• HABARI MPYA

    Wednesday, December 18, 2013

    YANGA SC WAINGIA KAMBINI PROTEA BILA OKWI

    Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
    YANGA SC wameingia kambini jioni hii katika hoteli ya Protea, Dar es Salaam kujiandaa na mpambano dhidi ya mahasimu wao wa jadi, Simba SC wa Nani Mtani Jembe, lakini mshambuliaji mpya Emmanuel Arnold Okwi bado hajawasili.
    Baadhi ya wapenzi wa Yanga na Waandishi wa Habari walifika Uwanja Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam kumpokea Okwi, lakini hakutokea na hakukuwa na taarifa za kutokea hadi wakaondoka.
    Kikosi cha Yanga kilichotoa sare ya 3-3 na Simba SC kikitoka kuongoza 3-0 hadi mapumziko katika mchezo uliopita wa Ligi Kuu.

    Lakini kocha Mholanzi, Ernie Brandts ameingia kambini jioni hii na wachezaji wake wote wengine kujiandaa na mchezo wa Jumamosi unaoandaliwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), wadhamini wa Simba na Yanga.
    Viingilio vya mechi hiyo ni Sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya kijani, bluu Sh. 7,000, rangi ya chungwa Sh. 10,000, VIP C Sh. 15,000, VIP B Sh. 20,000 wakati VIP A Sh. 40,000. 
    Tiketi zitaanza kuuzwa siku moja katika vituo mbalimbali, mchezo huo utafanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.
    Vituo ambavyo tiketi hizo zitauzwa keshokutwa (Ijumaa) ni Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Sokoni Kariakoo, mgahawa wa Steers ulioko mtaa wa Ohio/Samora, Oilcom Ubungo, Kituo cha Mafuta Buguruni, Dar Live Mbagala, Uwanja wa Uhuru, na BMM Salon iliyoko Sinza Madukani.
    Mechi hiyo itachezeshwa na Ramadhan Ibada (Kibo) kutoka Zanzibar, atakayesaidiwa na Ferdinand Chacha wa Bukoba, na Simon Charles kutoka Dodoma. Mwamuzi wa akiba ni Israel Nkongo wa Dar es Salaam wakati mtathimini wa waamuzi ni Soud Abdi wa Arusha.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA SC WAINGIA KAMBINI PROTEA BILA OKWI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top