• HABARI MPYA

    Tuesday, December 17, 2013

    HANS POPPE AWAAMBIA YANGA SC; “KWA OKWI WAMELIWA”

    Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
    MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili ya klabu ya Simba SC ya Dar es Salaam, Zacharia Hans Poppe amesema kwamba watani wao wa jadi, Yanga SC wameingia mkenge kumsajili Emmanuel Okwi na labda watamtumia kwenye mchezo wa Nani Mtani Jembe pekee, lakini zaidi ya hapo hatacheza Jangwani kwenye michuano yoyote rasmi.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY jioni hii, Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), amesema kwamba Okwi ni mchezaji halali wa Etoile du Sahel ya Tunisia na hawezi kucheza Yanga.
    Wameliwa; Zacharia Hans Poppe amewaambia Yanga SC wameingizwa mkenge kwa Okwi 

    Okwi akisaini Yanga SC mbele ya Mjumbe wa Kamati ya Mashindano ya klabu hiyo, Mussa Katabaro kushoto na wakili wa mchezaji huyo kulia

    “Mimi sina wasiwasi, naangalia tu sarakasi zao nikiwa najua wataangukia wapi. Yule mchezaji Yanga wameingizwa mkenge na FUFA (Shirikisho la Soka Uganda). Kwa sababu, Etoile ilimtoa kwa mkopo SC Villa na ndiyo maana hata FUFA walipotaka kumtumia katika CHAN, wakaambiwa haiwezekani kwa kuwa yule ni mchezaji wa Etoile,”alisema Hans Poppe.
    Jumapili Yanga SC ya Dar es Salaam ilitangaza kumsajili mshambuliaji wa zamani wa Simba SC, Emmanuel Arnold Okwi raia wa Uganda kwa Mkataba wa misimu miwili na nusu. 
    Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya klabu ya Yanga, Abdallah Ahmed Bin Kleb alisema siku hiyo Dar es Salaam kwamba wamemsajili Okwi na ataanza kuichezea timu hiyo mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Bara na michuano ya Afrika.
    Etoile du Sahel ya Tunisia ilimnunua Okwi kutoka Simba SC Januari mwaka huu kwa dola za Kimarekani 300,000, lakini mchezaji huyo akaamua kuachana na klabu hiyo na kurejea kupumzika kwao Uganda, kwa madai hakulipwa mishahara kwa miezi mitatu.
    Wakati huo huo, Etoile hadi sasa haijailipa Simba SC fedha zake za kumnunua mchezaji huyo na sakata lake limefikishwa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
    Baada ya Okwi kukaa bila kucheza kwa miezi sita, Shirikisho la Soka la Uganda (FUFA) lilimpigania aruhusiwe kurejea nyumbani kuichezea SC Villa ya huko ili kunusuru kiwango chake. 
    Hata hivyo, baada ya kung’ara na timu ya taifa ya Uganda ‘The Ceanes’ nchini Kenya kwenye Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge mwezi huu, Okwi amesajiliwa Yanga SC.
    Bin Kleb alisema kwamba walimsajili Okwi tarkiban siku sita zilizopita, lakini Hati yake ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) ilipatikana Jumapili na ndiyo maana wakaamua kumtangaza.
    Alipoulizwa kuhusu utata wa sakata lake ambalo limefika hadi FIFA, Kleb alisema; “Tumefuatilia kote, hadi kwa wanasheria, na tumefanikiwa kupata hadi ITC yake, nawaambia mashabiki wa Yanga wajue viongozi wao wanafanya kazi, hatuna stori nyingi, sisi tunafanya vitendo, tunafanya kazi kwa siri sana,”.
    “Na tumepitia sehemu zote, tumeona kabisa tuko sahihi katika kumsajili mchezaji huyu na hakutakuwa na tatizo lolote upande wetu,”alisema. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HANS POPPE AWAAMBIA YANGA SC; “KWA OKWI WAMELIWA” Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top