• HABARI MPYA

    Friday, March 30, 2012

    LWIZA KUSIMAMIA EL MERREIKH, PLATINUM CL


    SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF) limemteua Alfred Kisongole Lwiza wa Mwanza kuwa Kamishna wa mechi ya Ligi ya Mabingwa (CL) kati ya El Merreikh ya Sudan na FC Platinum ya Zimbabwe.
    Mechi hiyo ya marudiano ya raundi ya kwanza itachezwa Aprili 7 mwaka huu kwenye Uwanja wa El Merreikh jijini Khartoum, Sudan kuanzia saa 2 kamili usiku. Katika mechi ya kwanza iliyochezwa wikiendi hii jijini Harare timu hizo zilitoka sare ya mabao 2-2.
    El Merreikh ni moja ya timu ambazo CAF iliziingiza moja kwa moja katika raundi ya kwanza. FC Platinum iliingia raundi ya kwanza baada ya kuing’oa Green Mamba ya Swaziland katika raundi ya awali.
    Katika hatua nyingine, Chama cha Soka Zimbabwe (ZIFA) kimeomba mechi ya kirafiki kati ya timu yake ya Taifa ya wanawake na Twiga Stars. Mechi hiyo itakayochezwa kati ya Aprili 28 au 29 mwaka huu jijini Harare.
    Mechi hiyo ni sehemu ya maandalizi ya timu ya Zimbabwe kwa ajili ya kutafuta tiketi ya kucheza Fainali za Nane za Kombe la Afrika kwa Wanawake (AWC) zitakazofanyika Novemba mwaka huu nchini Equatorial Guinea.
    Twiga Stars ambayo iko kambini mkoani Pwani tangu Machi 25 mwaka huu chini ya Kocha Charles Boniface Mkwasa nayo inajiwinda kwa fainali hizo ambapo itacheza mechi ya kwanza Mei 26 mwaka huu jijini Addis Ababa dhidi ya Ethiopia. Zimbabwe yenyewe inacheza na Senegal.  
    Machi 10 mwaka huu, Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara alizindua akaunti ya Twiga Stars kupitia Tigo Pesa kuichangia timu hiyo ili ishiriki vyema michuano ya AWC.
    Wachangiaji wa Twiga Stars wanatakiwa kutuma mchango wao kwenda namba 13389 ambapo kiwango cha juu kinachoweza kutumwa kwa muhamala (transaction) mmoja ni sh. 500,000. Katika uzinduzi huo, Waziri Dk. Mukangara alichangia sh. milioni moja.
    Wakati huo huo: Mtihani kwa ajili ya mawakala wa wachezaji wanaotambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) utafanyika Machi 31 mwaka huu saa 4 kamili asubuhi ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (FIFA).
    Watu watatu wamejitokeza kufanya mtihani huo utakaokuwa na sehemu mbili. Sehemu ya kwanza ni maswali kutoka FIFA wakati nyingine ni kutoka TFF.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: LWIZA KUSIMAMIA EL MERREIKH, PLATINUM CL Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top