![]() |
| Abdi Kassim 'Babbi' akishangilia bao lake jana katika ushindi wa 3-2 wa timu yake dhidi ya timu ya akina Diouf |
KIUNGO wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, Abdi Kassim Sadallah ‘Babbi’ amemshauri kocha mpya wa Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa kutowapuuza wachezaji wakongwe katika kikosi chake kama anataka mafanikio.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana kwa simu kutoka Malaysia anakocheza kwa sasa, Babbi amesema kwamba wachezaji wakongwe ni muhimu katika timu wakichanganywa na vijana kwa ajili ya uwezo wao.
“Nchi za wenzetu hazipuuzi wakongwe ndiyo maana zinafanikiwa. Angalia Uganda wametutoa katika CHAN, lakini kikosini walikuwa wana wakongwe kama Hassan Wasswa na Robert Ssentongo,”amesema.
![]() |
| Abdi Kassim ni Nahodha wa timu yake |
![]() |
| Abdi Kassim na wenzake wakishangilia ushindi wa jana |
Babbi ambaye jana aliiongoza timu yake, UiTM FC kuifunga mabao 3-2 Sabah FC inayoongozwa na Mwanasoka bora wa zamani Afrika, Msenegali El Hadji Diouf katika Ligi Kuu ya Malaysia amemshauri Mkwasa kutofanya mambo kwa kukariri, bali afuatilie maendeleo ya wachezaji huko wachezapo kujua uwezo wao.
“Mimi ninacheza huku ni mchezaji tegemeo na ninafunga na kutengeneza nafasi. Naamini bado nina uwezo wa kuisaidia timu yangu ya taifa. Lakini siitwi tu kwa sababu Babbi nilikuwepo tangu wakati wa Maximo (Marcio), lakini wamezingatia uwezo wangu?”amehoji Babbi.
“Kwa mfano leo tu tumeshinda 3-2 dhidi ya Sabah anayochezea Diouf na mimi nimefunga bao la mita 20 na kutoa pasi za mabao yote mengine mawili, je sifai kuisaidia timu yangu?” amehoji tena Babbi.
Babbi amesema kwamba iwapo ataitwa hata kikosi cha awali cha Taifa Stars ataitikia wito na anaamini atamdhihirishia uwezo kocha Mkwasa na kumrejesha kikosini.
“Kwanza huku ninapocheza nimejifunza vitu zaidi ambavyo vinanipa uwezo zaidi wa kuisaidia timu yangu,”amesema Babbi.
Aidha, Babbi ameponda dhana ya kwamba wachezaji wakongwe hawafai tena Taifa Stars akisema ni potofu na ndiyo imechangia kushuka kwa soka yetu hivi sasa.
“Mchezaji huonekana uwanjani, tatizo kwetu ukishacheza Simba na Yanga unambiwa mzee, hilo ndilo linatufanya tusiendelee na tunawaua wachezaji haraka kwa kauli ya uzee, wakati ukifika mchezaji mwenyewe utamuona anaweka viatu juu bila ya kuambiwa,”amesema.
Babbi ambaye pia anafahamika kama Ballack wa Unguja, akifananishwa na kiungo wa zamani wa kimataifa wa Ujerumani, Michael Ballack ndiye mchezaji wa kwanza kufunga bao katika Uwanja mpya wa Taifa, Dar es Salaam baada ya kufunguliwa mwaka 2007.
Babbi alifunga bao hilo Septemba 1, mwaka 2007 katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Uganda, The Cranes- enzi hizo Taifa Stars ikifundishwa na kocha Mbrazil, Marcio Maximo.
![]() |
| Abdi Kassim kushoto akifurahia maisha Malaysia |
![]() |
| Abdi Kassim jana alifunga na kutoa pasi za mabao mengine mawili ya timu yake |
Babbi aliibukia Mlandege ya Zanzibar mwaka 2002 kabla ya 2004 kuhamia Mtibwa Sugar ya Morogoro ambako alidumu hadi 2007 aliponunuliwa na vigogo wa Tanzania, Yanga SC.
Mwaka 2011 Babbi aliuzwa Dong Tam Long Anya Vietnam ambako alicheza hadi 2012 aliporejea nyumbani kujiunga na Azam FC.
Mwaka 2013, Babbi alikwenda KMKM kabla ya mapema mwaka jana kujiunga na UiTM FC ambayo ana mwaka nayo wa pili sasa.







.png)
0 comments:
Post a Comment