• HABARI MPYA

    Monday, July 20, 2015

    MWAMEJA: UKIPA SI ‘LELE MAMA’, JIKAZENI VIJANA SIKUITWA TANZANIA ONE BURE BURE

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KIPA wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, Mwameja Mohamed Mwameja aliyewika Simba SC, amesema kwamba ukipa si ‘lele mama’.
    Mwameja aliyewahi pia kudakia Ndovu ya Arusha na Coastal Union ya Tanga, amewataka makipa kujituma na kuzingatia nidhamu kwenye fani hiyo ili kufikia mafanikio.
    Mwameja ambaye alipewa jina la Tanzania One kwa umahiri wake wa kusimama imara langoni amekiri kuwa kuna magolikipa wengi wa sasa ambao hawajitumi kama ipasavyo na hivyo kuleta mafanikio kwenye klabu zao na Taifa kwa ujumla.
    Mwameja amefanya mahojiano na tovuti ya Simba SC na kusema kwamba nidhamu na kujituma ndio siri ya mafanikio yake alioyapata wakati akiwa Simba.
    Pamoja na kustaafu tangu mwaka 2002, lakini Mwameja ameendelea kudakia timu za maveterani ili kulinda utimamu wake wa mwili

    “Nafasi hii ya kuwa mlinda mlango inahitaji umakini wa hali ya juu sana, kujituma na nidhamu jambo ambalo mpaka sasa bado walinda mlango wengi wanakosa sifa na tunu hizo muhimu katika soka,”amesema Mwameja aliyewahi pia kudakia Reading ya England.
    Kwa upande mwingine Mwameja ambaye anashiriki mafunzo ya Makocha wa makipa ya FIFA yanayofanyika uwanja wa Karume yalioandaliwa na TFF, ameushukuru uongozi wa Simba kwa kutambua umuhimu wake na kumuwezesha kushiriki kozi hiyo ambayo kwa mara ya kwanza inafanyika hapa Tanzania.
    “Unajua ujuzi hauozi, mafunzo ninayoyapata hapa kwa hakika yananiongezea uwezo mkubwa sana tofauti na uzoefu wangu na kufanya kazi kwa mazoea. Kwa kweli Simba naishukuru sana kwa maamuzi yake haya ya busara ya kuniwezesha kushiriki mafunzo haya yanayofanyika kwa mara ya kwanza Tanzania,”. 
    “Mimi ni mtu ninayeamini sana kwenye kujenga urithi kwa vijana na naamini kuwa ujuzi nitakaoendelea kuupata hapa, nitautumia kujenga makipa imara wa nchi hii,” alisema Mwameja, aliyezaliwa Desemba 21, mwaka 1964 Mwakidila mkoani Tanga. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MWAMEJA: UKIPA SI ‘LELE MAMA’, JIKAZENI VIJANA SIKUITWA TANZANIA ONE BURE BURE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top