• HABARI MPYA

    Wednesday, March 21, 2012

    MASHABIKI WA YANGA KUNG'ARA NA JEZI ZA SETIF JUMAPILI TAIFA


    BAADHI ya mashabiki wa Yanga wameanza kununua jezi za timu ya ESS Setif ya Algeria, ambayo Jumapili itacheza na wapinzani wao wa jadi, Simba SC mjini Dar es Salaam.
    Imekuwa desturi sasa kwa mashabiki wa timu hizo kuvaa jezi za wapinzani wa wapinzani wao na kuwashangilia kwenye mechi zao, kama mwendelezo wa kulipiana visasi.
    Simba walivaa jezi za Zamalek ilipocheza na Yanga mwezi uliopita katika Raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa. Yanga ilitolewa kwa jumla ya mabao 2-1, ikilazimishwa sare ya 1-1 nyumbani kabla ya kwenda kufungwa 1-0 ugenini.
    Ingawa Yanga waliishangilia Kiyovu Sport ya Rwanda ilipocheza na Simba katika Raundi ya Kwanza, lakini kwa kuwa wapinzani wao hao wamefuzu- hawajatosheka wanataka kuendelea hadi watolewe ndipo nao waridhike.
    Simba na Yanga ni wapinzani wa jadi wa enzi na enzi, lakini kushangilia timu za wapinzani wa wapinzani wao rasmi kuliibuka mwaka 1993, kwenye Uwanja wa Uhuru, zamani Taifa, Dar es Salaam.
    Simba ilikuwa inacheza Fainali ya Kombe la CAF dhidi ya Stella Abidjan ya Ivory Coast, ukiwa mchezo wa marudiano, baada ya ule wa awali kulazimisha sare ugenini.
    Hata hivyo, siku hiyo Simba walichapwa mabao mawili na pamoja na mashabiki wa Yanga kuwa kimya kwa muda mrefu kufuata itikadi ya uzalendo, lilipopigwa bao la pili na Boli Zozo, wakaanza kuimba; “Uzalendo umetushinda, uzalendo umetushinda”.
    Mizizi hiyo mibaya iliyofukiwa na Yanga mwaka 1993, Tanzania ikipoteza nafasi muhimu ya kutwaa taji kubwa la Afrika nyumbani, imeendelea kukomaa na sasa imefikia mashabiki wa Yanga wanavaa jezi nyekundu zaa Setif- ili tu kuikomoa Simba, bila ya kuzingatia historia ya klabu yao- kwamba chekundu chochote ni haramu kwao.       
     
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MASHABIKI WA YANGA KUNG'ARA NA JEZI ZA SETIF JUMAPILI TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top