• HABARI MPYA

    Tuesday, March 27, 2012

    REBECCA MALOPE KUTUA NA ZAWADI YA PASAKA DAR


    Rebecca Malope
    MALKIA wa muziki wa Injili nchini Afrika Kusini, Rebecca Malope, ameahidi kuwaletea Watanzania zawadi ya Pasaka atakapotumbuiza katika tamasha la nyimbo za Injili la Pasaka litakalofanyika Aprili 8 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Akizungumza jana kwa njia ya simu kutoka Afrika Kusini, Rebecca alisema amewaandalia zawadi nzuri mashabiki wa muziki wa Injili wa Tanzania, na akatoa mwito wajitokeze kwa wingi siku ya tukio ili kumshuhudia.
    "Naahidi kuwaletea Watanzania zawadi ya Pasaka... nimewaandalia vitu vipya ambavyo naamini watavifurahia," alisema Malope.
    Malope aliyezaliwa katika shamba la tumbaku Afrika Kusini, alisema katika tamasha hilo la Pasaka mwaka huu ataimba nyimbo mbalimbali zilizomo kwenye albamu zake.
    Rebecca amewahi kutamba na albamu za Saturday Nite (aliyoitoa Januari 1, 2009), Hlala Nami (Novemba 11, 2003), Siyabonga (Desemba 21, 2000), Free at Last (Novemba 18, 1997), African Classics (Mei 5, 2009) na Greatest Hits (Januari 10, 2006).
    Malope atakuwa mmoja kati waimbaji siku hiyo wakiwemo Rose Muhando, Solomon Mukubwa, Anastazia Mukabwa, Upendo Nkone, Upendo Kilahiro, Christina Shusho, Atosha Kissava, Mwinjilisti Faraja Ntaboba, Ephraim Sekeleti, Maryanne Tutuma, kundi la Glorious Celebration na kwaya ya Kinondoni Revival.
    Mwenyekiti wa Kamati inayoratibu tamasha hilo chini ya Kampuni ya Msama Promotions ya Dar es Salaam, Alex Msama, alisema Rebecca ataungana na waimbaji wa muziki wa Injili kutoka nchi jirani za Zambia, Kenya na Jamhuri ya Kidemokrasia na Congo (DRC).
    Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe. Baada ya kutikisa Uwanja wa Taifa, mashambulizi mengine yatahamia kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma Aprili 9 mwaka huu ambako mgeni rasmi atakuwa Naibu Spika, Job Ndugai.
    Tamasha la mwaka huu malengo yake makubwa ni kuchangisha fedha kwa ajili ya kuwasomesha watoto yatima na kuwasaidia mitaji wanawake wajane.
    Kiingilio katika tamasha hilo kimetengwa katika kategoria tatu na kitakuwa sh. 2,000 kwa watoto, sh. 5,000 kwa viti vya kawaida na viti maalumu sh. 10,000.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: REBECCA MALOPE KUTUA NA ZAWADI YA PASAKA DAR Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top