewano yatakayoijenga Simba imara na kuleta burudani kwa wapenzi na mashabiki.
    “Sisi ni marafiki wa Simba, tunachokifanya lazima kiendane na tafsiri ya neno lenyewe na isije ikawa tofauti kuwa ni maadui wa Simba, naomba ushirikiano wa pamoja kuhakikisha tunafanikisha malengo yetu,” alisema Hans Poppe katika shukrani zake.
    Awali, mmoja wa waasisi wa kundi hilo, Jaji mstaafu Thomas Mihayo alisema mwelekeo na dira ya kundi hilo vilipotea, hivyo kuwa na imani kwa viongozi wapya kufanya kazi ambayo itakuwa na faida kwa maendeleo ya Simba.
    Jaji Mihayo alisema kundi hili limekuwa na malengo mazuri, lakini kinachokwamisha sasa hivi ni wanachama wake kutokuwa wamoja na kuwataka kurudisha umoja na kufuatialia kwa karibu mambo ambayo yanapangwa kwa ajili ya utekelezaji.
    Viongozi waliomaliza muda wao mbali na Salum Abdallah (Mwenyekiti), wengine ni Johnson Masabala (Makamu Mwenyekiti) na Issa Batenga aliyekuwa katibu wa kundi hilo.
    Hans Poppe kwa pamoja na Jaji Mihayo wametoa rai nzuri kuhusu mustakabali wa F.O.S.- kwanza kushirikiana na uongozi uliopo madarakani ili kuondoa dhana potofu.
    Matatizo, misigano ni changamoto za kawaida, ambazo umefika wakati sasa watu wajifunze kuyakabili hayo mambo badala ya kujenga chuki na uadui usio na msingi.
    Na taasisi yoyote bora, itatokana na wafuasi wasioburuzwa- hivyo katika namna hii malumbano, misigano lazima viwepo katika kila mtu kuonyesha msimamo wake, mwisho wa siku mwenye hoja ndiye mshindi. 
    Naona ipo hoja chini ya Hans Poppe tukaishuhudia F.O.S. mpya, itakayorejesha imani yake mbele ya wapenzi, wanachama na wadau wengine wote wa Simba.
    Ingawa wengi walianza kumfahamu Hans Poppe, aliyezaliwa mwaka 1956 mjini Dar es Salaam siku za karibuni na wengi wakiamini huyu ni mtoto wa Hans Poppe aliyewahi kutuhumiwa kwa kesi ya uhaini, lakini huyu yupo ndani ya Simba kwa muda mrefu.
    Kihistoria, baada ya kumaliza elimu ya sekondari, Zacharia alijiunga na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) ambako alifikia cheo cha Kapteni, kabla ya kuachishwa kazi na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela, kwa tuhuma za uhaini, dhidi ya serikali ya awamu ya kwanza, ya hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, mwaka 1983.
    Lakini mwaka 1995, Zacharia aliachiwa huru kwa msamaha wa rais wa awamu ya pili, Alhaj Ally Hassan Mwinyi, mwezi mmoja kabla hajamuachia Ikulu ya Tanzania, Benjamin William Mkapa, rais wa awamu ya tatu.
    Kama zinavyosema sheria za nchi, mtu aliyehukumiwa kifungo, hana haki ya kugombea wadhifa wowote au kuajiriwa tena, Zacharia naye hakuweza kurejea kazini, badala yake akaamua kujiajiri, kwa kuanzisha miradi yake mwenyewe, ambayo leo ikiwa ni miaka 17 baadaye, miradi hiyo imesimama imara.
    Alianza kuipenda Simba SC mwanzoni kabisa mwa miaka ya 1970, akiwa kijana mdogo na zaidi mwenyewe anasema, mechi ambayo ilimfanya ajitamke rasmi yeye ni Simba damu ilikuwa dhidi ya wapinzani wa jadi, Yanga Juni 23, mwaka 1973, ambayo Wekundu wa Msimbazi, walishinda 1-0, bao pekee la Haidari Abeid ‘Muchacho’ dakika ya 68.
    Zacharia aliendelea kuwa mpenzi wa Simba, hadi baadaye akaamua kuwa mwanachama, lakini siku zote alikuwa pembeni, hadi lilipoundwa kundi la Friends Of Simba ndipo akaamua kujiunga nalo, ili naye aweze kutoa michango yake zaidi.
    Wakati wa uongozi wa Mwenyekiti, Hassan Daalal ambao ulionekana kuelemewa na majukumu ya timu, ndipo Hans Poppe alipata umaarufu zaidi ndani ya Simba, kutokana na kusaidia zaidi.
    Baada ya uongozi wa Daalal kugundua umuhimu wake, ukampa jukumu la kusimamia fedha na alifanikiwa kudhibiti fedha na kuanzisha mpango wa kuiwezesha klabu kujitegemea katika mambo mbalimbali, ikiwemo suala la usajili badala ya kutembeza bakuli.
    Kutokana na kufanya kwake vizuri katika jukumu hilo, wengi miongoni mwa wanachama na viongozi wa Simba wakamuomba agombee Uenyekiti, lakini sheria za nchi kwa sababu amewahi kutumikia kifungo jela, zikambana.
    Akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Hans Poppe amesaidia sana kuiwezesha klabu kukusanya fedha na kutunza, ambazo zimeiwezesha klabu kujitegemea kusajili kwa takriban asilimia 85.  Na ni fedha ambazo zimetokana na mapato ya milangoni, udhamini wa TBL, pango za majengo ya klabu na mauzo ya wachezaji Mbwana Samatta, Patrick Ochan na Mussa Mgosi na nyingine kutokana na michango wanayojichangisha..
    Unaweza kuona kabisa, F.O.S. imepata kiongozi mzuri, mwenye rekodi nzuri, busara, weledi na hekima na vema zaidi ni mzoefu wa mikikimikiki, si mtu ‘laini laini’ na kwa kuwa ahadi zake zimesikika na hilo ndilo tatizo kubwa kwa sasa, basi na ajue amebeba matarajio ya wana Simba.
    Wakati tunampongeza Hans Poppe kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa F.O.S., lakini anapaswa kujua anakabiliwa na mtihani mkubwa wa kurejesha imani ya kundi hilo ndani ya klabu kwa ujumla. Alamsiki.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HANS POPPE ANAKABILIWA NA CHANGAMOTO YA KUBADILI TASWIRA YA F.O.S. Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top