• HABARI MPYA

    Tuesday, July 07, 2015

    BAHATI ‘ALIYOIPIGA TEKE’ JOHN BOCCO YAANGUKIA KWA MGANDA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    MSHAMBULIAJI Frank Kalanda wa Uganda iliyoitoa Tanzania katika Raundi ya Kwanza kufuzu CHAN ya mwakani, amechukua nafasi ya John Raphael Bocco klabu ya Free State Stars ya Afrika Kusini.
    Azam FC ilikubali kumuuza mshambuliaji wake John Raphael Bocco ‘Adebayor’ kwa dola za Kimarekani 80,000 zaidi ya Sh. Milioni 160,000 za Tanzania kwa klabu ya Free State Stars, lakini mchezaji huyo ‘akazingua’.
    Mrisho Khalfan Ngassa aliyesajiliwa na Free State Mei mwaka huu kutoka Yanga SC, ndiye aliyemuunganishia Bocco dili la kujiunga na timu hiyo ya Ligi Kuu ya ABSA.
    Mazungumzo baina ya FS na Bocco yalifanyika vizuri na mshambuliaji wa Tanzania mwishowe akawaambia Azam FC; “Ninabaki hapa hapa, siendi popote, mimi bado”.
    Kalanda kulia akiwa na Mrisho Ngassa kwenye la FS kwa safari la Johannesburg kuweka kambi
    Wachezaji wa FS walisimama kidogo 'kuchimba dawa' wakiwa njiani kuelekea Johannesburg
    Mrisho Ngassa aliingia dukani kununua mahitaji madogo madogo ya kambini wakiwa njiani kuelekea Johannesburg 

    FS ilimpa mshahara mzuri Bocco, mara mbili ya ule anaopata Azam FC kwa sasa, lakini haikutosha kumshawishi mshambuliaji mrefu ahamie Bethlehem, ndipo ikaamua kuhamia kwa Kalanda aliyechangamkia dili ‘chap chap’.
    Tayari Kalanda yupo kambini na FS katika hoteli ya Lake View mjini Johannesburg kujiandaa na Ligi Kuu ya Afrika Kusini, inayotarajiwa kuanza Agosti 8, mwaka huu.
    Timu hiyo ya kocha Mmalawi, Kinnah Phiri inatarajiwa kuanza na Black Aces, wakati mechi ya pili watacheza na mabingwa watetezi, Kaizer Chiefs. Mechi ya kwanza, Kaizer wataanza kutetea taji lao dhidi ya Chippa United Agosti 8.
    Kwa mujibu wa ratiba ya msimu wa PSL wa 2015-16, Mamelodi Sundowns wataanza na Platinum Stars, Orlando Pirates na SuperSport United, wakati timu mbili zilizopanda msimu huu, Golden Arrows na Jomo Cosmos watakuwa nyumbani na University ya Pretoria na ugenini na Maritzburg United.
    Kalanda anayetokea URA ya kwao, ametua kwa bei rahisi Bethlehem na mshahara nafuu kuliko ambao FS ingetoa kwa Bocco. 
    Tanzania, Taifa Stars baada ya kufungwa 3-0 na Uganda katika mchezo wa kwanza Zanzibar ilimfukuza aliyekuwa kocha wake Mholanzi, Mart Nooij na timu hiyo kukabidhiwa kwa mzalendo, Charles Boniface Mkwasa ambaye alikwenda kutoa sare ya 1-1 na Uganda katika mchezo wa marudiano mjini Kampala.
    John Bocco amekataa kujiunga na FS, nafasi ambayo imechukuliwa na Mganda Sekisambu
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BAHATI ‘ALIYOIPIGA TEKE’ JOHN BOCCO YAANGUKIA KWA MGANDA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top