• HABARI MPYA

    Thursday, February 13, 2014

    HATIMA YA LOGARUSIC SIMBA SC...

    Na Renatus Mahima, Dar es Salaam
    IKIWA imebaki miezi mitatu kabla ya kumalizika kwa mkataba wa kocha wa Simba, Zdravko Logarusic, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya klabu hiyo, Zacharia Hans Poppe amesema hatma ya kocha huyo iko mikononi mwa kamati yao ya ufundi.
    Logarusic, raia wa Croatia mwenye umri wa miaka 51, ana mkataba wa miezi sita kuinoa Simba aliousaini mbele ya Poppe mjini hapa mchana wa Desemba 2 mwaka jana kabla ya kuanza rasmi kazi ya kukifundisha kikosi hicho cha Msimbazi akirithi mikoba ya mtangulizi wake, Alhaj Abdallah Athumani Seif 'King Kibadeni' aliyetimuliwa mara tu baada ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu huu.
    Kamati ya Ufundi itaamua; Kocha wa Simba SC, Zdravko Logarusic suala la kuendelea kuinoa timu hiyo litaamuliwa na Kamati ya Ufundi

    Aidha, katika mkataba huo, kuna kipengele ambacho kinatamka kwamba kocha huyo atapewa mkataba mrefu na mnono endapo timu ya Simba chini yake itafanya vizuri msimu huu.
    Akizungumza BIN ZUBEIRY mjini hapa leo mchana, Poppe amesema Kamati ya Ufundi ya Simba ndiyo itakayoamua hatma ya kocha huyo baada ya kufanya tathimini ya kazi yake. Kamati hiyo inaongozwa na mwenyekiti Damian Manembe na makamu wake, Ibrahim Masoud 'Maestro'.
    "Kamati yangu imekamilisha usajili wa wachezaji waliohitajika msimu huu, natambua makubaliano yetu na kocha huyo (Logarusic) lakini kamati yangu haina mamlaka ya kumchukulia hatua, kamati inayohusika na masuala ya ufundi ndiyo itaangalia kazi yake kabla ya kuamua kumpa mkataba mpya au kuachana naye," amesema Poppe.
    Logarusic aliikuta Simba ikiwa nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom ikiizidiwa pointi nne na wapinhzani wao wa jadi, Yanga waliokuwa vinara Yanga huku ikizidiwa pointi tatu na Mbeya City na Azam FC walikokuwa wakikamata nafasi za pili na tatu. 
    Sasa timu hiyo ambayo keshokutwa itashuka ugenini kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine kuvaana na wababe Mbeya City iko nafasi ya nne ikiwa na pointi 31 baada ya kushikwa kwa sare ya bao moja na mabingwa wa Tanzania Bara 1999 na 2000, Mtibwa Sugar kabla ya kupata kipigo kisichotarajiwa cha bao 1-0 kutoka kwa Mgambo Shooting katika mechi mbili zilizopita.
    Simba sasa inazidiwa pointi tano na vinara Azam FC, nne dhidi ya Yanga na tatu dhidi ya wapinzani wao wa kesho Mbeya City huku ikiwa imecheza mechi moja zaidi ya Azam na Yanga. 
    Ukali wa Loga akiwa mazozeni na hata wakati wa mechi, kunaonekana wazi kuwa tatizo kati ya wa wachezaji wa Simba na kocha huyo wa zamani wa mabingwa wa Kenya, Gor Mahia.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HATIMA YA LOGARUSIC SIMBA SC... Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top