• HABARI MPYA

    Tuesday, July 28, 2015

    AZAM HAIFUNGIKI, YANGA PENALTI ‘MAAMUMA’, DAKIKA 90 ZIKIISHA KWA SARE NINI MATARAJIO?

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    NYASI za Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kesho zitakanyagika kwa mchezo wa miamba ya Jiji, Azam FC na Yanga SC katika Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.
    Itakuwa mara ya pili, Yanga SC na Azam FC kukutana katika Kombe la Kagame, baada ya mwaka 2012 kukutana katika fainali pale pale Uwanja wa Taifa wa Dar es Salaam.
    Ilikuwa Julai 28, mwaka 2012 katika mchezo uliochezeshwa na refa Thierry Nkurunziza wa Burundi, Yanga SC ilipoibuka na ushindi wa mabao 2-0 wafungaji Hamisi Kiiza ‘Diego’ dakika ya 44 na Said Bahanunzi ‘Spider Man’ dakika ya 90 na ushei.
    Mabeki wanaoweza kucheza kama viungo pia, Shomary Kapombe wa Azam FC (kulia) na Mbuyu Twite wa Yanga SC (kushoto) wakigombea mpira katika mchezo uliopita uliozikutanisha timu hizo katika Ligi Kuu. 

    Iwapo dakika 90 za mchezo zitamalizika kwa sare yoyote, sharia ya mikwaju ya penaltI itachukua nafasi moja kwa moja.
    Hadi kufika hatua hii, Azam FC haijafungwa hata bao moja- maana yake ni timu yenye ukuta imara zaidi katika mashindano haya hadi sasa.
    Katika mechi za makundi, Yanga SC ilibahatika kupata jumla ya penalti tatu katika mechi mbili na kwa bahati mbaya, walikosa zote. 
    Ikiwa nyuma kwa mabao 2-1 mbele ya Gor Mahia ya Kenya katika mchezo wa kwanza wa Kundi A, Yanga ilipewa penalti dakika za lala salama, lakini Nahodha wake, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ akaenda kukosa.
    Katika mchezo wa pili wa kundi hilo dhidi ya Telecom ya Djibouti, Yanga SC walikosa penalti mbili mfululizo, ya kwanza Amisi Tambwe na ya pili Simon Msuva zote kipindi cha kwanza. Yanga ilishinda 3-0.
    Cannavaro, Tambwe na Msuva ni wachezaji wanaoaminiwa zaidi Yanga SC kwa kupiga mikwaju ya penalti, lakini kwa kushindwa kufunga kwenye mechi za makundi, maana yake hali ya kujiamini kwao binafasi imepungua.
    Je, tutarajie nini iwapo mchezo utamalizika kwa sare na penalti zikapewa nafasi ya kuamua mshindi? Kesho si mbali, zimebaki saa kadhaa tu. Tuombe uzima ‘Inshaallah’.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM HAIFUNGIKI, YANGA PENALTI ‘MAAMUMA’, DAKIKA 90 ZIKIISHA KWA SARE NINI MATARAJIO? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top