• HABARI MPYA

    Wednesday, December 18, 2013

    SIMBA NA YANGA MTANI JEMBE KIINGILIO BUKU TANO

    Na Boniface Wambura, Ilala
    KIINGILIO cha chini kwenye mechi ya Mtani Jembe kati ya Simba na Yanga itakayochezwa Jumamosi (Desemba 21 mwaka huu) ni sh. 5,000. Kiingilio hicho ni kwa viti vya rangi ya kijani ambavyo ni 19,648.
    Kwa upande wa viti vya rangi ya bluu kiingilio ni sh. 7,000, viti vya rangi ya chungwa itakuwa sh. 10,000, VIP C kiingilio ni sh. 15,000, VIP B itakuwa sh. 20,000 wakati VIP A yenye viti 748 tu tiketi moja itapatikana kwa sh. 40,000. 
    Tiketi zitaanza kuuzwa siku moja katika vituo mbalimbali, mchezo huo utafanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.
    Mrisho Ngassa wa Yanga akijaribu kubinuka tik tak katika mechi iliyopita ya watani ya Ligi Kuu ya Bara iliyoisha kwa sare ya 3-3. Je, Jumamosi itakuwaje?

    Vituo ambavyo tiketi hizo zitauzwa keshokutwa (Ijumaa) ni Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Sokoni Kariakoo, mgahawa wa Steers ulioko mtaa wa Ohio/Samora, Oilcom Ubungo, Kituo cha Mafuta Buguruni, Dar Live Mbagala, Uwanja wa Uhuru, na BMM Salon iliyoko Sinza Madukani.
    Mechi hiyo itachezeshwa na Ramadhan Ibada (Kibo) kutoka Zanzibar, ambapo atasaidiwa na Ferdinand Chacha wa Bukoba, na Simon Charles kutoka Dodoma. Mwamuzi wa akiba ni Israel Nkongo wa Dar es Salaam wakati mtathimini wa waamuzi ni Soud Abdi wa Arusha.
    Wakati huo huo; Kikosi cha wachezaji 20 na viongozi tisa cha timu ya Tanzania ya wasichana chini ya miaka 20 (Tanzanite) kimewasili leo jijini Johannesburg tayari kwa mechi dhidi ya wenyeji Afrika Kusini (Batsesana).
    Mechi hiyo ya marudiano ya raundi ya pili kuwania tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia kwa wasichana wenye umri chini ya miaka 20 zitakazofanyika mwakani nchini Canada.
    Tanzanite imefikia Millpark Garden Court Hotel tayari kwa mechi hiyo itakayochezwa Jumamosi katika Uwanja wa Dobsonville ulioko Soweto, Johannesburg kuanzia saa 9.30 alasiri kwa saa za Afrika Kusini.
    Wachezaji wa Tanzanite walioko katika kikosi hicho ni Amina Bilali, Amina Hemed, Amisa Hussein, Anastaz Katunzi, Anna Mwaisula, Belina Nyamwihula, Donisia Minja, Fatuma Maonyo, Happiness Mwaipaja, Latifa Salum, Maimuna Kaimu, Najiat Idrisa, Neema Kiniga, Rehema Rhamia, Sada Hussein, Shelda Mafuru, Stumai Athuman, Tatu Salum, Theresa Kashilim na Vumilia Maarifa.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA NA YANGA MTANI JEMBE KIINGILIO BUKU TANO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top