• HABARI MPYA

    Friday, July 17, 2015

    SIMBA SC WAREJEA LEO DAR, ‘WAWAHI’ KOMBE LA KAGAME

    Na Princess Aasia, DAR ES SALAAM
    MABINGWA wa zamani wa Tanzania na Afrika Mashariki na Kati, Simba SC wanatarajiwa kurejea leo Dar es Salaam kutoka Lushoto, Tanga walipokuwa wameweka kambi kwa wiki mbili zilizopita.
    Simba SC wamemua kuvunja kambi yao ya Lushoto, kufuatia taarifa za kusogezwa mbele kwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kutoka Agosti hadi Septemba. 
    Awali, washindi hao wa pili wa Kombe la CAF (sasa Shirikisho) mwaka 1993, walipanga kwenda Zanzibar wakitoka Lushoto, lakini baada ya Ligi Kuu kusogezwa mbele, haijulikani hatua inayofuata kwao.
    Lakini inawezekana kikosi hicho cha Kocha Muingereza, Dylan Kerr kikaendelea na mazoezi hapa hapa Dar es Salaam.

    Kikosi cha Simba SC kinachotarajiwa kurejea leo Dar es Salaam ni makipa; Peter Manyika
    David Robert Kisu, Denis Deonis Richard na Ivo Mapunda, mabeki, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Hassan Ramadhani ‘Kessy’, Samih Hajji Nuhu, Hassan Isihaka, Murushid Juuko na Mohamed Fakih Khatib.
    Viungo ni Jonas Mkude, Said Ndemla, 
    Abdi Banda, Awadh Juma, Simon Sserenkuma, Peter Mwalyanzi na washambuliaji Mussa Hassan Mgosi, Ibrahim Hajib, Hamisi Kiiza, Elias Maguli, Issa Abdallah Ngoa, Emmanuel Alex Massawe, Michael Mgimwa, Mbaruku Yusuph na Saidi Issa.
    Benchi la ufundi limeongozwa na kocha Mkuu, Dylan Kerr, Kocha Msaidizi, Suleiman Matola, Kocha wa makipa Iddi Salim Abdul, Kocha wa viungo, Dusan Momcilovic na Daktari Yassin Gembe.
    Simba SC watatua leo Dar es Salaam wakati michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame inaanza kesho, wenyeji Tanzania Bara wakiwakilishwa na Yanga SC na Azam FC.
    Kufanya vibaya kwa Simba SC kwa miaka mitatu iliyopita katika Ligi Kuu, kumewafanya siyo tu wakose nafasi ya kucheza Kombe la Kagame, bali hata michano ya Afrika, yaani Kombe la Washindi na Ligi ya Mabingwa. 
    Lakini msimu huu, chini ya Rais wake, Evans Elieza Aveva- Simba SC imepania kurejesha heshima.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC WAREJEA LEO DAR, ‘WAWAHI’ KOMBE LA KAGAME Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top