• HABARI MPYA

    Thursday, July 30, 2015

    YANGA SASA WAJITATHMINI VIZURI BAADA YA KUTOLEWA NA AZAM KAGAME

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    NDOTO za Yanga SC kutwaa taji la sita la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame zimeyeyuka jana baada ya kupigwa na Azam FC kwa penalti 5-3 kufuatia sare ya 0-0 ndani ya dakika 90.
    Katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, shujaa wa Azam FC alikuwa ni kipa Aishi Salum Manula aliyepangua penalti ya beki mpya wa kushoto wa Yanga SC, Mwinyi Hajji Mngwali.
    Aggrey Morris akaenda kufunga penalti ya mwisho ya Azam FC na kuzima kabisa matarumbeta na shangwe za Yanga SC Uwanja wa Taifa.
    Penalti nyingine za Azam FC zilifungwa na Kipre Herman Tchetche, Serge Wawa Pascal wote raia wa Ivory Coast, John Bocco na Himid Mao, wakati za Yanga SC zilifungwa na Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Salum Telela na Godfrey Mwashiuya.  
    Kwa ujumla, mchezo wa jana timu zote zilicheza kwa tahadhari zaidi kana kwamba zilihitaji kwenda kuumalizia mchezo huo katika matuta.
    Mabeki Nadir Haroub 'Cannavaro' wa Yanga SC na Serge Wawa Pascal wa Azam FC wakiwania mpira wa juu jana
    Makocha wa Yanga SC, kutoka kulia Pluijm, Mkwasa na kocha wa makipa Juma Pondamali



    Azam FC sasa itamenyana na KCCA ya Uganda katika Nusu ya pili Ijumaa, baada ya Khartoum N na Gor Mahia kupambana katika Nusu Fainali ya kwanza.
    Utamu ni kwamba, Nusu Fainali zote zitakuwa marudio ya mechi za makundi, kwanza Azam FC iliifunga 1-0 KCCA katika mechi ya Kundi C na Khartoum N ilitoka sare ya 1-1 na Gor Mahia katika mchezo wa Kundi A.
    Yanga SC ambayo imetwaa Kombe la Kagame mara tano katika miaka ya 1975, 1993, 1999, 2011 na 2012 sasa wanarudi kwenye maandalizi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, wakianza na mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya hao hao, Azam FC.
    Katika michuano ya Kagame ya mwaka huu, Yanga SC inayofundishwa na Mholanzi, Hans van der Pluijm na mzalendo, Charles Boniface Mkwasa ambaye pia ni kocha wa timu ya taifa, Taifa Stars- ilitumia wachezaji wake wote nyota iliyonao.
    Ambao hawakutumiwa, basi hawamo kwenye mipango ya makocha- na wengine tayari wapo njiani kutolewa kwa mkopo.
    Wachezaji wapya kikosini Yanga SC walikuwa ni wazalendo, Malimi Busungu, Godfrey Mwashiuya, Deus Kaseke, Mwinyi Mngwali na wageni Joseph Zutah na Donald Ngoma.
    Azam FC waliwapumzisha baadhi yao nyota wao kama Kipre Balou, Brian Majwega na hawakutaka kuwatumia wachezaji wapya, Allan Wanga na Ramadhani Singano ‘Messi’.
    Maana yake hata kama Azam FC wangetolewa, wangekuwa na cha kuzungumza kwamba hawakuwa na baadhi ya nyota wao kwenye mashindano.
    Lakini Yanga SC walikuwa ‘full muziki’ na hawakuwa na matokeo ya kufurahisha sana katika mashindano haya kwa ujumla.
    Hawa ndiyo wawakilishi wetu katika Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani- michuano ambayo Tanzania haina rekodi ya kufanya vizuri.
    Michuano ya Kagame kwa Yanga imekwisha- lakini mashindnao yenyewe haswa yatafikia tamati Jumapili. Hii ni fursa nzuri sasa kwa benchi la Ufundi la Yanga SC kuitathmini timu upya kuelekea Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa mwakani.    
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA SASA WAJITATHMINI VIZURI BAADA YA KUTOLEWA NA AZAM KAGAME Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top