• HABARI MPYA

    Sunday, July 26, 2015

    GOR MAHIA WAPAA KILELENI KUNDI A KOMBE LA KAGAME, YANGA NA KHARTOUM SASA KAZI IPO

    Kinara wa mabao Kombe la kagame, Michael Olunga wa Gor Mahia (kulia) akipambana na beki Mrundi wa Telecom, Hussein Butoyi leo
    GOR Mahia ya Kenya imepanda kileleni mwa Kundi A kufuatia ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya vibonde Telecom ya Djibouti katika mchezo wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame mchana wa leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Kogalo sasa wanafikisha pointi 10 baada ya kushinda mechi tatu za kundi hilo, dhidi ya Yanga SC 2-1, KMKM 3-1 na Telecom 3-1, wakati mechi nyingine walitoka sare ya 1-1 na Khartoum N ya Sudan. 
    Kiungo wa zamani wa Azam FC, George Odhiambo ‘Blackberry’ aliifungia Gor bao la kwanza dakika ya 13, kabla ya Michael Olunga kufunga bao lake la nne katika mashindano ya mwaka huu dakika ya 28
    Kipindi cha kwanza kilimalizika timu ya Mscotland, Frank Nutal ikiwa mbele kwa mabao 2-0 na kipindi cha pili, Telecom walifanikiwa kupata bao dakika ya 74 kupitia kwa Said Hassan Elmi.
    Enock Agwanda akaihakikishia Gor ushindi kwa bao zuri dakika ya 79 na sasa mabingwa wa Kenya wanawateremshia Khartoum nafasi ya pili, mbele Yanga SC iliyo nafasi ya tatu.
    Khartoum wenye pointi saba na Yanga pointi sita watahitimisha mechi za makundi Kombe la Kagame 2015 kwa mchezo baina yao kuanzia Saa 10:00 jioni ya leo Uwanja wa Taifa.
    Khartoum wanaweza kurejea kileleni iwapo watashinda kwa wastani mzuri wa mabao dhidi ya Yanga SC. 
    Mshindi wa kwanza wa Kundi A atakutana na Malakia ya Sudan Kusini katika Robo Fainali, mshindi wa pili atakutana na Azam FC wakati mshindi wa tatu atakutana na APR ya Rwanda.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: GOR MAHIA WAPAA KILELENI KUNDI A KOMBE LA KAGAME, YANGA NA KHARTOUM SASA KAZI IPO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top