• HABARI MPYA

    Tuesday, December 31, 2013

    RASMI, YANGA YAJITOA KOMBE LA MAPINDUZI, OKWI NA KIIZA SIMU ZAO HAZIPATIKANI TANGU ASUBUHI

    Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
    RASMI. Yanga SC imejitoa katika michuano ya Kombe la Mapinduzi, kwa sababu timu yao haina benchi la Ufundi, baada ya kufukuzwa kwa Kocha Mkuu, Ernie Brandts.
    Ofisa Habari wa Yanga SC, Baraka Kizuguto ameiambia BIN ZUBEIRY muda huu kwamba, uongozi umefikia hatua hiyo kwa sababu bado hawajapata benchi jipya la Ufundi.
    Kikosi cha Yanga kilichofungwa 3-1 Kombe la Mapinduzi 

    Yanga SC ilikuwa imepangwa Kundi C la michuano hiyo inayoanza kesho pamoja na Spice Star, Azam FC na Tusker ya Kenya- maana yake kwa kujitoa kwao, Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) kitalazimika kupanga upya Ratiba yake au kuiingiza timu nyingine katika nafasi ya mabingwa hao wa Bara.
    Mapema jana, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga SC, Mussa Katabaro aliiambia BIN ZUBEIRY kwamba wanachelewa kwenda Zanzibar kwa sababu hawajapata mwaliko na waliwaandikia barua ZFA juu ya hilo, lakini hadi sasa hawajapata majibu.
    Wakati huo huo: Wachezaji wawili Waganda wa Yanga SC, Emmanuel Arnold Okwi na Hamisi Friday Kiiza waliotarajiwa kuwasili leo Dar es Salaam kutoka kwao, Kampala kujiunga na wenzao wamekuwa wakipigiwa simu tangu asubuhi, lakini hazipatikani.
    Kizuguto amesema kwamba jana alizungumza na wachezaji hao na wakamthibitisha kwamba wanakuja leo, lakini kila akiwapigia simu hawapatikani. 
    Je, wako angani kwenye ndege wanakuja, au wamezima simu kuepuka usumbufu? 
    Ikumbukwe Yanga SC ilimfukuza kocha wake, Mholanzi, Ernie Brandts baada ya kufungwa mabao 3-1 na mahasimu wao, Simba SC katika mechi ya Nani Mtani Jembe Desemba 21, mwaka huu.
    Pamoja na kumfukuza Mholanzi huyo, Yanga inataka kuwafukuza na Wasaidizi wake pia na tayari imekwishafikia makubaliano na Charles Boniface Mkwasa, awe kocha Msaidizi, nafasi ya Freddy Felix Minziro. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: RASMI, YANGA YAJITOA KOMBE LA MAPINDUZI, OKWI NA KIIZA SIMU ZAO HAZIPATIKANI TANGU ASUBUHI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top