• HABARI MPYA

    Sunday, December 22, 2013

    MANJI: HATUKUMSAJILI KASEJA AIFUNGE SIMBA, ASEMA MSIMBAZI WALISHINDA MECHI YA FETE JANA

    Na Mahmoud Zubeiry, Jangwani
    MWENYEKITI wa Yanga SC, Yussuf Manji amesema kwamba hawakumsajili Juma Kaseja kwa ajili ya kuifunga Simba SC, bali wamemsajili awasaidie kwenye michuano ya Afrika.
    Manji ameyasema hayo leo asubuhi makao makuu ya klabu, Jangwani, Dar es Salaam wakati akizungumza na Waandishi wa Habari, siku moja baada ya Yanga kufungwa 3-1 na Simba SC katika mechi ya Nani Mtani Jembe Uwanja wa Taifa, Kaseja akiwa langoni.
    Manji akizungumza na Waandishi wa Habari leo makao makuu ya Yanga. Kushoto ni Makamu Mwenyekiti, Clement Sanga

    Manji alikuwa akimjibu Katibu wa Baraza la Wazee la Yanga, Mzee Ibrahim Akilimali aliyeushutumu uongozi kusajili Juma Kaseja ni makosa.
    “Huyu mzee nadhani umri umemzidi, lakini nataka nimkumbushe, huyo Ivo Mapunda aliondoka Yanga akiwa anatumikia adhabu ya kufungiwa miezi sita na uongzi wa wakati huo kwa tuhuma za kufungisha kwenye mechi na Simba SC,”.
    “Lakini pia nataka nimuulize, wakati Simba inarudisha mabao yote matatu Kaseja alikuwapo langoni? Nadhani hivi vitu si vizuri, tuache kulaumiana tushikamane kwa mustakabali mzuri wa timu,”alisema Manji.
    Manji amesema wanaheshimu uwezo wa Kaseja kwa sababu ndiye kipa aliyedaka mechi nyingi za mashindano ya Afrika kati ya makipa wote nchini, hivyo thamani yake haitashuka kwa kufungwa mabao matatu jana.
    Pamoja na hayo, Manji amesema kwamba mechi ya jana haikuwa na uzito wowote kwao ni sawa na bonanza au fete, hivyo kufungwa haijawaumiza.
    “Tuliamua kucheza kumfurahisha  mdhamini TBL, tumefungwa lakini bado tunaongoza ligi, hatujapoteza pointi hata moja, ile ilikuwa fete tu,”alisema Manji.
    Manji amekiri Simba SC walicheza vizuri zaidi jana na walistahili ushindi na anawapongeza kwa hilo, pamoja na wadhamini, TBL kwa kuandaa mechi hiyo.
    Manji amesema kuelekea mzunguko wa pili wa Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Afrika wataboresha timu na benchi la ufundi na timu itaenda tena kambini Ulaya, hivyo anaamini mwakani makali yao yatafufuka na watatetea ubingwa.   
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MANJI: HATUKUMSAJILI KASEJA AIFUNGE SIMBA, ASEMA MSIMBAZI WALISHINDA MECHI YA FETE JANA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top