• HABARI MPYA

  Sunday, January 01, 2017

  HAJIB: TIMU ITAKAYOTOA OFA NZURI NDIYO ITANIPATA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM 
  MSHAMBULIAJI chipukizi wa kimataifa wa Tanzania, Ibrahim Hajib Migomba amerejea nchini jana na kusema kwamba atajiunga na timu itakayompa ofa nzuri kati ya Haras El Hodoud ya Misri na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.
  Akizungumza na Bin Zubeiry Sports - Online leo baada ya kuwasili nchini kutoka Misri alipokwenda kufanya majaribio klabu ya Haras El Hodoud, Hajib amesema kwamba anaweka mbele maslahi katika kuamua timu ya kujiunga nayo.
  Pamoja na kufuzu majaribio na vipimo vya afya Haras El Hodoud, lakini imeripotiwa Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini pia inatamaka mchezaji huyo wa Simba kwa kusaini naye mkataba moja kwa moja bila majaribio.
  Ibrahim Hajib akiwa na wachezaji wa Haras El Hodoud mjini Alexandria, Misri wiki hii

  Na akizungumzia hilo, Hajib amesema; “Ni kweli nimesikia hizo habari, na si Kaizer tu, timu nyingine kama mbili za Afrika Kusini nazo zimetangaza ofa. Kwanza ninamshukuru Mungu. Mungu ni mkubwa, sasa tusubiri haya maneno yawe vitendo ndiyo tufanye maamuzi,”.
  Kuhusu Haras, Hajib amesema kwamba amefanya mazungumzo ya awali na Haras El Hodoud na kufikia makubaliano, lakini kwanza wanatakiwa kumalizana na klabu yake ya sasa, Simba SC.
  “Ninamshukuru Mungu nimefurahia siku zangu chache za kuwa Alexandria, nilikuwa katika klabu nzuri, mazingira mazuri na wachezaji wenzangu kule wamenikubali mapema sana. Sasa baada ya yote, ninawasikilizia wao tu ni jinsi gani watalimalizia hili suala,”amesema.
  Kwa upande wake, Katibu wa Simba, Patrick Kahemele amesema klabu haijapokea ofa yoyote kutoka Haras El Hodoud wala taarifa ya majibu ya majaribio ya mchezaji. “Sisi wenyewe tunasikia tu kutoka kwenye vyombo vya habari kwamba Hajib kafuzu. Kwa hiyo tunasubiri majibu rasmi,”amesema. 
  Wakala anayeshughulikia mipango ya Hajib nchini Afrika Kusini, Rodgers Mathaba kwa upande wake alikiri juu ya mchezaji huyo kutakiwa na Kaizer Chiefs.
  “Ni kweli, Kaizer wanamtaka Hajib. Najua alikuwa Misri, nasubiri arejee Dar es Salaam nimpigie simu nizungumze naye. Tayari nimekwishazungumza na kocha Steve Khompela wa Kaizer,”alisema.
  Hajib alikuwa ana wiki nzuri ya majaribio Haras El Hodoud ikiwemo kufunga bao moja katika ushindi wa 4-0 kwenye mchezo wa kirafiki Ijumaa.
  Mathaba ndiye aliyempeleka Hajib Afrika Kusini kwa majaribio pia, klabu ya Lamontville Golden Arrows FC ya Ligi Kuu ya ABSA nchini humo na pamoja na kufuzu, wakamtaka arejee Simba kumalizia Mkataba ili baadaye aende kama mchezaji huru.
  Lakini sasa mambo yamebadilika na klabu za Afrika Kusini na Misri zipo tayari kumnunua Hajib kutoka Simba.   
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: HAJIB: TIMU ITAKAYOTOA OFA NZURI NDIYO ITANIPATA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top