• HABARI MPYA

    Sunday, December 22, 2013

    TFF IWASILIANE NA FIFA KUHUSU OKWI, ISIPUMBAZWE NA KAULI ZA FUFA

    SAKATA la mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda, Emmanuel Okwi limechukua sura mpya baada ya Shirikisho la Soka la Uganda (FUFA) kusema ni halali kuchezea Yanga.
    Okwi alikuwa mchezaji wa Simba SC ya Dar es Salaam tangu mwaka 2010 hadi alipouzwa Etoile du Sahel ya Tunisia kwa dola za Kimarekani 300,000, lakini mchezaji huyo akaamua kuachana na klabu hiyo na kurejea kupumzika kwao Uganda, kwa madai hakulipwa mishahara kwa miezi mitatu.

    Wakati huo huo, Etoile hadi sasa haijailipa Simba SC fedha zake za kumnunua mchezaji huyo na sakata lake limefikishwa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
    Baada ya Okwi kukaa bila kucheza kwa miezi sita, Shirikisho la Soka la Uganda (FUFA) lilimpigania aruhusiwe kurejea nyumbani kuichezea SC Villa ya huko ili kunusuru kiwango chake. 
    Ukifuata historia hii unaweza kuona huyu ni mchezaji halali wa Etoile, inayodaiwa na Simba SC dola 300,000, lakini Yanga SC, wanasema wamejiridhisha wako sahihi kabisa katika kumsajili Okwi kutoka Villa.
    Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya klabu ya Yanga, Abdallah Ahmed Bin Kleb alisema Jumapili mjini Dar es Salaam kwamba wamemsajili Okwi na ataanza kuichezea timu hiyo mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Bara na michuano ya Afrika kwa misimu miwili na nusu.
    Bin Kleb alisema kwamba walimsajili Okwi tarkiban siku sita zilizopita, lakini Hati yake ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) ilipatikana Jumapili na ndiyo maana wakaamua kumtangaza siku hiyo.
    “Tumefuatilia kote, hadi kwa wanasheria, na tumefanikiwa kupata hadi ITC yake, nawaambia mashabiki wa Yanga wajue viongozi wao wanafanya kazi, hatuna stori nyingi, sisi tunafanya vitendo, tunafanya kazi kwa siri sana,”. “Na tumepitia sehemu zote, tumeona kabisa tuko sahihi katika kumsajili mchezaji huyu na hakutakuwa na tatizo lolote upande wetu,”alisema.
    Okwi aliwasili juzi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam tayari kuanza kuutumikia Mkataba wake wa miaka miwili ndani ya klabu ya Yanga SC ya Tanzania na kusema; “Nimekuja Yanga kufanya kazi,” na alipoulizwa kuhusu utata wa usajili wake, akasema; “Mimi nimekuja kufanya kazi, hayo mengine, mamlaka husika zitajua,”alisema Okwi aliyekuwa amevalia jezi nambari 25 ya Yanga.   
    Na Kaimu Mkurugenzi wa Mashindano wa Shirikisho la Soka Uganda (FUFA), Decolas Kiiza, amesema kwamba Shikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) limeridhia mshambuliaji Emmanuel Arnold Okwi kujiunga na mabingwa wa Tanzania, Yanga SC.
    “Ndiyo, tuliwaandikia FIFA na wamesema mchezaji huyo alikuwa huru kusajiliwa,”alisema  Kiiza. Mapema wiki hii, Ofisa Mtendaji Mkuu wa FUFA na kiungo wa zamani wa SC Villa ya Uganda na timu ya taifa ‘The Cranes’,  Edgar Watson, alisema waliwasiliana na FIFA kupata ufafanuzi zaidi juu ya suala la Okwi kusajiliwa Yanga.
    Lakini bado TFF inapaswa kufuata utaratibu ili kujiridhisha yenyewe kabla ya kumuidhinisha huyo mchezaji kucheza Yanga, hiyo ni faida kwa klabu yenyewe pia baadaye.
    TP Mazembe iliwahi kupokonywa ushindi kwa kumtumia mchezaji ambaye alikuwa bado ana Mkataba na klabu nyingine na Simba iliyokuwa imetolewa na timu hiyo ya DRC ikanufaika kwa kurejeshwa kwenye michuano ya Afrika.
    Hivyo TFF isijiridhishe kwa maelezo ya Kiiza wa FUFA na Yanga, ifanye mawasiliano yenyewe na FIFA, jambo ambalo ni jepesi tu.  
    Yote kwa yote, bado haifuti deni la Etoile kwa Simba SC la dola za Kimarekani 300,000 kama kweli yalikuwapo makubaliano ya kiwango hicho cha fedha kwa ajili ya mauziano ya mchezaji huyo, basi zitalipwa.
    Na kwa sababu kuna kanuni ya FIFA inayosema klabu inatakiwa kuwa imemaliza kulipa malipo ya fedha za kumnunua mchezaji kabla ya kumaliza Mkataba wake au kumtoa sehemu nyingine, sasa Etoile watalazimika kuilipa Simba SC mara moja kama walishindwa kesi na Okwi.
    Simba SC wangekuwa wamekwishafika katika hatua nzuri kwenye madai hayo, kama wangekuwa wamelipa ada ya dola za Kimarekani 10,000 baada ya kufungua kesi FIFA, lakini kwa kupeleka malalamiko bila ada hiyo, kesi yao haijawezwa kusikilizwa. Ila sasa ili kupata haki yao, Simba lazima walipe fedha hizo FIFA iweze kuisikiliza kesi hiyo na kutoa hukumu.
    Kama kweli Simba waliandikishiana na Etoile malipo yanayotajwa, basi wana Simba hawana haja ya kuwa na kimuhemuhe, fedha zao zitalipwa tu. Jumapili njema.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TFF IWASILIANE NA FIFA KUHUSU OKWI, ISIPUMBAZWE NA KAULI ZA FUFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top