• HABARI MPYA

  Sunday, January 01, 2017

  SIMBA YAANZA VYEMA KOMBE LA MAPINDUZI, LUIZIO AFUNGUA AKAUNTI YA MABAO

  Na Mwandishi Wetu, ZANZIBAR
  SIMBA SC imeanza vyema michuano ya Kombe la Mapinduzi baada ya kuifunga Taifa Jang’ombe mabao 2-1 katika mchezo wa Kundi A usiku huu Uwanja wa Amaan, Zanzibar. 
  Hadi mapumziko, Simba walikuwa mbele kwa mabao 2-0 yaliyofungwa na wachezaji wa zamani wa Mtibwa Sugar, Muzamil Yassin na Juma Luizio.
  Kiungo Muzamil Yassin alianza kuifungia Simba dakika ya 27 baada ya kuwahi mpira uliogonga mwamba na kurudi kufuatia shuti la beki Mzimbabwe, Method Mwanjali ambalo lilimshinda kipa Ahmed Suleiman.
  Mshambuliaji Juma Luizio akafunga kwa shuti la umbali wa mita 17 baada ya kuwatoka mabeki wawili wa Taifa, kufuatia pasi ya Muzamil Yassin.
  Luizio anayecheza kwa mkopo kutoka Zesco United ya Zambia akiichezea kwa mara ya pili Simba leo, alidumu uwanjani kwa dakika 60 tu kabla ya kumpisha Mrundi, Laudit Mavugo. 
  Beki wa kati wa Simba, Novaty Lufunga akajifunga kwa kichwa katika harakati za kuokoa mpira wa kona uliochongwa na Hassan Bakari dakika ya 76 kuipatia Taifa bao la kufutia machozi.
  Katika mchezo uliotangulia, URA iliichapa 2-0 KVZ. Simba sasa inalingana kwa pointi na URA na Taifa iliyoifunga Jang’ombe Boys 1-0 katika mchezo wa kwanza Ijumaa.
  Kikosi cha Simba leo kilikuwa; Daniel Agyei, Hamad Juma, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Novaty Lufunga, Method Mwanjali, James Kotei, Shiza Kichuya/Mwinyi Kazimoto, Muzamil Yassin, Juma Luizio/Laudit Mavgugo dk60, Said Ndemla na Jamal Mnyate/Moses Kitundu dk66.
  Taifa Jang’ombe; Ahmed Suleiman, Adam Hamad, Saleh Mgeni/Hassan Bakari dk59, Abdallah Shaibu, Samir Yahya, Khatib Simai, Ally Mlanga, Baraka Ushindi/Mohmed Salum ‘Messi’ dk56, Seif Hassan, Adam Ibrahim/Method Apigi dk62 na Yahya Tumbo/Nelson Gabriel dk72.  
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA YAANZA VYEMA KOMBE LA MAPINDUZI, LUIZIO AFUNGUA AKAUNTI YA MABAO Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top