• HABARI MPYA

    Friday, December 27, 2013

    MKWASA: NAJIAMINI, NDIYO MAANA NIMEKUBALI KURUDI YANGA

    Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
    KOCHA Mkuu wa Ruvu Shooting, Charles Boniface Mkwasa amekubali kushuka cheo hadi kuwa Kocha Msaidizi wa klabu ya Yanga SC ya Dar es Salaam na wakati wowote atasaini Mkataba wa kuanza kazi Jangwani.
    Mkwasa aliiongoza kwa mara ya mwisho Ruvu Shooting jana ikifungwa mabao 3-0 na Azam FC katika mchezo wa kirafiki, Uwanja wa Azam Complex na baada ya mechi hiyo akasema; “Kweli, niko njiani kurejea Yanga, lakini bado sijasaini Mkataba, tumefikia makubaliano tu,”alisema kiungo huyo wa zamani wa kimataifa wa Tanzania.
    Najiamini; Charles Boniface Mkwasa amesema anajiamini ndiyo maana amekubali kazi Yanga
       
    Mkwasa amesema makocha wengi wa Tanzania kwa sasa wanaogopa kufanya kazi timu za Simba na Yanga kutokana na desturi ya kufukuza walimu ovyo, lakini yeye anajiamini atafanya kazi nzuri ambayo itamuepushia ‘balaa’ la kutupiwa virago.
    “Mimi ni mwalimu ambaye najiamini, naweza kufanya kazi sehemu yoyote wakati wowote, hii Yanga SC mimi nimekwishafanya kazi kwa mafanikio kama mchezaji na kama kocha pia, sina wasiwasi wowote,”alisema Mkwasa maarufu kama Master enzi zake anatamba katika safu ya kiungo.
    Charles Boniface Mkwasa aliyezaliwa Aprili 10, mwaka 1955 mjini Morogoro alijiunga na Yanga SC kwa mara ya kwanza kama mchezaji mwaka 1978 akitokea Tumbaku ya Morogoro na akacheza hadi 1988 alipostaafu na kwenda kuanza maisha ya ukocha katika klabu ya Super Star ya Dar es Salaam mwaka 1989.
    Mwaka 1990 kwa ufadhili wa waliokuwa wafadhili wa Yanga SC, chini ya marehemu Mohamed Viran ‘Babu’, Mkwasa alikwenda kusomea ukocha nchini Brazil na aliporejea akawa kocha Msaidizi wa Yanga chini ya marehemu Syllersaid Salmin Kahema Mziray.
    Mkwasa alianza vizuri Yanga SC baada ya kuiwezesha kufika Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati visiwani Zanzibar mwaka 1992 ambako walifungwa na Simba SC kwa penalti 5-4 kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 120. 
    Mwaka 1993 Mkwasa akiwa Msaidizi wa Mrundi, marehemu Nzoyisaba Tauzany ‘Bundes’ akaiwezesha Yanga kutwaa Kombe hilo ambalo sasa linaitwa Kagame mjini Kampala, Uganda kabla ya mwaka 1994 kuhamia Sigara alipokwenda kuwa Kocha Mkuu.
    Mkwasa aliifanya Sigara kuwa tishio katika soka ya Tanzania hadi kushiriki michuano ya Afrika, kabla ya kutupwa na kampuni na timu kuchukuliwa wafanyabiashara kuanzia Azim Dewji, baadaye Alex Kajumulo na Merey Balhaboub. TCC ilipoitema Sigara, Mkwasa akaenda kufundisha nje ya nchi kwa mara ya kwanza, katika klabu ya Al Khaboura ya Oman mwaka 1997.
    Alikaa Oman kwa msimu mmoja kabla ya kurejea mwaka 1998 na kujiunga na Prisons ya Mbeya, ambayo mwaka 1999 aliipa ubingwa wa iliyokuwa Ligi Kuu ya Muungano na kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2000.  
    Mume huyo wa Betty Mkwasa mwaka 2000 alikwenda Ujerumani kusomea ukocha na aliporejea mwaka 2001 akajiunga na Coastal Union ya Tanga kabla ya mwaka huo huo baadaye kuajiriwa tena na Yanga kama kocha Mkuu, akichukua nafasi ya Mkongo Raoul Jean Pierre Shungu.
    Master Mkwasa aliendelea kuwa kocha wa mafanikio Jangwani baada ya kuiwezesha timu hiyo kufika hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa, ambako ilitolewa kwa mbinde na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini kwa jumla ya mabao 6-5, sare ya 3-3 Mwanza na kufungwa 3-2 Afrika Kusini.   
    Mwaka 2003 Mkwasa aliachana na Yanga akaenda kufungua kituo chake cha mafunzo ya soka kwa vijana, Pangolin kilichoibua vipaji kadhaa kabla ya mwaka 2005 kuchukuliwa na Moro United, enzi hizo ikiwa chini ya bilionea Merey Balhaboub.
    Mkwasa aliifanya Moro kuwa tishio na hadi ikacheza Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati mwaka 2006 mjini Dar es Salaam ikifungwa 2-1 na Polisi ya Uganda iliyoibuka bingwa, katika mechi pekee ya klabu kuhudhuriwa na Rais wa sasa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete.
    Mwaka 2007 Mkwasa akaenda Miembeni ya Zanzibar aliyoipa ubingwa wa visiwani humo kabla ya 2009 kuja Dar es Salaam kuifundisha African Lyon hadi 2010 alipokwenda Ruvu Shooting ya Pwani, ambako amefanya kazi hadi sasa anarejea Yanga kama kocha Msaidizi.
    Mkwasa pia amefundisha kwa mafanikio timu za taifa kuanzia za vijana, wakubwa hadi wanawake, mwaka 2001 akiwa na marehemu Mziray waliipa Taifa Stars Kombe la Castle mjini Mwanza wakati timu ya wanawake, Twiga Stars ameipa tiketi mbili za michuano ya Afrika, Mataifa ya Afrika 2010 na Michezo ya Afrika 2012.
    Yanga inamchukua Mkwasa kuwa Msaidizi wa kocha mpya wanayemtafuta kwa sasa, baada ya kufukuza benchi zima la Ufundi chini ya Kocha Mholanzi, Ernie Bradts na Wasaidizi wake, Freddy Felix Minziro na Razack Ssiwa.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MKWASA: NAJIAMINI, NDIYO MAANA NIMEKUBALI KURUDI YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top